< Warumi 2 >

1 Kwa hiyo hauna udhuru, wewe uhukumuye, kwa maana katika yale uhukumuyo mwingine wajitia hatiani mwenyewe. Kwa maana wewe uhukumuye unafanya mambo yale yale.
Basi, rafiki, kama unawahukumu wengine, huwezi kamwe kujitetea haidhuru wewe ni nani. Kwa maana, kwa kuwahukumu wengine, unajilaani wewe mwenyewe kwa vile nawe unayafanya mambo yaleyale unayohukumu.
2 Lakini twajua kwamba hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao mambo kama hayo.
Tunajua kwamba hukumu ya Mungu kwa wale wanaofanya mambo kama hayo ni hukumu ya haki.
3 Lakini wewe tafakari hili, wewe ambaye unahukumu wale wanaotenda mambo hayo ingawa nawe unafanya mambo yayo hayo. Je utaepuka hukumu ya Mungu?
Lakini wewe, rafiki, unayewahukumu wale wanaofanya mambo kama hayo bali wewe pia unayafanya, je unadhani utaiepa hukumu ya Mungu?
4 Au unafikiri kidogo sana juu ya wingi wa wema wake, kuchelewa kwa adhabu yake, na uvumilivu wake? Je, hujui kwamba wema wake unapaswa kukuelekeza katika toba?
Au labda unaudharau wema wake mkuu, uvumilivu wake na saburi yake, bila kutambua kwamba wema wake huo una shabaha ya kukuongoza upate kutubu?
5 Bali kwa kadiri ya ugumu wako na kwa moyo wako usio na toba wajiwekea mwenyewe akiba ya ghadhabu kwa siku ile ya ghadhabu, yaani, siku ile ya ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu.
Lakini unao ugumu na ukaidi wa moyo, na hivyo unajilundikia adhabu kwa Siku ile ambayo ghadhabu ya Mungu na hukumu zake za haki vitadhihirishwa.
6 Yeye atamlipa kila mtu kipimo sawa na matendo yake:
Siku hiyo Mungu atamlipa kila mmoja kufuatana na matendo yake.
7 kwa wale ambao kwa uthabiti wa matendo mema wametafuta sifa, heshima na kutokuharibika, atawapa uzima wa milele. (aiōnios g166)
Wale wanaozingatia kutenda mema, kutafuta utukufu na heshima ya Mungu na kutokufa, watapata uzima wa milele. (aiōnios g166)
8 Lakini kwa wale ambao ni wabinafsi, wasioitii kweli bali hutii dhuluma, ghadhabu na hasira kali itakuja.
Lakini wale wengine wenye ubinafsi, wenye kukataa mambo ya haki na kufuata uovu, wataangukiwa na ghadhabu na hasira ya Mungu.
9 Mungu ataleta dhiki na shida juu ya kila nafsi ya binadamu aliyefanya uovu, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.
Mateso na maumivu yatampata binadamu yeyote atendaye uovu. Yatawapata Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.
10 Lakini sifa, heshima na amani itakuja kwa kila mtu atendaye mema, kwa Myahudi kwanza, na kwa Myunani pia.
Lakini Mungu atawapa utukufu, heshima na amani wale wanaotenda mema; Wayahudi kwanza, na watu wa mataifa mengine pia.
11 Kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu.
Maana Mungu hambagui mtu yeyote.
12 Kwa maana kama vile wengi waliokosa pasipo sheria watapotea pasipo sheria, na kama vile wengi waliokosa kulingana na sheria watahukumiwa kwa sheria.
Wale wanaotenda dhambi bila kuijua Sheria ya Mose wataangamia ingawaje hawajui Sheria. Na wale wanaotenda dhambi wakiwa wanaijua Sheria watahukumiwa kisheria.
13 Maana si wasikiaji wa sheria walio wenye haki mbele za Mungu, bali ni wale waitendao sheria watakaohesabiwa haki.
Mtu hafanywi kuwa mwadilifu mbele yake Mungu kwa kuisikia Sheria, bali kwa kuitii Sheria.
14 Kwa maana watu wa Mataifa, ambao hawana sheria, wanafanya kwa asili mambo ya sheria, wao, wamekuwa sheria kwa nafsi zao, ingawa wao hawana sheria.
Mathalan: watu wa mataifa mengine hawana Sheria ya Mose; lakini kila wanapotimiza matakwa ya Sheria wakiongozwa na dhamiri zao, wao wenyewe wanakuwa kipimo cha Sheria ingawa hawaijui Sheria.
15 Kwa hili wanaonesha kwamba matendo yanayohitajika kwa mujibu wa sheria yameandikwa ndani ya mioyo yao. Dhamiri zao pia zinawashuhudia wao, na mawazo yao wenyewe ama huwashitaki au huwalinda wao wenyewe
Mwenendo wao unaonyesha kwamba matakwa ya Sheria yameandikwa mioyoni mwao. Dhamiri zao zinashuhudia pia jambo hilo, maana fikira zao mara nyingine huwashtaki, na mara nyingine huwatetea.
16 na pia kwa Mungu. Haya yatatokea katika siku ambayo Mungu atazihukumu siri za watu wote, sawasawa na injili yangu, kwa njia ya Yesu Kristo.
Hivyo, kufuatana na hii Habari Njema ninayohubiri, ndivyo itakavyokuwa wakati Mungu atakapohukumu mambo ya siri ya binadamu kwa njia ya Yesu Kristo.
17 Tuseme kwamba unajiita mwenyewe Myahudi, aliyekaa katika sheria, shangilia kwa kujisifu katika Mungu,
Na wewe, je? Wewe mwenyewe unajiita Myahudi; unaitumainia Sheria na kujivunia kuwa wa Mungu;
18 yajue mapenzi yake, na kupima mambo ambayo yanatofautiana nayo, baada ya kuagizwa na sheria.
kwa njia ya Sheria unajua matakwa ya Mungu na unaweza kuchagua jambo jema;
19 Na tuseme kwamba una ujasiri kwamba wewe mwenyewe ni kiongozi wa kipofu, mwanga kwa wale walio gizani,
wewe unajiona kuwa kiongozi wa vipofu na mwanga kwa wale walio gizani;
20 msahihishaji wa wajinga, mwalimu wa watoto, na kwamba unayo katika sheria jinsi ya elimu na kweli.
unajiona kuwa mkufunzi wa wajinga na mwalimu wa wale wasiokomaa bado. Unayo katika Sheria picha kamili ya elimu na ukweli.
21 Wewe basi, uhubiriye mwingine, je, hujifundishi mwenyewe? Wewe uhubiriye kutokuiba, je wewe huiba?
Basi, wewe unawafundisha wengine; kwa nini hujifundishi wewe mwenyewe? Unawahubiria wengine wasiibe, lakini kumbe wewe mwenyewe unaiba.
22 Wewe usemae usizini, je unazini? Wewe uchukiaye sanamu, je unaiba hekaluni?
Unasema: “Msizini,” na huku wewe unazini; unachukia sanamu za miungu hali wewe unajitajirisha kwa kuiba katika nyumba za miungu.
23 Wewe ujisifuye katika sheria, je haumfedheheshi Mungu katika kuvunja sheria?
Kwa kujigamba ati unayo Sheria ya Mungu, je huoni kwamba kwa kuivunja Sheria unamdharau Mungu?
24 Kwa maana “jina la Mungu linafedheheshwa kati ya watu wa mataifa kwa sababu yenu,” kama ilivyoandikwa.
Kama vile Maandiko Matakatifu yasemavyo: “Watu wa mataifa mengine wamelikufuru jina la Mungu kwa sababu yenu ninyi Wayahudi!”
25 Kwa maana Kutahiriwa kweli kwafaa kama ukitii sheria, lakini kama wewe ni mkiukaji wa sheria, kutahiriwa kwako kunakuwa kutokutahiriwa.
Kutahiriwa kwako kutakuwa na maana kama ukiitii Sheria. Lakini kama unaivunja Sheria, basi, ni afadhali ungalibaki bila kutahiriwa.
26 Basi, ikiwa, mtu asiyetahiriwa anaendelea kushika matakwa ya sheria, je kutokutahiriwa kwake hakutachukuliwa kana kwamba ametahiriwa?
Kama mtu wa mataifa mengine ambaye hakutahiriwa akitimiza matakwa ya Sheria, hakika atafikiriwa kana kwamba ametahiriwa.
27 Na yeye asiyetahiriwa kwa asili hatakuhukumu kama akitimiza sheria? Hii ni kwa sababu una maandiko yaliyoandikwa na tohara pia lakini bado u mkiukaji wa sheria!
Watu wa mataifa mengine watakuhukumu wewe Myahudi kama ukiivunja Sheria, ingawaje unayo maandishi ya Sheria na umetahiriwa, hali wao wanaitii Sheria ingawa hawakutahiriwa.
28 Kwa maana yeye si Myahudi aliye kwa hali ya nje; wala kutahiriwa si kule ambako ni kwa nje tu katika mwili.
Ndiyo kusema, si kila anayeonekana kwa nje kuwa Myahudi ni Myahudi wa kweli, wala mtu hawi Myahudi wa kweli ati kwa kuwa ametahiriwa kimwili.
29 Lakini yeye ni Myahudi aliye kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko. Sifa ya mtu wa namna hiyo haitokani na watu bali yatoka kwa Mungu.
Myahudi wa kweli ni yule aliye Myahudi kwa ndani, yaani yule ambaye ametahiriwa moyoni. Hili ni jambo la Roho, na si jambo la maandishi ya Sheria. Mtu wa namna hiyo anapata sifa, si kutoka kwa watu, bali kutoka kwa Mungu.

< Warumi 2 >