< Wimbo wa Sulemani 5 >

1 Nimekuja katika bustani yangu, dada yangu, bibi arusi wangu; Nimekusanya udi wangu na manukato yangu. Nimekula mziga wangu wa asali na asali yangu; Nimekunywa mvinyo wangu pamoja na maziwa yangu. Marafiki wanazungumza na wapenzi Kuleni, marafiki; kunyweni na mlewe na mapenzi. Mwanamke mdogo akizungumza mwenyewe
Nimekuja kwenye bustani yangu, dada yangu, bibi arusi wangu; nimekusanya manemane yangu pamoja na kikolezo changu. Nimekula sega langu la asali na asali yangu; nimekunywa divai yangu na maziwa yangu. Marafiki Kuleni, enyi marafiki, mnywe; kunyweni ya kutosha, ee wapenzi.
2 Nilikuwa nimelala, lakini moyo wangu ulikuwa umeamka katika ndoto. Sauti ya mpenzi wangu yabisha na kusema, “Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu, hua wangu, wangu usiye na doa, kwa kuwa kichwa changu kimelowa na matone, nywele zangu na unyevu wa usiku.”
Nililala lakini moyo wangu ulikuwa macho. Sikiliza! Mpenzi wangu anabisha: “Nifungulie, dada yangu, mpenzi wangu, hua wangu, asiye na hitilafu. Kichwa changu kimeloa umande, na nywele zangu manyunyu ya usiku.”
3 “Nimevua joho langu; lazima nilivae tena? Nimeosha miguu yangu; lazima ni ichafue?”
Nimevua joho langu: je, ni lazima nivae tena? Nimenawa miguu yangu: je, ni lazima niichafue tena?
4 Mpenzi wangu anaeka mkono wake kwenye kitasa, na moyo wangu ukawaka kwa ajili yake.
Mpenzi wangu aliweka mkono wake kwenye tundu la komeo; moyo wangu ulianza kugonga kwa ajili yake.
5 Nimeamka kumfungulia mlango mpenzi wangu; mikono yangu ikawa yamiminika na udi, vidole vyangu na unyevu wa udi, katika komeo la mlango.
Niliinuka kumfungulia mpenzi wangu, mikono yangu ikidondosha manemane, vidole vyangu vikitiririka manemane, penye vipini vya komeo.
6 Nimemfungulia mlango mpenzi wangu, lakini mpenzi wangu aligeuka na kwenda. Moyo wangu ukadidimia; nikakosa tumaini. Nikamtafuta, lakini sikumpata; nikamuita, lakini hakunijibu.
Nilimfungulia mpenzi wangu, lakini mpenzi wangu alishaondoka; alikuwa amekwenda zake. Moyo wangu ulishuka kwa kuondoka kwake. Nilimtafuta lakini sikumpata. Nilimwita lakini hakunijibu.
7 Walinzi waliokuwa wakizunguka mjini walinipata mimi; walinipiga chini na kunijeruhi; askari katika ukuta walichukua nguo yangu ya juu. Mwanamke mdogo akizungumza na wanawake wa mji
Walinzi walinikuta walipokuwa wakifanya zamu za ulinzi mjini. Walinipiga, wakanijeruhi, wakaninyangʼanya joho langu, hao walinzi wa kuta!
8 Ninataka uhaidi, mabinti wa Yerusalemu, kwamba mkimuona mpenzi wangu, mwambie ninaumwa sababu ya upendo wangu kwake. Wanawake wa mji wakizungumza na mwanamke mdogo
Enyi binti za Yerusalemu, ninawaagiza: kama mkimpata mpenzi wangu, mtamwambia nini? Mwambieni ninazimia kwa mapenzi.
9 Mpenzi wako ana ubora gani kuliko mwanaume mwengine, wewe uliye mzuri miongoni mwa wanawake? Kwanini mpenzi wako bora kuliko mpenzi mwengine, hadi utuulize tuweke nadhiri kama hii? Mwanamke mdogo akizungumza na wanawake wa mji
Je, mpendwa wako ni bora kuliko wengine namna gani, wewe uliye mzuri kupita wanawake wote? Je, mpendwa wako ni mzuri kuliko wengine, namna gani, hata unatuagiza hivyo?
10 Mpenzi wangu amenawiri na ana ng'aa, kati ya wanaume elfu kumi.
Mpenzi wangu anangʼaa, tena ni mwekundu, wa kuvutia miongoni mwa wanaume kumi elfu.
11 Kichwa chake ni dhahabu safi; nywele zake ni laini na nyeusi kama kunguru.
Kichwa chake ni dhahabu safi kuliko zote, nywele zake ni za mawimbi na ni nyeusi kama kunguru.
12 Macho yake ni kama ya hua pembezoni ya vijito vya maji, yameoshwa na maziwa, yameundwa kama mikufu.
Macho yake ni kama ya hua kandokando ya vijito vya maji, aliyeogeshwa kwenye maziwa, yaliyopangwa kama vito vya thamani.
13 Mashavu yake ni kama vitanda vya manukato, vinavyotoa arufu ya marashi. Midomo yake nni nyinyoro, inayo tiririka udi.
Mashavu yake ni kama matuta ya vikolezo yakitoa manukato. Midomo yake ni kama yungiyungi inayodondosha manemane.
14 Mikono yake ni ya mianzi ya dhahabu iliyo zungushiwa mikufu; tumbo lake ni pembe lililo funikwa yakuti samawi.
Mikono yake ni fimbo za dhahabu iliyopambwa kwa krisolitho. Mwili wake ni kama pembe ya ndovu iliyongʼarishwa iliyopambwa na yakuti samawi.
15 Miguu yake ni nguzo za marimari, iliyo ekwa juu ya dhahabu safi; muonekano wake ni kama Lebanoni, mizuri kama mierezi.
Miguu yake ni nguzo za marmar zilizosimikwa katika vitako vya dhahabu safi. Sura yake ni kama Lebanoni, bora kama miti yake ya mierezi.
16 Mdomo wake ni mtamu; ni mzuri sana. Huyu ni mpenzi wangu, na huyu ni rafiki yangu, mabinti wa Yerusalemu.
Kinywa chake chenyewe ni utamu, kwa ujumla yeye ni wa kupendeza. Huyu ndiye mpenzi wangu, huyu ndiye rafiki yangu, ee binti za Yerusalemu.

< Wimbo wa Sulemani 5 >