< 1 Wakorintho 2 >
1 Ndugu, mimi nilipokuja kwenu sikuwahubiria siri ya ujumbe wa Mungu kwa ufasaha wa lugha, au kwa hekima ya binadamu.
2 Nilipokuwa kwenu niliamua kutojua chochote kile isipokuwa tu kumjua Yesu Kristo; naam, Kristo aliyesulubiwa.
3 Nilipokuwa kwenu nilikuwa dhaifu, natetemeka kwa hofu nyingi.
4 Hotuba zangu na mahubiri yangu sikuyatoa kwa maneno ya kuvutia na ya hekima, bali kwa uthibitisho mwingi na nguvu ya Roho.
5 Nilifanya hivyo kusudi imani yenu ipate kutegemea nguvu ya Mungu, na si hekima ya binadamu.
6 Hata hivyo, sisi tunatumia lugha ya hekima kwa wale waliokomaa kiroho; lakini hekima hiyo si ya hapa duniani, wala si ya watawala wa dunia hii ambao wako katika mkumbo wa kupotea. (aiōn )
7 Hekima tunayotumia ni hekima ya siri ya Mungu, hekima iliyofichika, ambayo Mungu aliiazimia tangu mwanzo kwa ajili ya utukufu wetu. (aiōn )
8 Ni hekima ambayo watawala wa dunia hii hawakuielewa; maana wangalielewa, hawangalimsulubisha Bwana wa utukufu. (aiōn )
9 Lakini, ni kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: “Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao.”
10 Hayo ndiyo mambo Mungu aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake. Maana Roho huchunguza kila kitu hata mambo ya ndani kabisa ya Mungu.
11 Nani awezaye kujua mambo ya ndani ya mtu isipokuwa roho yake mtu huyo? Hali kadhalika, hakuna ajuaye mambo ya Mungu isipokuwa Roho wa Mungu.
12 Sasa sisi hatukuipokea roho ya ulimwengu, bali tumepokea Roho atokaye kwa Mungu ili atuwezeshe kujua yale tuliyojaliwa na Mungu.
13 Basi sisi twafundisha, si kwa maneno tuliyofundishwa kwa hekima ya binadamu, bali kwa maneno tuliyofundishwa na Roho, tukifafanua mambo ya kiroho kwa walio na huyo Roho.
14 Mtu wa kidunia hapokei mambo ya Roho wa Mungu. Kwake mtu huyo mambo hayo ni upumbavu mtupu; yanapita akili yake; maana yanaweza tu kutambuliwa kwa msaada wa Roho.
15 Lakini mtu aliye na huyo Roho anaweza kubainisha ubora wa kila kitu, naye mwenyewe hahukumiwi na mtu mwingine.
16 Maandiko yasema: “Nani awezaye kuifahamu akili ya Bwana? Nani awezaye kumshauri?” Lakini sisi tunayo akili ya Kristo.