< 2 Wakorintho 2 >
1 Basi nimeamua nisiwatembelee tena kuwatia huzuni.
Hivyo nilikusudia moyoni mwangu nisifanye ziara nyingine yenye kuwaumiza ninyi.
2 Maana nikiwahuzunisha ninyi, basi, ni nani atakayenifariji? Ni walewale niliowahuzunisha!
Kwa kuwa kama nikiwahuzunisha ninyi, ni nani aliyebaki wa kunifurahisha isipokuwa ninyi ambao nimewahuzunisha?
3 Ndiyo maana niliwaandikia—sikutaka kuja kwenu na kuhuzunishwa na ninyi ambao ndio mngepaswa kuwa furaha yangu. Nina hakika kwamba, mimi nikifurahi, ninyi nyote pia mnafurahi.
Niliandika hivyo kama nilivyofanya, ili nikija nisihuzunishwe na wale watu ambao wangenifanya nifurahi. Nina uhakika na ninyi nyote, kwamba wote mngeshiriki furaha yangu.
4 Nilipowaandikia hapo awali katika hali ya huzuni na sikitiko moyoni na kwa machozi mengi, haikuwa kwa ajili ya kuwahuzunisha ninyi, bali kwa ajili ya kuwaonyesheni kwamba nawapenda mno.
Kwa maana niliwaandikia kutokana na dhiki kubwa na kutaabika sana kwa moyo wangu tena kwa machozi mengi, shabaha yangu si ili niwasababishe mhuzunike bali kuwaonyesha kina cha upendo wangu kwenu.
5 Ikiwa kuna mtu aliyemhuzunisha mwingine, hakunihuzunisha mimi—ila amewahuzunisha ninyi nyote, na sipendi kuwa mkali zaidi.
Lakini ikiwa mtu yeyote amesababisha huzuni, kwa kiasi fulani hakunihuzunisha mimi kama vile alivyowahuzunisha ninyi nyote, ili nisiwe mkali kupita kiasi.
6 Adhabu aliyokwisha pata kutoka kwa wengi wenu inamtosha.
Adhabu hii aliyopewa na wengi inamtosha.
7 Iliyobakia ni afadhali kwenu kumsamehe mtu huyo na kumpa moyo ili asije akahuzunika mno na kukata tamaa kabisa.
Basi sasa badala yake, inawapasa kumsamehe na kumfariji, ili asigubikwe na huzuni kupita kiasi.
8 Kwa hiyo nawasihi: mwonyesheni kwamba mnampenda.
Kwa hiyo, nawasihi, mpate kuuthibitisha tena upendo wenu kwa ajili yake.
9 Madhumuni yangu kuandika ile barua yalikuwa kutaka kujua kama mko tayari kutii katika kila jambo.
Sababu ya kuwaandikia ni kuona kama mngeweza kushinda hilo jaribio na kutii katika kila jambo.
10 Mkimsamehe mtu, nami pia ninamsamehe. Maana ninaposamehe—kama kweli ninacho cha kusamehe—nasamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,
Kama ninyi mkimsamehe mtu yeyote, mimi pia nimemsamehe. Kile nilichosamehe, kama kulikuwa na kitu chochote cha kusamehe, nimekwisha kusamehe mbele ya Kristo kwa ajili yenu,
11 ili tusimpe nafasi Shetani atudanganye; maana twaijua mipango yake ilivyo.
ili Shetani asitushinde. Kwa maana hatuachi kuzijua hila zake.
12 Nilipofika Troa kuhubiri Habari Njema ya Kristo, nilikuta mlango u wazi kwa ajili ya kazi ya Bwana.
Basi nilipofika Troa kuhubiri Injili ya Kristo na kukuta kwamba Bwana alikuwa amenifungulia mlango,
13 Lakini nilifadhaika sana kwa kutomkuta ndugu yetu Tito. Ndiyo maana niliwaaga wote pale nikaenda Makedonia.
bado nilikuwa sina utulivu akilini mwangu kwa sababu sikumkuta ndugu yangu Tito huko. Hivyo niliagana nao nikaenda Makedonia.
14 Lakini, shukrani kwa Mungu anayetuongoza daima katika msafara wa ushindi wa Kristo. Yeye hutufanya tuueneze ukweli wa Kristo kama harufu nzuri, kila mahali.
Lakini Mungu ashukuriwe, yeye ambaye siku zote hutufanya tuandamane kwa ushindi tukiwa ndani ya Kristo. Naye kupitia kwetu hueneza kila mahali harufu nzuri ya kumjua yeye.
15 Maana sisi ni kama harufu nzuri ya ubani ambayo Kristo anamtolea Mungu, harufu nzuri inayofikia wote wanaookolewa na wanaopotea.
Kwa maana sisi kwa Mungu ni harufu nzuri ya manukato ya Kristo miongoni mwa wale wanaookolewa na kwa wale wanaopotea.
16 Kwa wale wanaopotea, harufu hiyo ni kifo; lakini kwa wale wanaookolewa, harufu hiyo ni uhai. Nani basi, awezaye kushiriki katika kazi ya namna hiyo?
Kwa wale wanaopotea, sisi ni harufu ya mauti iletayo mauti; lakini kwa wale wanaookolewa, sisi ni harufu nzuri iletayo uzima. Ni nani awezaye mambo hayo?
17 Sisi si kama wengine ambao hufanya biashara na ujumbe wa Mungu; sisi tunahubiri kwa unyofu mbele ya Mungu, kama watu tuliotumwa na Mungu, tukiwa tumeungana na Kristo.
Tofauti na watu wengine wengi, sisi hatufanyi biashara na Neno la Mungu kwa ajili ya kupata faida. Kinyume chake, katika Kristo tunalisema Neno la Mungu kwa unyoofu, kama watu tuliotumwa kutoka kwa Mungu.