< Zekaria 12 >
1 Hili ni tamko la neno la Yahwe kwa Israeli - Bwana asema, azitandaye mbingu na kuweka msingi wa dunia, aiumbaye roho ya mtu ndani yake,
Hili ni neno la Bwana kuhusu Israeli. Bwana, yeye azitandaye mbingu, awekaye misingi ya dunia na aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake, asema:
2 “Tazama, nitaifanya Yerusalemu kuwa kikombe kiwafadhaishacho watu wote wamzungukao. Itakuwa hivyo hivyo pia kwa Yuda wakati wa kuhusuriwa kwa Yerusalemu.
“Nitakwenda kufanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumbisha mataifa yote yanayoizunguka. Yuda utazingirwa kwa vita na Yerusalemu pia.
3 Katika siku hiyo, nitaifanya Yerusalemu kuwa jiwe zito kwa watu wa jamaa zote. Kila atakayejaribu kuliinua jiwe hilo atajihumiza sana, na mataifa yote ya dunia yatakusanyika kinyume cha mji huo.
Katika siku hiyo, wakati mataifa yote ya dunia yatakapokusanyika dhidi yake, nitaufanya Yerusalemu kuwa jabali lisilosogezwa kwa mataifa yote. Wote watakaojaribu kulisogeza watajiumiza wenyewe.
4 Katika siku hiyo asema Yahwe - nitampiga kila farasi kwa ushangao na kila mpanda farasi kwa wendawazimu. Nitaiangalia nyumba ya Yuda kwa upendeleo na nami nitawapiga kwa upofu farasi wa majeshi.
Katika siku hiyo nitampiga kila farasi kwa hofu ya ghafula, naye ampandaye nitampiga kwa uwazimu,” asema Bwana. “Nitalielekeza jicho langu la ulinzi juu ya nyumba ya Yuda, nami nitawapofusha farasi wote wa mataifa.
5 Ndipo watawala wa Yuda watakapojisemea mioyoni mwao, 'Wakaao Yerusalemu ndio nguvu yetu kwa sababu ya Yahwe wa majeshi, Mungu wao.'
Kisha viongozi wa Yuda watasema mioyoni mwao, ‘Watu wa Yerusalemu wana nguvu kwa sababu Bwana Mwenye Nguvu Zote ni Mungu wao.’
6 Katika siku hiyo nitawafanya watawala wa Yuda kuwa kama mitungi ya moto katika miti na kama miali ya moto kati ya nafaka isimamayo, kwani utateketeza watu wote walio karibu upande wao wa kulia na kushoto. Yerusalemu atakaa mahali pake tena.
“Katika siku hiyo nitawafanya viongozi wa Yuda kuwa kama kigae cha moto ndani ya lundo la kuni, kama mwenge uwakao kati ya miganda. Watateketeza kulia na kushoto mataifa yote yanayowazunguka, lakini Yerusalemu utabaki salama mahali pake.
7 Yahwe ataziokoa hema za Yuda kwanza, ili kwamba utukufu ya nyumba ya Daudi na utukufu wa wale waishio Yerusalemu hautazidi sehemu iliyosalia ya Yuda.
“Bwana atayaokoa makao ya Yuda kwanza, ili heshima ya nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu isiwe kubwa zaidi kuliko ile ya Yuda.
8 Katika siku hiyo Yahwe atakuwa mtetezi wa wakao Yerusalemu, na siku hiyo waliodhaifu miongoni mwao watakuwa kama Daudi, wakati nyumba ya Daudi watakuwa kama Mungu, kama malaika wa Yahwe mbele yao.
Katika siku hiyo, Bwana atawakinga wale waishio Yerusalemu, ili kwamba aliye dhaifu kupita wote miongoni mwao awe kama Daudi, nayo nyumba ya Daudi itakuwa kama Mungu, kama Malaika wa Bwana akiwatangulia.
9 “Itakuwa kwamba katika siku hiyo nitaanza kuyaharibu mataifa yote yajayo kinyume cha Yerusalemu.
Katika siku hiyo nitatoka kuangamiza mataifa yote yatakayoshambulia Yerusalemu.
10 Lakini nitamwaga roho ya huruma na kuiombea nyumba ya Daudi na wakao Yerusalemu, hivyo wataniangalia mimi, waliomchoma kwa mkuki. Wataniombolezea, kama amwombolezeaye mwana wa pekee; watamwombolezea kwa uchungu sana kama aombolezaye kifo cha mzaliwa wa kwanza.
“Nami nitamiminia nyumba ya Daudi na wakazi wa Yerusalemu roho ya neema na maombi. Watanitazama mimi, yule waliyemchoma. Nao watamwombolezea kama mtu anayemwombolezea mwanawe wa pekee na kusikitika kwa uchungu kama anayemsikitikia mzaliwa wake wa kwanza wa kiume.
11 Katika siku hiyo maombolezo huko Yerusalemu yatakuwa kama maombolezo ya Hadadi Rimoni katika tambarare za Megido.
Katika siku hiyo kilio kitakuwa kikubwa Yerusalemu, kama kilio cha Hadad-Rimoni katika tambarare ya Megido.
12 Nchi itaomboleza, kila ukoo peke yao. Ukoo wa nyumba ya Daudi utakuwa peke yake na wake zao watakuwa peke yao mbali na wanaume. Ukoo wa nyumba ya Nathani utakuwa peke yao na wake zao watakuwa peke yao mbali na waume.
Nchi itaomboleza, kila ukoo peke yake, nao wake zao peke yao. Ukoo wa nyumba ya Daudi na wake zao, ukoo wa nyumba ya Nathani na wake zao,
13 Ukoo wa nyumba ya Lawi utakuwa peke yao na wake zao watakuwa peke yao mbali na waume. Ukoo wa Washimei utakuwa peke yao na wake zao watakuwa peke yao mbali na waume.
ukoo wa nyumba ya Lawi na wake zao, ukoo wa Shimei na wake zao,
14 Kila ukoo uliosalia - kila mmoja utakuwa peke yake na wake watakuwa pekee mbali na waume.
na koo zote zilizobaki na wake zao.