< 1 Yohana 2 >
1 Watoto wangu, ninawaandikieni mambo haya, kusudi msitende dhambi. Lakini, ikijatokea mtu akatenda dhambi, tunaye mmoja ambaye hutuombea kwa Baba, ndiye Yesu Kristo aliye mwadilifu kabisa.
2 Kristo ndiye sadaka iondoayo dhambi zetu; wala si dhambi zetu sisi tu, bali pia dhambi za ulimwengu wote.
3 Tukizitii amri za Mungu, basi, tunaweza kuwa na hakika kwamba tunamjua.
4 Mtu akisema kwamba anamjua, lakini hazitii amri zake, basi mtu huyo ni mwongo, na ukweli haumo ndani yake.
5 Lakini mtu yeyote anayeshika neno la Mungu, huyo ndiye aliye na upendo kamili wa Mungu ndani yake. Hivi ndivyo tunavyoweza kuwa na hakika kwamba tunaungana naye:
6 mtu yeyote anayesema kwamba ameungana na Mungu, anapaswa kuishi kama alivyoishi Yesu Kristo.
7 Wapenzi wangu, amri hii ninayowaandikieni si amri mpya; ni amri ileile ya zamani mliyokuwa nayo tangu mwanzo. Amri hiyo ya zamani ni ule ujumbe mliousikia.
8 Hata hivyo, amri hii ninayowaandikieni ni amri mpya, na ukweli wake unaonekana ndani ya Kristo na ndani yenu pia. Maana giza linatoweka, na mwanga wa ukweli umekwisha anza kuangaza.
9 Yeyote asemaye kwamba yumo katika mwanga, lakini anamchukia ndugu yake, mtu huyo bado yumo gizani.
10 Yeyote ampendaye ndugu yake, yuko katika mwanga, na hamna chochote ndani yake kiwezacho kumkwaza mtu mwingine.
11 Lakini anayemchukia ndugu yake, yumo gizani; anatembea gizani, na hajui anakokwenda, maana giza limempofusha.
12 Ninawaandikieni ninyi watoto, kwa kuwa dhambi zenu zimeondolewa kwa jina la Kristo.
13 Nawaandikieni ninyi kina baba kwani mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo, Nawaandikieni ninyi vijana kwa sababu mmemshinda yule Mwovu.
14 Nawaandikieni ninyi watoto, kwa sababu mnamjua Baba. Nawaandikieni ninyi kina baba, kwa kuwa mnamjua yeye ambaye amekuwako tangu mwanzo. Nawaandikieni ninyi vijana kwa sababu mna nguvu; neno la Mungu limo ndani yenu na mmemshinda yule Mwovu.
15 Msiupende ulimwengu, wala chochote kilicho cha ulimwengu. Mtu anayeupenda ulimwengu, upendo wa Baba hauwezi kuwamo ndani yake.
16 Vitu vyote vya ulimwengu-tamaa mbaya za mwili, vitu wanavyoviona watu na kuvitamani, majivuno yasababishwayo na mali-vyote hivyo havitoki kwa Baba, bali vyatoka kwa ulimwengu.
17 Ulimwengu pamoja na vitu vyake vyote vyenye kutamanika unapita; lakini mtu atendaye atakalo Mungu, anaishi milele. (aiōn )
18 Watoto, mwisho u karibu! Mlikwisha sikia kwamba adui wa Kristo anakuja, na sasa adui wengi wa Kristo wamekwisha fika, na hivyo twajua kwamba mwisho u karibu.
19 Watu hao wametokea kati yetu lakini hawakuwa kweli wa kwetu na ndiyo maana walituacha; Kama wangalikuwa wa kwetu, wangalibaki nasi. Lakini waliondoka, wakaenda zao, kusudi ionekane wazi kwamba hawakuwa kamwe wa kwetu.
20 Ninyi, lakini, mlipata kumiminiwa Roho Mtakatifu na Kristo, na hivyo mnaujua ukweli.
21 Basi, nawaandikieni, si kwa kuwa hamuujui ukweli, bali kwa sababu mnaujua; na pia mnajua kwamba uongo wowote haupatikani katika ukweli.
22 Mwongo ni nani? Ni yule anayekana kwamba Yesu ni Masiha. Mtu wa namna hiyo ni adui wa Kristo—anamkana Baba na Mwana.
23 Maana yeyote anayemkana Mwana, anamkana pia Baba; na yeyote anayemkubali Mwana, anampata Baba pia.
24 Basi, ujumbe ule mliousikia tangu mwanzo na ukae mioyoni mwenu. Kama ujumbe huo mliousikia tangu mwanzo ukikaa ndani yenu, basi, mtaishi daima katika umoja na Mwana na Baba.
25 Na ahadi aliyotuahidia sisi ndiyo hii: uzima wa milele. (aiōnios )
26 Nimewaandikieni mambo haya kuhusu wale wanaotaka kuwapotosha ninyi.
27 Lakini, kwa upande wenu ninyi, Kristo aliwamiminieni Roho wake. Na kama akiendelea kukaa ndani yenu, hamhitaji kufundishwa na mtu yeyote. Maana Roho wake anawafundisheni kila kitu na mafundisho yake ni ya kweli, si ya uongo. Basi shikeni mafundisho ya huyo Roho na kubaki katika muungano na Kristo.
28 Naam, watoto, kaeni ndani yake kusudi wakati atakapotokea tuwe hodari bila kuwa na sababu ya kujificha kwa aibu Siku ya kuja kwake.
29 Mnajua kwamba Kristo ni mwadilifu kabisa; basi, mnapaswa kujua pia kwamba kila mtu atendaye mambo adili ni mtoto wa Mungu.