< Zekaria 8 >

1 Neno la Yahwe wa majeshi likanijia kusema,
Neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote likanijia tena.
2 “Yahwe wa majeshi asema hivi: Nina huzuni kwa ajili ya Sayuni kwa wivu mkuu na ninamaumivu kwa hasira nyingi!
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Nina wivu sana kwa ajili ya Sayuni, ninawaka wivu kwa ajili yake.”
3 Yahwe wa majeshi asema hivi: Nitairudia Sayuni nami nitakaa kati ya Yerusalemu, kwa kuwa Yerusalemu itaitwa mji wa kweli na mlima wa Yahwe wa majeshi utaitwa Mlima Mtakatifu!
Hili ndilo asemalo Bwana: “Nitarudi Sayuni na kufanya makao Yerusalemu. Kisha Yerusalemu utaitwa mji wa kweli, mlima wa Bwana Mwenye Nguvu Zote utaitwa Mlima Mtakatifu.”
4 Yahwe wa majeshi asema hivi: Kwa mara nyingine tena kutakuwa na vikongwe katika mitaa ya Yerusalemu, na kila mtu ataitaji mkongojo mkononi mwake kwa vile alivyo mzee.
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Kwa mara nyingine tena wazee wanaume kwa wanawake walioshiba umri wataketi katika barabara za Yerusalemu, kila mmoja akiwa na mkongojo wake mkononi kwa sababu ya umri wake.
5 Pia mitaa ya mji itajazwa na vijana wa kiume na kike wachezao.
Barabara za mji zitajaa wavulana na wasichana wanaocheza humo.”
6 Yahwe wa majeshi asema hivi: ikiwa jambo laonekana haliwezekani katika macho ya masalia ya watu hawa katika siku hizo, je haliwezekani pia machoni pangu? - asema Yahwe.
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Mambo haya yanaweza kuonekana ya ajabu kwa mabaki ya watu wakati huo, lakini yaweza kuwa ya ajabu kwangu?” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
7 Yahwe wa majeshi asema hivi: Tazama, nipo tayari kuwaokoa watu wangu kutoka nchi ya mawio na ya machweo ya jua!
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Nitawaokoa watu wangu kutoka nchi za mashariki na magharibi.
8 Kwa maana nitawarudisha tena, nao wataishi ndani ya Yerusalemu, hivyo watakuwa watu wangu tena, nami nitakuwa Mungu wao katika kweli na utakatifu!
Nitawarudisha waje kuishi Yerusalemu, watakuwa watu wangu nami nitakuwa mwaminifu na wa haki kwao kama Mungu wao.”
9 Yahwe wa majeshi asema hivi: Ninyi mnaoendelea kusikia maneno yaleyale yaliyotoka katika vinywa vya manabii msingi wa nyumba yangu ulipowekwa - hii nyumba yangu, Yahwe wa majeshi: Itieni nguvu mikono yenu ili hekalu lijengwe.
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Ninyi ambao sasa mnasikia maneno haya yanayozungumzwa na manabii ambao walikuwepo wakati wa kuwekwa kwa msingi wa nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu Zote, mikono yenu na iwe na nguvu ili Hekalu liweze kujengwa.
10 Kwani kabla ya siku hizo hakuna mazao yaliyokusanywa na yeyote ndani yake, hakukuwa na faida siyo kwa mtu hata mnyama, na hakukuwa na amani kutoka kwa adui kwa kila aliyekwenda au kuja. Nilimfanya kila mtu kuwa kinyume cha mwenzake.
Kabla ya wakati huo, hapakuwepo na ujira kwa mtu wala mnyama. Hakuna mtu aliyeweza kufanya shughuli yake kwa usalama kwa sababu ya adui yake, kwa kuwa nilikuwa nimemfanya kila mtu adui wa jirani yake.
11 Lakini sasa haitakuwa kama mwanzo, nitakuwa pamoja na masalia ya watu hawa - asema Yahwe wa majeshi.
Lakini sasa sitawatendea mabaki ya watu hawa kama nilivyowatenda zamani,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
12 Kwani mbegu za amani zitapandwa; mzabibu unaokua utatoa matunda yake na nchi itatoa mazao yake; anga zitatoa umande, kwa maana nitawapa masalia ya watu hawa kumilki haya yote.
“Mbegu itakua vizuri, mzabibu utazaa matunda yake, ardhi itatoa mazao yake, na mbingu zitadondosha umande wake. Vitu hivi vyote nitawapa mabaki ya watu kama urithi wao.
13 Ulikuwa mfano wa laana kwa mataifa mengine, enyi nyumba ya Yuda na nyumba ya Israeli. Hivyo nitawaokoa nanyi mtakuwa baraka. Msiogope; haya mikono yenu itiwe nguvu!
Jinsi mlivyokuwa kitu cha laana katikati ya mataifa, ee Yuda na Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka. Msiogope, bali iacheni mikono yenu iwe na nguvu.”
14 Kwa maana Yahwe wa majeshi asema hivi: Kama nilivyopanga kuwatenda mabaya babu zenu walipochokoza hasira yangu - asema Yahwe wa majeshi - na wala sikujuta,
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Kama nilivyokuwa nimekusudia kuleta maangamizi juu yenu, wakati baba zenu waliponikasirisha na sikuonyesha huruma,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote,
15 ndivyo nitakavyoazimia kuutenda mema tena Yerusalemu na nyumba ya Yuda katika siku hizi! Msiogope!
“hivyo sasa nimeazimia kufanya mema tena kwa Yerusalemu na Yuda. Msiogope.
16 Haya ndiyo mambo mnayopaswa kufanya: Kasemeni kweli, kila mtu na jirani yake. Hukumuni kwa haki, usawa na amani katika malango yenu.
Haya ndiyo mtakayoyafanya: Semeni kweli kila mtu kwa mwenzake, na mtoe hukumu ya kweli na haki kwenye mahakama zenu,
17 Na asiwepo miongoni mwenu anayeazimu uovu moyoni mwake dhidi ya jirani yake, wala kuvutwa na viapo vya uongo; kwani haya yote ndiyo mambo ninayoyachukia! - asema Yahwe.”
usipange mabaya dhidi ya jirani yako, wala msipende kuapa kwa uongo. Nayachukia yote haya,” asema Bwana.
18 Kisha neno la Yahwe wa majeshi likanijia kusema,
Neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote likanijia tena.
19 “Yahwe wa majeshi asema hivi: Mifungo ya mwezi wa nne, mwezi wa tano, mwezi wa saba na mwezi wa kumi itakuwa nyakati za furaha ya kila aina, kwa nyumba ya Yuda! Kwa hiyo pendeni kweli na amani!
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Saumu za miezi ya nne, tano, saba na kumi itakuwa sikukuu za furaha na za shangwe kwa Yuda. Kwa hiyo uipende kweli na amani.”
20 Yahwe wa majeshi asema hivi: Watu watakuja tena, hata wanaoishi miji mingine.
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Mataifa mengi na wakazi wa miji mingi watakuja,
21 Watu wa mji mmoja watakwenda mji mwingine na kusema, “Haya twendeni haraka mbele ya Yahwe tukaombe na kumtafuta Yahwe wa majeshi! Sisi wenyewe tunakwenda pia.
na wenyeji wa mji mmoja watakwenda kwenye mji mwingine na kusema, ‘Twende mara moja na tukamsihi Bwana, na kumtafuta Bwana Mwenye Nguvu Zote. Mimi mwenyewe ninakwenda.’
22 Watu wengi na mataifa yenye nguvu yatakuja kumtafuta Yahwe wa majeshi huko Yerusalemu na kuomba upendeleo kwa Yahwe!
Pia watu wa kabila nyingi na mataifa yenye nguvu yatakuja Yerusalemu kumtafuta Bwana Mwenye Nguvu Zote na kumsihi.”
23 Yahwe wa majeshi asema hivi: Katika siku hizo watu kumi kutoka katika kila lugha na taifa watashika upindo wa kanzu zenu na kusema, “Haya sisi nasi tutakwenda pamoja nanyi, kwani tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nayi!”
Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: “Katika siku hizo watu kumi kutoka lugha zote na mataifa, watangʼangʼania upindo wa joho la Myahudi mmoja na kusema, ‘Twende pamoja nawe kwa sababu tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nawe.’”

< Zekaria 8 >