< Zekaria 7 >
1 Mwaka wa minne wa utawala mfalme Dario, siku ya nne ya mwezi wa Kisleu(ambao ni mwezi wa tisa), neno la Yahwe lilimjia Zekaria kusema.
Katika mwaka wa nne wa utawala wa Mfalme Dario, neno la Bwana lilimjia Zekaria siku ya nne ya mwezi wa tisa, mwezi wa Kisleu.
2 Watu wa Betheli wamemtuma Shareza, Regemu Meleki na watu wao kuomba mbele ya uso wa Yahwe.
Watu wa Betheli walikuwa wamemtuma Shareza na Regem-Meleki pamoja na watu wao, kumsihi Bwana
3 Wakaongea na makuhani waliokuwa katika nyumba ya Yahwe wa majeshi na kwa manabii; wakasema, “Je niomboleze katika mwezi wa tano kwa njia ya kufunga, kama nilivyofanya miaka mingi hii?”
kwa kuwauliza makuhani wa nyumba ya Bwana Mwenye Nguvu Zote na manabii, “Je, imempasa kuomboleza na kufunga katika mwezi wa tano, kama ambavyo nimekuwa nikifanya kwa miaka mingi?”
4 Ndipo neno la Yahwe wa majeshi liliponijia kusema,
Kisha neno la Bwana Mwenye Nguvu Zote likanijia kusema:
5 “Ongea na watu wote wa nchi na makuhani uwaambie, “Mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba katika hii miaka sabini, je kweli mlifunga kwa ajili yangu?
“Waulize watu wote wa nchi na makuhani, ‘Je, mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na wa saba kwa miaka sabini iliyopita, mlifunga kweli kwa ajili yangu?
6 Na mlipokula na kunywa, hamkula na kunywa kwa ajili yenu wenyewe?
Na mlipokuwa mkila na kunywa, je, hamkuwa mnasherehekea kwa ajili ya nafsi zenu?
7 Je hayo siyo maneno aliyosema Yahwe kwa vinywa vya manabii wa zamani, mlipokuwa bado mnaishi Yerusalemu na miji ya kandokando yenye mafanikio na iliyokaa Negebu, na upande wa magharibi chini ya vilima?”
Je, haya sio maneno ya Bwana aliyosema kupitia manabii waliotangulia, wakati Yerusalemu pamoja na miji inayoizunguka ilipokuwa katika hali ya utulivu na ya mafanikio, wakati Negebu na Shefala zikiwa zimekaliwa na watu?’”
8 Neno la Yahwe likamjia Zekaria kusema,
Neno la Bwana likamjia tena Zekaria:
9 “Yahwe wa majeshi asema hivi, 'Hukumuni kwa haki, uaminifu wa agano, na rehema. Kila mtu na amtendee hivi ndugu yake.
“Hivi ndivyo asemavyo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Fanyeni hukumu za haki, onyesheni rehema na huruma ninyi kwa ninyi.
10 Juu ya mjane na yatima, mgeni, na masikini - usiwanyanyase, na asiwepo miongoni mwenu anayepanga madhara yoyote dhidi ya mwingine mioyoni mwenu.
Msimwonee mjane wala yatima, mgeni wala maskini. Msiwaziane mabaya mioyoni mwenu ninyi kwa ninyi.’
11 Lakini waliyashupaza mabega yao na hawakujari. Waliziba masikio yao ili wasisikie.
“Lakini wakakataa kusikiliza, wakanipa kisogo kwa ukaidi na kuziba masikio yao.
12 Waliifanya mioyo yao kuwa migumu kama mwamba ili wasiisikie sheria au neno la Yahwe wa majeshi. Alipeleka ujumbe kwa watu nyakati za zamani kwa Roho wake, kwa vinywa vya manabii. Lakini watu hawakusikia, hivyo Yahwe wa majeshi aliwakasirikia sana.
Wakaifanya mioyo yao migumu kama jiwe gumu na hawakuisikiliza sheria au maneno ambayo Bwana Mwenye Nguvu Zote aliyatuma kwa njia ya Roho wake kupitia manabii waliotangulia. Kwa hiyo Bwana Mwenye Nguvu Zote alikasirika sana.
13 Hata ikawa alipoita hawakusikia. Vilevile,” asema Yahwe wa majeshi, “wataniita, lakini sitasikiliza.
“‘Wakati nilipoita, hawakusikiliza, kwa hiyo walipoita, sikusikiliza,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
14 Kwa maana nitawatawanya kwa upepo wa kisurisuri katika mataifa yote ambayo hawajawai kuyaona, na baada yao nchi itakuwa wazi. Kwa kuwa hakuna hata mmoja atakayepita au kukaa katika hiyo nchi kwa kuwa wameigeuza nchi yao yenye kupendeza kuwa isiyofaa.
‘Niliwatawanya kwa upepo wa kisulisuli miongoni mwa mataifa yote, mahali ambapo walikuwa wageni. Nchi ikaachwa ukiwa nyuma yao kiasi kwamba hakuna aliyeweza kuingia au kutoka. Hivi ndivyo walivyoifanya ile nchi iliyokuwa imependeza kuwa ukiwa.’”