< Warumi 5 >
1 Kwa kuwa tumehesabiwa haki kwa njia ya imani, tuna amani na Mungu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.
2 Kupitia yeye sisi pia tuna fursa kwa njia ya imani katika neema hii ambayo ndani yake tunasimama. Tunafurahi katika ujasiri atupao Mungu kwa ajili ya baadaye, ujasiri ambao tutashiriki katika utukufu wa Mungu.
3 Siyo hili tu, lakini pia tunafurahi katika mateso yetu. Tunajua kwamba mateso huzaa uvumilivu.
4 Uvumilivu huzaa kukubalika, na kukubalika huzaa ujasiri kwa ajili ya baadaye.
5 Ujasiri huu haukatishi tamaa, kwa sababu upendo wa Mungu umemwagwa katika mioyo yetu kupitia Roho Mtakatifu, ambaye alitolewa kwetu.
6 Kwa tulipokuwa tungali tu dhaifu, kwa wakati muafaka Kristo alikufa kwa ajili ya waovu.
7 Kwa kuwa itakuwa vigumu mmoja kufa kwa ajili ya mtu mwenye haki. Hii ni kwamba, pengine mtu angethubutu kufa kwa ajili ya mtu mwema.
8 Lakini Mungu amehakikisha upendo wake mwenyewe kwetu, kwa sababu wakati tulipokuwa tungali wenye dhambi, Kristo alikufa kwa ajili yetu.
9 Kisha zaidi ya yote, sasa kwa kuwa tumehesabiwa haki kwa damu yake, tutaokolewa kwa hiyo kutoka katika gadhabu ya Mungu.
10 Kwa kuwa, ikiwa wakati tulipokuwa maadui, tulipatanishwa na Mungu kwa njia ya kifo cha mwanae, zaidi sana, baada ya kuwa tumekwisha patanishwa, tutaokolewa kwa maisha yake.
11 Siyo hivi tu, bali pia tunafurahi katika Mungu kupitia Bwana Yesu Kristo, kupitia yeye ambaye sasa tumepokea upatanisho huu.
12 Kwa hiyo basi, kama kupitia mtu mmoja dhambi iliingia duniani, kwa njia hii kifo kiliingia kwa njia ya dhambi. Na kifo kikasambaa kwa watu wote, kwa sababu wote walifanya dhambi.
13 Kwa kuwa hadi sheria, dhambi ilikuwa duniani, lakini dhambi haihesabiki wakati hakuna sheria.
14 Hata hivyo, kifo kilitawala kutoka Adamu hadi Musa, hata juu ya wale ambao hawakufanya dhambi kama kutotii kwa Adamu, ambaye ni mfano wa yeye ambaye angekuja.
15 Lakini hata hivyo, zawadi ya bure si kama kosa. Kwa kuwa ikiwa kwa kosa la mmoja wengi walikufa, zaidi sana neema ya Mungu na zawadi kwa neema ya mtu mmoja, Yesu Kristo, imezidi kuongezeka kwa wengi.
16 Kwa kuwa zawadi si kama matokeo ya yule ambaye alifanya dhambi. Kwa kuwa kwa upande mwingine, hukumu ya adhabu ilikuja kwa sababu ya kosa la mtu mmoja. Lakini kwa upande mwingine, kipawa cha bure kinachotoka katika kuhesabiwa haki kilikuja baada ya makosa mengi.
17 Kwa maana, ikiwa kwa kosa la mmoja, kifo kilitawala kupitia mmoja, zaidi sana wale ambao watapokea neema nyingi pamoja na kipawa cha haki watatawala kupitia maisha ya mmoja, Yesu Kristo.
18 Hivyo basi, kama kupitia kosa moja watu wote walikuja kwenye hukumu, ingawa kupitia tendo moja la haki kulikuja kuhesabiwa haki ya maisha kwa watu wote.
19 Kwa kuwa kama kupitia kutotii kwa mtu mmoja wengi walifanywa wenye dhambi, hivyo kupitia utii wa mmoja wengi watafanywa wenye haki.
20 Lakini sheria iliingia pamoja, ili kwamba kosa liweze kuenea. Lakini mahali ambapo dhambi ilizidi kuwa nyingi, neema iliongezeka hata zaidi.
21 Hii ilitokea ili kwamba, kama dhambi ilivyotawala katika kifo, ndivyo hata neema inaweza kutawala kupitia haki kwa ajili ya maisha ya milele kupitia Yesu Kristo Bwana wetu. (aiōnios )