< Warumi 3 >
1 Kisha ni faida gani aliyo nayo Myahudi? Na faida ya tohara ni nini?
2 Ni vyema sana kwa kila njia. Awali ya yote, Wayahudi walikabidhiwa ufunuo kutoka kwa Mungu.
3 Lakini, itakuwaje iwapo baadhi ya Wayahudi hawakuwa na imani? Je, kutokuamini kwao kutafanya uaminifu wa Mungu kuwa batili?
4 La hasha. Badala yake, acha Mungu aonekane kuwa kweli, hata kama kila mtu ni mwongo. Kama ilivyokuwa imeandikwa, “Ya kwamba uweze kuonekana kuwa mwenye haki katika maneno yako, na uweze kushinda uingiapo katika hukumu.”
5 Lakini ikiwa uovu wetu unaonesha haki ya Mungu, tuseme nini? Mungu si dhalimu atoapo ghadhabu yake, je yupo hivyo? Naongea kutokana na mantiki ya kibinadamu.
6 La hasha! Ni jinsi gani basi Mungu atauhukumu ulimwengu?
7 Lakini ikiwa kweli ya Mungu kupitia uongo wangu hutoa sifa tele kwa ajili yake, kwa nini ningali bado nahukumiwa kama mwenye dhambi?
8 Kwa nini tusiseme, kama tulivyosingiziwa na kama wengine wanavyothibitisha kwamba tunasema, “Tufanye uovu, ili mema yaje”? Hukumu juu yao ni ya haki.
9 Ni nini basi? Tunajitetea wenyewe? Hapana kabisa. Kwa kuwa sisi tayari tumewatuhumu Wayahudi na Wayunani wote pamoja, ya kuwa wapo chini ya dhambi.
10 Hii ni kama ilivyoandikwa: “Hakuna mwenye haki, hata mmoja.
11 Hakuna mtu ambaye anaelewa. Hakuna mtu ambaye anamtafuta Mungu.
12 Wote wamegeuka. Wao kwa pamoja wamekuwa hawana maana. Hakuna atendaye mema, la, hata mmoja.
13 Makoo yao ni kaburi lililo wazi. Ndimi zao zimedanganya. Sumu ya nyoka ipo chini ya midomo yao.
14 Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.
15 Miguu yao ina mbio kumwaga damu.
16 Uharibifu na mateso yapo katika njia zao.
17 Watu hawa hawajajua njia ya amani.
18 Hakuna hofu ya Mungu mbele ya macho yao.”
19 Sasa tunajua kwamba chochote sheria isemacho, husema na wale walio chini ya sheria. Hii ni ili kwamba kila kinywa kifungwe, na hivyo kwamba ulimwengu wote uweze kuwajibika kwa Mungu.
20 Hii ni kwa sababu hakuna mwili utakaohesabiwa haki kwa matendo ya sheria mbele za macho yake. Kwa kuwa kupitia Sheria huja ufahamu wa dhambi.
21 Lakini sasa pasipo sheria, haki ya Mungu imejulikana. Ilishuhudiwa kwa sheria na Manabii,
22 hiyo ni, haki ya Mungu kupitia imani katika Yesu Kristo kwa wale wote wanaoamini. Maana hakuna tofauti.
23 Kwa kuwa wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu.
24 Wamehesabiwa haki bure kwa neema yake kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu.
25 Kwa maana Mungu alimtoa Kristo Yesu awe upatanisho kwa njia ya imani katika damu yake. Alimtoa Kristo kama ushahidi wa haki yake, kwa sababu ya kuziachilia dhambi zilizopita
26 katika uvumilivu wake. Haya yote yalitokea ili kuonesha haki yake wakati huu wa sasa. Hii ilikuwa ili aweze kujithibitisha mwenyewe kuwa haki, na kuonesha kwamba humhesabia haki mtu yeyote kwa sababu ya imani katika Yesu.
27 Kuwapi basi kujisifu? Kumetengwa. Kwa misingi ipi? Misingi ya matendo? Hapana, lakini kwa misingi ya imani.
28 Hivyo tunahitimisha kwamba mtu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.
29 Au Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Je yeye si Mungu wa watu wa Mataifa pia? Ndiyo, wa mataifa pia.
30 Ikiwa kwa kweli Mungu ni mmoja, atawahesabia haki walio wa tohara kwa imani, na wasiotahiriwa kwa njia ya imani.
31 Je sisi twaibatilisha sheria kwa imani? La hasha! Kinyume cha hayo, sisi twaithibitisha sheria.