< 1 Wakorintho 16 >

1 Sasa, yahusu ule mchango kwa ajili ya watu wa Mungu: fanyeni kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia.
Basi kuhusu changizo kwa ajili ya watakatifu: Kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia, fanyeni vivyo hivyo.
2 Kila Jumapili kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha kadiri ya mapato yake, ili kusiwe na haja ya kufanya mchango wakati nitakapokuja.
Siku ya kwanza ya kila juma, kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha, kulingana na mapato yake na fedha hizo aziweke akiba, ili nitakapokuja pasiwe na lazima ya kufanya mchango.
3 Wakati nitakapokuja kwenu, nitawatuma wale mtakaowachagua miongoni mwenu wapeleke barua na zawadi zenu Yerusalemu.
Kwa hiyo nitakapowasili, nitawapa wale mtakaowachagua barua za kuwatambulisha, ili kuwatuma wapeleke zawadi zenu huko Yerusalemu.
4 Kama itafaa nami niende, basi, watakwenda pamoja nami.
Kama ikionekana ni vyema na mimi niende, basi hao watu watafuatana nami.
5 Nitakuja kwenu, baada ya kupitia Makedonia—maana nataraji kupitia Makedonia.
Baada ya kupitia Makedonia nitakuja kwenu, maana ninakusudia kupitia Makedonia.
6 Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari yangu kokote nitakakokwenda.
Huenda nitakaa nanyi kwa muda, au hata kukaa nanyi kipindi chote cha baridi, ili mweze kunisaidia katika safari yangu, popote niendapo.
7 Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari. Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu.
Kwa maana sitaki niwaone sasa na kupita tu; natarajia kuwa nanyi kwa muda wa kutosha, kama Bwana akipenda.
8 Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste.
Lakini nitakaa Efeso mpaka wakati wa Pentekoste,
9 Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi.
kwa maana mlango mkubwa umefunguliwa kwangu kufanya kazi yenye matunda, nako huko kuna adui wengi wanaonipinga.
10 Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi.
Ikiwa Timotheo atakuja kwenu, hakikisheni kwamba hana hofu yoyote akiwa nanyi, kwa sababu anafanya kazi ya Bwana, kama mimi nifanyavyo.
11 Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja na ndugu zetu.
Basi asiwepo mtu atakayekataa kumpokea. Msafirisheni kwa amani ili aweze kunijia tena. Namtarajia pamoja na ndugu.
12 Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara itakapowezekana.
Basi kwa habari za ndugu yetu Apolo, nimemsihi kwa bidii aje kwenu pamoja na hao ndugu. Ingawa alikuwa hapendi kabisa kuja sasa, lakini atakuja apatapo nafasi.
13 Kesheni, simameni imara katika imani, muwe hodari na wenye nguvu.
Kesheni, simameni imara katika imani, fanyeni kiume, kuweni mashujaa kuweni hodari.
14 Kila mfanyacho kifanyike kwa upendo.
Fanyeni kila kitu katika upendo.
15 Ndugu, mnaifahamu jamaa ya Stefana; wao ni watu wa kwanza kabisa kuipokea imani ya Kikristo katika Akaya, na wamejitolea kuwatumikia watu wa Mungu. Ninawasihi ninyi ndugu zangu,
Ninyi mnajua kwamba watu wa nyumbani mwa Stefana ndio waliokuwa wa kwanza kuamini katika Akaya, nao wamejitoa kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu. Ndugu nawasihi,
16 muufuate uongozi wa watu kama hao, na uongozi wa kila mtu afanyaye kazi na kutumikia pamoja nao.
mjitie katika kuwahudumia watu kama hawa na kila mmoja aingiaye kwenye kazi na kuifanya kwa bidii.
17 Nafurahi sana kwamba Stefana, Fortunato na Akaiko wamefika; wamelijaza pengo lililokuwako kwa kutokuwako kwenu.
Nilifurahi wakati Stefana, Fortunato na Akaiko walipofika, kwa sababu wamenipatia yale niliyopungukiwa kutoka kwenu.
18 Wameiburudisha roho yangu na yenu pia. Kwa hiyo inafaa kuwakumbuka watu wa namna hii.
Kwa kuwa waliiburudisha roho yangu na zenu pia. Watu kama hawa wanastahili kutambuliwa.
19 Makanisa yote ya Asia yanawasalimuni. Akula na Priskila pamoja na watu wote wa Mungu walio nyumbani mwao wanawasalimuni sana katika Bwana.
Makanisa ya Asia yanawasalimu. Akila na Prisila, pamoja na kanisa lililoko nyumbani kwao wanawasalimu sana katika Bwana.
20 Ndugu wote wanawasalimuni. Nanyi salimianeni kwa ishara ya mapendo ya Mungu.
Ndugu wote walioko hapa wanawasalimu. Salimianeni kwa busu takatifu.
21 Mimi Paulo nawasalimuni, nikiandika kwa mkono wangu mwenyewe.
Mimi, Paulo, naandika salamu hizi kwa mkono wangu mwenyewe.
22 Yeyote asiyempenda Bwana, na alaaniwe. MARANA THA—BWANA, njoo!
Kama mtu yeyote hampendi Bwana Yesu Kristo, na alaaniwe. Bwana wetu, njoo.
23 Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.
Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.
24 Mapendo yangu yawe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu.
Upendo wangu uwe nanyi nyote katika Kristo Yesu. Amen.

< 1 Wakorintho 16 >