< Warumi 7 >
1 Au hamjui, ndugu zangu (kwa kuwa naongea na watu wanaoijua sheria), kwamba sheria humtawala mtu anapokuwa hai?
2 Kwa maana mwanamke aliyeolewa amefungwa na sheria kwa yule mme wake anapokuwa hai, lakini ikiwa mme wake atakufa, atakuwa amewekwa huru kutoka sheria ya ndoa.
3 Hivyo basi, wakati mme wake angali akiishi, ikiwa anaishi na mwanamme mwingine, ataitwa mzinzi. Lakini ikiwa mme wake akifa, yuko huru dhidi ya sheria, hivyo hatakuwa mzinzi ikiwa anaishi na mwanamme mwingine.
4 Kwa hiyo, ndugu zangu, ninyi pia mlifanywa wafu kwa sheria kwa njia ya mwili wa Kristo. Imekuwa hivi ili mpate kuunganishwa na mwingine, kwake yeye ambaye alifufuliwa kutoka wafu ili tuweze kumzalia Mungu matunda.
5 Kwa maana tulipokuwa katika hali ya mwili, tamaa za dhambi ziliamshwa katika viungo vyetu kwa njia ya sheria na kuizalia mauti matunda.
6 Lakini sasa tumefunguliwa kutoka katika sheria. Tumeifia ile hali iliyotupinga. Ili sisi tupate kutumika katika hali mpya ya Roho, na si katika hali ya zamani ya andiko.
7 Tusemeje basi? Sheria ni dhambi? La hasha. Hata hivyo, nisingelitambua dhambi, isingelikuwa kwa njia ya sheria. Kwa kuwa nisingelijua kutamani kama sheria isingelisema, “Usitamani.”
8 Lakini dhambi ilipata nafasi kwa ile amri na ikaleta ndani yangu kila aina ya kutamani. Kwa maana dhambi pasipo sheria imekufa.
9 Nami nilikuwa hai hapo kwanza bila sheria, lakini ilipokuja ile amri, dhambi ilipata uhai, nami nikafa.
10 Ile amri na ambayo ingelileta uzima iligeuka kuwa mauti kwangu.
11 Kwa maana dhambi ilipata nafasi kwa ile amri na ikanidanganya. Kupitia ile amri, iliniua.
12 Hivyo sheria ni takatifu, na ile amri ni takatifu, ya yaki, na njema.
13 Hivyo basi ile iliyo njema ilikuwa mauti kwangu mimi? Isiwe hivyo kamwe. Lakini dhambi, ili ionekane kuwa ni dhambi hasa kupitia ile njema, ilileta mauti ndani yangu. Hii ilikuwa ili kwamba kupitia ile amri, dhambi izidi kuwa mbaya mno.
14 Kwa maana twajua ya kuwa sheria asili yake ni ya rohoni, lakini mimi ni mtu wa mwilini. Nimeuzwa chini ya utumwa wa dhambi.
15 Maana nifanyalo, silielewi dhahiri. Kwa kuwa lile nilipendalo kutenda, silitendi, na lile nilichukialo, ndilo ninalolitenda.
16 Lakini kama nikilitenda lile nisilolipenda, nakubaliana na sheria ya kuwa sheria ni njema.
17 Lakini sasa si mimi nafsi yangu ninayetenda hilo, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
18 Kwa maana najua ya kuwa ndani yangu, yaani ndani ya mwili wangu, halikai jambo jema. Kwa kuwa tamaa ya lililo jema imo ndani yangu, lakini silitendi.
19 Kwa maana lile jema nilipendalo silitendi, bali lile ovu nisilolipenda ndilo nilitendalo.
20 Sasa kama natenda lile nisilolipenda, si mimi binafsi nilitendaye, bali ni ile dhambi ikaayo ndani yangu.
21 Nimefahama, tena, imo kanuni ndani yangu ya kutaka kutenda lililo jema, lakini uovu hakika umo ndani yangu.
22 Kwa maana naifurahia sheria ya Mungu kwa utu wa ndani.
23 Lakini naona kanuni iliyo tofauti katika viungo vya mwili wangu. Inapiga vita dhidi ya kanuni mpya katika akili zangu. Inanifanya mimi mateka kwa kanuni ya dhambi iliyo katika viungo vya mwili wangu.
24 Mimi ni mtu wa huzuni! Ni nani atakayeniokoa na mwili huu wa mauti?
25 Lakini shukrani kwa Mungu kwa Yesu Kristo Bwana wetu! Hivyo basi. Mimi mwenyewe kwa akili zangu naitumikia sheria ya Mungu. Bali, kwa mwili naitumikia kanuni ya dhambi.