< 1 Timotheo 3 >
1 Msemo huu ni wa kweli: mtu akitaka kuwa kiongozi katika kanisa, huyo anatamani kazi nzuri.
2 Basi, kiongozi wa kanisa anapaswa awe mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu; ni lazima awe mkarimu na anayeweza kufundisha;
3 asiwe mlevi au mtu wa matata, bali awe mpole, apendaye amani; asiwe mtu wa kupenda fedha;
4 anapaswa awe mtu awezaye kuongoza vema nyumba yake, na kuwafanya watoto wake wawe watii kwa heshima yote.
5 Maana kama mtu hawezi kuongoza vema nyumba yake, atawezaje kulitunza kanisa la Mungu?
6 Mtu ambaye hajakomaa bado katika imani asifanywe kuwa kiongozi katika kanisa, asije akajaa majivuno na kuhukumiwa kama vile Ibilisi alivyohukumiwa.
7 Anapaswa awe mwenye sifa njema kati ya watu walio nje ya kanisa, ili asije akalaumiwa na kuanguka katika mtego wa Ibilisi.
8 Wasaidizi katika kanisa wanapaswa pia kuwa watu wenye tabia njema na wanyofu; wasiwe wanywaji mno wa divai au wenye tamaa ya fedha;
9 wanapaswa kuzingatia kwa dhamiri njema ukweli wa ndani wa imani.
10 Ni lazima kwanza wathibitishwe, na wakionekana kuwa wanafaa, basi, watoe huduma yao.
11 Wake zao wanapaswa pia kuwa na tabia njema, wasiowasengenya watu, wenye kiasi na waaminifu katika mambo yote.
12 Msaidizi katika kanisa lazima awe na mke moja tu, na awezaye kuongoza vema watoto wake na nyumba yake.
13 Maana wasaidizi wanaofanya kazi yao vizuri hujipatia msimamo mzuri, na wanaweza kusema bila hofu juu ya imani yao katika Kristo Yesu.
14 Ninakuandikia barua hii nikiwa na matumaini ya kuja kwako hivi karibuni.
15 Lakini kama nikicheleweshwa, basi, barua hii itakufahamisha mwenendo tunaopaswa kuwa nao katika nyumba ya Mungu, ambayo ni kanisa la Mungu aliye hai, na ambalo ni nguzo na msingi wa ukweli.
16 Hakuna mashaka yoyote juu ya ukuu wa siri ya dini yetu: Alionekana katika umbo la kibinadamu alithibitishwa na Roho kuwa ni mwadilifu, akaonekana na malaika. Alihubiriwa kati ya mataifa, aliaminiwa popote ulimwenguni, akachukuliwa juu mbinguni katika utukufu.