< 1 Wathesalonike 1 >

1 Mimi Paulo, Silwano na Timotheo tunawaandikia ninyi jumuiya ya kanisa la Thesalonike, ambao ni watu wake Mungu Baba, na wa Bwana Yesu Kristo.
Paulo, Silvano na Timotheo: Kwa kanisa la Wathesalonike, ninyi mlio ndani ya Mungu Baba yetu na ndani ya Bwana Yesu Kristo: Neema iwe kwenu na amani.
2 Tunamshukuru Mungu daima kwa ajili yenu ninyi nyote na kuwakumbukeni daima katika sala zetu.
Siku zote tunamshukuru Mungu kwa ajili yenu ninyi nyote, tukiwataja kwenye maombi yetu daima.
3 Maana, mbele ya Mungu Baba yetu, twakumbuka jinsi mnavyoonyesha imani yenu kwa matendo, jinsi upendo wenu unavyowawezesha kufanya kazi kwa bidii, na jinsi tumaini lenu katika Bwana wetu Yesu Kristo lilivyo thabiti.
Tunaikumbuka daima kazi yenu ya imani mbele za Mungu aliye Baba yetu, taabu yenu katika upendo na saburi yenu ya tumaini katika Bwana wetu Yesu Kristo.
4 Ndugu, twajua kwamba Mungu anawapenda na kwamba amewateua muwe watu wake,
Ndugu zetu mpendwao na Mungu, kwa kuwa tunajua kwamba Mungu amewachagua,
5 maana wakati tulipowahubirieni ile Habari Njema haikuwa kwa maneno tu, bali pia kwa nguvu na kwa Roho Mtakatifu, tukiwa na hakika kwamba ujumbe huo ulikuwa wa kweli. Mnajua jinsi tulivyoishi pamoja nanyi; tuliishi kwa manufaa yenu.
kwa sababu ujumbe wetu wa Injili haukuja kwenu kwa maneno matupu bali pia ulidhihirishwa katika nguvu na katika Roho Mtakatifu, tena ukiwa na uthibitisho kamili, kama vile ninyi wenyewe mnavyojua jinsi tulivyoenenda katikati yenu kwa ajili yenu.
6 Ninyi mlifuata mfano wetu, na kumwiga Bwana. Ingawa mliteswa sana, mliupokea ujumbe huo kwa furaha itokayo kwa Roho Mtakatifu.
Nanyi mkawa wafuasi wetu na wa Bwana, ingawa mlipata mateso mengi, mlilipokea lile Neno kwa furaha katika Roho Mtakatifu.
7 Kwa hiyo ninyi mmekuwa mfano mzuri kwa waumini wote wa Makedonia na Akaya.
Hivyo ninyi mkawa kielelezo kwa waumini wote katika Makedonia na Akaya.
8 Maana, kutokana na bidii yenu ujumbe wa Bwana umesikika si tu huko Makedonia na Akaya, bali imani yenu kwa Mungu imeenea popote. Tena hatuhitaji kusema zaidi.
Kwa maana kutoka kwenu neno la Bwana limesikika, si katika Makedonia na Akaya tu, bali pia imani yenu katika Mungu imejulikana kila mahali kiasi kwamba hatuna haja ya kusema lolote kwa habari yake.
9 Watu hao wanazungumza juu ya ziara yetu kwenu: jinsi mlivyotukaribisha, jinsi mlivyoziacha sanamu mkamgeukia Mungu aliye hai na wa kweli,
Kwa maana watu wa maeneo hayo wenyewe wanaeleza jinsi mlivyotupokea na jinsi mlivyomgeukia Mungu mkaacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli
10 na sasa mwamngojea Mwanae ashuke kutoka mbinguni, Yesu, ambaye Mungu alimfufua kutoka wafu, na ambaye anatuokoa katika ghadhabu ya Mungu inayokuja.
na ili kumngojea Mwanawe kutoka mbinguni, ambaye Mungu alimfufua kutoka kwa wafu: yaani, Yesu, yeye aliyetuokoa kutoka ghadhabu inayokuja.

< 1 Wathesalonike 1 >