< Warumi 4 >
1 Tutasema nini tena kwamba Abrahamu, baba yetu kwa jinsi ya mwili, amepatikana?
Tuseme nini basi, kuhusu Abrahamu baba yetu kwa jinsi ya mwili: yeye alipataje kujua jambo hili?
2 Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, angekuwa na sababu ya kujisifu, lakini si mbele za Mungu.
Kwa maana ikiwa Abrahamu alihesabiwa haki kwa matendo, basi, anacho kitu cha kujivunia, lakini si mbele za Mungu.
3 Kwani maandiko yanasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu, na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
Kwa maana Maandiko yasemaje? “Abrahamu alimwamini Mungu na ikahesabiwa kwake kuwa haki.”
4 Sasa kwa mtu afanyaye kazi, malipo yake hayahesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.
Basi mtu afanyapo kazi, mshahara wake hauhesabiwi kwake kuwa ni zawadi, bali ni haki yake anayostahili.
5 Lakini kwa mtu asiyefanya kazi bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtaua, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.
Lakini kwa mtu ambaye hafanyi kazi na anamtumaini Mungu, yeye ambaye huwahesabia waovu haki, imani yake inahesabiwa kuwa haki.
6 Daudi pia hunena baraka juu ya mtu ambaye Mungu amhesabia haki pasipo matendo.
Daudi pia alisema vivyo hivyo aliponena juu ya baraka za mtu ambaye Mungu humhesabia haki pasipo matendo:
7 Alisema, “Wamebarikiwa wale ambao maovu yao yamesamehewa na ambao dhambi zao zimefunikwa.
“Wamebarikiwa wale ambao wamesamehewa makosa yao, ambao dhambi zao zimefunikwa.
8 Amebarikiwa mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.”
Heri mtu yule Bwana hamhesabii dhambi zake.”
9 Basi je baraka hizi ni kwa wale waliotahiriwa tu, au pia kwa wale wasiotahiriwa? Kwa maana twasema, “kwa Abrahamu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki.”
Je, huku kubarikiwa ni kwa wale waliotahiriwa peke yao, au pia na kwa wale wasiotahiriwa? Tunasema, “Imani ya Abrahamu ilihesabiwa kwake kuwa haki.”
10 Hivyo ilihesabiwaje basi? Wakati Abrahamu alikuwa katika tohara, au kabla hajatahiriwa? Haikuwa katika kutahiriwa, bali katika kutotahiriwa.
Je, ni lini basi ilipohesabiwa kwake kuwa haki? Je, ilikuwa kabla au baada ya kutahiriwa kwake? Haikuwa baada, ila kabla hajatahiriwa.
11 Abrahamu alipokea alama ya kutahiriwa. Huu ulikuwa muhuri wa ile haki ya imani aliyokuwa nayo tayari kabla hajatahiriwa. Matokeo ya ishara hii ni kwamba alifanyika kuwa baba wa wote waaminio, hata kama wapo katika kutotahiriwa. Hii ina maana kwamba haki itahesabiwa kwao.
Alipewa ishara ya tohara kuwa muhuri wa haki aliyokuwa nayo kwa imani hata alipokuwa bado hajatahiriwa. Kusudi lilikuwa kumfanya baba wa wote wale waaminio pasipo kutahiriwa na ambao wamehesabiwa haki.
12 Hii pia ilimaanisha kuwa Abrahamu alifanyika baba wa tohara si tu kwa wale wanaotokana na tohara, bali pia wale wanaozifuata nyayo za baba yetu Abrahamu. Na hii ndiyo imani aliyokuwa nayo kwa wasiotahiriwa.
Vivyo hivyo awe baba wa wale waliotahiriwa ambao si kwamba wametahiriwa tu, bali pia wanafuata mfano wa imani ambayo Baba yetu Abrahamu alikuwa nayo kabla ya kutahiriwa.
13 Kwa maana haikuwa kwa sheria kwamba ahadi ilitolewa kwa Abrahamu na uzao wake, ahadi hii ya kwamba watakuwa warithi wa dunia. isipokuwa, ilikuwa kupitia haki ya imani.
Kwa maana ile ahadi kwamba angeurithi ulimwengu haikuja kwa Abrahamu au kwa wazao wake kwa njia ya sheria bali kwa njia ya haki ipatikanayo kwa imani.
14 Kwa maana kama wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.
Kwa maana ikiwa wale waishio kwa sheria ndio warithi, imani haina thamani na ahadi haifai kitu,
15 Kwa sababu sheria huleta ghadhabu, lakini pale ambapo hakuna sheria, pia hakuna kutotii.
kwa sababu sheria huleta ghadhabu. Mahali ambapo hakuna sheria hakuna makosa.
16 Kwa sababu hii hili hutokea kwa imani, ili iwe kwa neema. Matokeo yake, ahadi ni dhahiri kwa uzao wote. Na wazawa hawa si tu wale wanaojua sheria, bali pia wale ambao ni wa imani ya Abrahamu. Kwa maana yeye ni baba yetu sisi sote,
Kwa hiyo, ahadi huja kwa njia ya imani, ili iwe ni kwa neema, na itolewe kwa wazao wa Abrahamu, si kwa wale walio wa sheria peke yao, bali pia kwa wale walio wa imani ya Abrahamu. Yeye ndiye baba yetu sisi sote.
17 kama ilivyoandikwa, “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Abrahamu alikuwa katika uwepo wa yule aliyemwamini, yaani, Mungu ambaye huwapa wafu uzima na kuyaita mambo ambayo hayapo ili yaweze kuwepo.
Kama ilivyoandikwa: “Nimekufanya wewe kuwa baba wa mataifa mengi.” Yeye ni baba yetu mbele za Mungu, ambaye yeye alimwamini, yule Mungu anaye fufua waliokufa, na kuvitaja vile vitu ambavyo haviko kana kwamba vimekwisha kuwako.
18 Licha ya hali zote za nje, Abrahamu kwa ujasiri alimuamini Mungu kwa siku zijazo. Hivyo akawa baba wa mataifa mengi, kulingana na kile kilichonenwa,”... Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.”
Akitarajia yasiyoweza kutarajiwa, Abrahamu akaamini, akawa baba wa mataifa mengi, kama alivyoahidiwa kwamba, “Uzao wako utakuwa mwingi mno.”
19 Yeye hakuwa dhaifu katika imani. Abrahamu alikiri kwamba mwili wake mwenyewe ulikwisha kufa - alikuwa na umri wa karibu miaka mia moja. Pia alikubaliana na hali ya kufa ya tumbo la Sara.
Abrahamu hakuwa dhaifu katika imani hata alipofikiri juu ya mwili wake, ambao ulikuwa kama uliokufa, kwani umri wake ulikuwa unakaribia miaka mia moja, au alipofikiri juu ya ufu wa tumbo la Sara.
20 Lakini kwa sababu ya ahadi ya Mungu, Abrahamu hakusita katika kutokuamini. Bali, alitiwa nguvu katika imani na alimsifu Mungu.
Lakini Abrahamu hakusitasita kwa kutokuamini ahadi ya Mungu, bali alitiwa nguvu katika imani yake na kumpa Mungu utukufu,
21 Alikuwa akijua hakika ya kuwa kile ambacho Mungu ameahidi, alikuwa pia na uwezo wa kukikamilisha.
akiwa na hakika kabisa kwamba Mungu alikuwa na uwezo wa kutimiza lile aliloahidi.
22 Kwa hiyo hii pia ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.
Hii ndio sababu, “ilihesabiwa kwake kuwa haki.”
23 Sasa haikuandikwa tu kwa faida yake, kwamba ilihesabiwa kwake.
Maneno haya “ilihesabiwa kwake kuwa haki,” hayakuandikwa kwa ajili yake peke yake,
24 Iliandikwa kwa ajili yetu pia, kwa waliowekewa kuhesabiwa, sisi ambao tunaamini katika yeye aliyemfufua Bwana wetu Yesu kutoka wafu.
bali kwa ajili yetu sisi pia ambao Mungu atatupa haki, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu kutoka kwa wafu.
25 Huyu ni yule ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu na kufufuliwa ili tupate kuhesabiwa haki.
Alitolewa afe kwa ajili ya dhambi zetu, naye alifufuliwa kutoka mauti ili tuhesabiwe haki.