< Ruth 2 >
1 Basi Elimeleki mme wa Naomi, alikuwa na jamaa aitwaye Boazi, aliye kuwa tajiri, na mtu maarufu.
Basi Naomi alikuwa na jamaa wa upande wa mume wake, kutoka ukoo wa Elimeleki, mtu maarufu ambaye aliitwa Boazi.
2 Ruth, Mmoabu, alimwambia Naomi, “Ngoja niende nikakusanye mabaki ya chakula katika shamba. Nitamfuata yeyote ambaye nitapata kibali machoni pake.” Hivyo naomi akamwambia, “Nenda, mwanangu.”
Ruthu, Mmoabu, akamwambia Naomi, “Nitakwenda mashambani nikaokote mabaki ya nafaka nyuma ya yule nitakayepata kibali machoni pake.” Naomi akamwambia, “Nenda, binti yangu.”
3 Ruth alienda kuvuna kwenye shamba akiwafuata kwa nyuma wavunaji. Na kumbe ile sehemu ya shamba ilikuwa ni mali ya Boazi, aliyekuwa na mahusiano na Elimeleki.
Basi akaenda, akaokota mabaki ya nafaka mashambani nyuma ya wavunaji. Ikatokea kwamba alijikuta anafanya kazi kwenye shamba lililokuwa mali ya Boazi, ambaye alitoka kwenye ukoo wa Elimeleki.
4 Tazama, Boazi alikuja kutoka bethelehemu na kuwaambia wavunaji, “Yahweh awe nanyi.” Wakamjibu, “Yahweh akubariki.”
Papo hapo Boazi akarudi kutoka Bethlehemu, akawasalimu wavunaji, akasema, “Bwana awe nanyi!” Nao wakamjibu, “Bwana akubariki.”
5 Ndipo Boazi akamwambia mtumishi wake aliyekuwa akiwasimamia wavunaji, “Vipi bwana huyu msichana ni wa nani?”
Boazi akamuuliza msimamizi wa wavunaji, “Je, yule mwanamwali ni wa nani?”
6 Mtumishi msimamizi wa wavunaji alijibu na kusema, “Ni msichana Mmoabu aliyerudi na Naomi kutoka nchi ya Moabu.
Msimamizi akamjibu, “Ni yule Mmoabu aliyerudi kutoka nchi ya Moabu pamoja na Naomi.
7 Aliniambia, 'Tafadhali niruhusu kuvuna na kukusanya mabaki ya wavunaji.' Hivyo alikuja na ameendelea kuvuna toka asubuhi mpaka sasa, isipokuwa amepumzika kidogo katika nyumba.”
Yeye aliomba, ‘Tafadhali niruhusu niokote na kukusanya miongoni mwa miganda nyuma ya wavunaji.’ Naye ameshinda shambani tangu asubuhi pasipo kupumzika, isipokuwa kwa muda mfupi kivulini.”
8 Kisha Boazi akamwambia Ruth, “Unanisikiliza, mwanangu? Usiende kuvuna kwenye shamba lingine; usiondoke shambani kwangu. Badala yake, baki hapa na wasichana wangu wa kazi.
Kisha Boazi akamwambia Ruthu, “Binti yangu, nisikilize. Usiende kuokota mabaki ya mavuno katika shamba lingine, na usiondoke hapa. Kaa hapa na hawa watumishi wangu wa kike.
9 Yaelekeze tu macho yako kwenye shamba ambamo wanaume wanavuna na ufuatie nyuma ya wanawake wengine. Je, sikuwaelekeza wanaume wasikuguse? Na upatapo kiu, unaweza kwenda kunywa maji kwenye mtungi ambao wanaume wamejaza.”
Angalia shamba wanaume wanamovuna, ufuate nyuma yao. Nimewaamuru wanaume hawa wasikuguse. Wakati wowote ukiona kiu, nenda kwenye mitungi ukanywe maji waliyoyateka wanaume hawa.”
10 Ndipo akapiga magoti mbele ya Boazi, na kugusisha kichwa chake chini. Akamwambia, “Kwa nini nimepata kibali machoni pako, hata unijali mimi mgeni?”
Kwa ajili ya hili, akasujudu mpaka nchi, akamwambia, “Jinsi gani nimepata kibali machoni pako, hata ukanijali mimi mgeni?”
11 Boazi akajibu na kumwabia, “Nimekwisha ambiwa, yote uliyo yafanya tangu mme wako afariki. Umewaacha baba yako, mama, na nchi uliyozaliwa kumfuata mama mkwe wako na kuja kwa watu usiowajua.
Boazi akamjibu, “Nimeambiwa yote uliyomtendea mama mkwe wako tangu mume wako alipofariki, na jinsi ulivyomwacha baba yako na mama yako na nchi yako ulimozaliwa, ukaja kuishi na watu ambao hukuwafahamu awali.
12 Yahweh akulipe kwa matendo yako. Yahweh akulipe kwa wingi, Mungu wa Israeli, ambaye chini ya mbawa zake umepata kimbilio.”
Bwana na akulipe kwa yale uliyoyatenda. Ubarikiwe kwa wingi na Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye umekimbilia mabawani mwake.”
13 Ruth akasema, “Nipate kibali machoni pako, bwana wangu, kwa kuwa umenifariji, na umeongea wema kwangu, ingawa mimi sio mmoja wa watumishi wako wa kike.”
Kisha Ruthu akasema, “Naomba niendelee kupata kibali machoni pako, bwana wangu. Kwa maana umenifariji na umezungumza kwa ukarimu na mjakazi wako, hata ingawa mimi si bora kama mmoja wa watumishi wako wa kike.”
14 Wakati wa chakula Boazi alimwambia Ruth, “Njoo hapa, ule baadhi ya mikate, na uchovye kipande katika divai.” Alikaa kando ya wavunaji, na Boazi akampatia kiasi cha nafaka zilizo kaangwa. Ruth alikula mpaka alipotosheka na kusaza.
Wakati wa chakula, Boazi akamwambia Ruthu, “Karibia hapa. Kula mkate na uchovye ndani ya siki.” Alipoketi pamoja na wavunaji, akampa nafaka zilizookwa. Akala kiasi alichotaka na kusaza.
15 Alipoinuka kwenda kuvuna, Boazi aliamuru vijana wake, akisema, “Mwacheni avune hata katika masuke, na msimwambie lolote baya.
Alipoinuka ili kuokota mabaki ya nafaka, Boazi akawaagiza watu wake, “Hata kama atakusanya kati ya miganda, msimzuie.
16 Na pia muachie baadhi ya masuke katika vifurushi kwa ajili yake, na muaache ili ayavune. Msimkemee.”
Badala yake, toeni masuke katika miganda, mwachieni ayaokote, na msimkemee.”
17 Kwa hiyo alivuna mpaka jioni. Kisha akatenganisha nafaka na majani ambayo amevuna, nazo nafaka zilikuwa kama efa moja ya shairi.
Basi Ruthu akaokota masazo shambani hata jioni. Akatwanga ile shayiri aliyokusanya, ikajaa efa moja.
18 Akazibeba na kwenda katika mji. Ndipo mama mkwe wake aliona kile alichokivuna. Ruth pia alimletea mama mkwe wake nafaka zilizo kaangwa alizobakiza kwenye chakula chake.
Akaibeba na kuelekea mjini, naye mama mkwe wake akaona jinsi alivyoweza kuokota nafaka nyingi. Pia Ruthu akachukua kile alichobakiza baada ya kula na kushiba, akampa.
19 Mama mkwe wake akamwambia, “Umevunia wapi uliko vunia leo? Ulienda kufanyia wapi kazi? abarikiwe mtu aliye kusaidia.” Ndipo Ruth akamwambia mama mkwe wake kuhusu mtu aliye miliki shamba alilokuwa akifanya kazi. Alimwambia, “Jina la mtu ambaye alimiliki shamba nililokuwa nikifanya kazi ni Boazi.”
Basi mkwewe akamuuliza, “Je, umeokota wapi leo? Umefanya kazi wapi? Abarikiwe mtu yule aliyekujali.” Ndipo Ruthu akamwambia mama mkwe wake juu ya yule ambaye yeye alikuwa amefanyia kazi katika shamba lake. Akasema, “Yule mtu niliyefanyia kazi kwake leo, anaitwa Boazi.”
20 Naomi akamwambia Ruth, “Abarikiwe na Yahweh, ambaye hakuondoa uaminifu wake kwa walio hai na wafu.” Naomi akamwambia, “Huyo mtu ni jamaa wa karibu nasi, ni jamaa yetu mkombozi.”
Naye Naomi akamwambia mkwewe, “Bwana ambariki! Hakuacha kuonyesha fadhili zake kwa walio hai na kwa waliokufa.” Pia akamwambia, “Huyo mtu ni mmoja wa jamaa yetu wa karibu anayestahili kutukomboa.”
21 Ruth Mmoabu akamwambia, “Ni kweli, aliniambia, 'Ukae karibu na vijana wangu wa kiume mpaka watakapo maliza mavuno yangu yote.'”
Kisha Ruthu, Mmoabu, akasema, “Hata aliniambia, ‘Kaa pamoja na watumishi wangu mpaka watakapomaliza kuvuna nafaka yangu yote.’”
22 Naomi akamwambia Ruth mke wa mtoto wake wa kiume, “Ni vizuri, mwanangu, kuwa uende pamoja na wasichana wake wa kazi, ili kwamba usije pata madhara yeyote katika shamba lolote.”
Kisha Naomi akamwambia Ruthu mkwewe, “Binti yangu, itakuwa vyema wewe ufuatane na wasichana wake, kwa sababu katika shamba la mtu mwingine wanaweza kukudhuru.”
23 Kwa hiyo alikaa karibu na wafanyakazi wa kike ili avune mpaka mwisho wa mavuno ya shayiri na mavuno ya ngano. Na alikuwa akiishi pamoja na mama mkwe wake.
Kwa hivyo Ruthu akafuatana na watumishi wa kike wa Boazi, akaokota mpaka mwisho wa mavuno ya shayiri na ya ngano. Naye aliishi na mama mkwe wake.