< Tito 2 >
1 Lakini wewe yaseme yale yanayoendana na maelekezo ya kuaminika.
2 Wazee wawe na kiasi, heshima, busara, imani safi, katika upendo, na katika uvumilivu.
3 Vilevile wanawake wazee lazima daima wajioneshe wao wenyewe kama wenye kujiheshimu, na sio wasengenyaji. Lazima wasiwe watumwa wa pombe.
4 Wanapaswa kufundisha yaliyo mazuri ili kuwaandaa wasichana kwa busara kuwapenda waume zao na watoto wao.
5 Wanapaswa kuwafundisha kuwa na busara, wasafi, watunzaji wazuri wa nyumba zao, na watii kwa waume zao wenyewe. Inawalazimu kufanya mambo haya ili kwamba neno la Mungu lisitukanwe.
6 katika namna iyo hiyo, watieni moyo vijana wa kiume wawe na busara.
7 Katika njia zote jiwekeni wenyewe kuwa mfano katika kazi nzuri; na mfundishapo, onesheni uadilifu na heshima.
8 Ongeeni ujumbe wenye afya na usio na dosari, ili kwamba yeyote apingaye aaibishwe kwa sababu hana baya la kusema juu yetu.
9 Watumwa na wawatii mabwana zao katika kila kitu. Wanapaswa kuwafurahisha na sio kubishana nao.
10 Hawapaswi kuiba. Badala yake, wanapaswa kuonesha imani yote nzuri ili kwamba katika njia zote wayapambe mafundisho yetu kumhusu Mungu mwokozi wetu.
11 Kwa kuwa neema ya Mungu imeonekana kwa watu wote.
12 Inatufundisha kukataa mambo yasiyo ya kimungu na tamaa za kidunia. Inatufundisha kuishi kwa busara, kwa haki, na katika njia za kimungu kwa wakati huu. (aiōn )
13 Wakati tunatarajia kupokea tumaini letu lenye baraka, mwonekano wa utukufu wa Mungu wetu mkuu na Mwokozi wetu Yesu Kristo.
14 Yesu alijitoa mwenyewe kwa ajili yetu ili kutukomboa kutoka katika uasi na kutufanya wasafi, kwa ajili yake, watu maalumu walio na hamu ya kufanya kazi nzuri.
15 Yaseme na kuyasisitiza mambo haya. Kemea kwa mamlaka yote. Usikubali mtu yeyote akupuuze.