< Warumi 15 >

1 Sasa sisi tulio na nguvu tunapaswa kuuchukua udhaifu wa walio dhaifu, na hatupaswi kujipendeza wenyewe.
Sisi tulio na nguvu, hatuna budi kuchukuliana na kushindwa kwa wale walio dhaifu wala si kujipendeza nafsi zetu wenyewe.
2 Kila mmoja wetu ampendeze jirani yake kwani ni jambo jema, kwa lengo la kumjenga.
Kila mmoja wetu inampasa kumpendeza jirani yake kwa mambo mema, ili kumjenga katika imani.
3 Kwani hata Kristo hakujipendeza mwenyewe. Badala yake, ilikuwa kama ilivyoandikwa, “Matusi ya wale waliokutukana yamenipata mimi.”
Kwa maana hata Kristo hakujipendeza mwenyewe, bali kama ilivyoandikwa: “Matukano yao wale wanaokutukana wewe yalinipata mimi.”
4 Kwa chochote kilichotangulia kuandikwa, kiliandikwa kwa kutuelekeza, kwa kusudi kwamba kupitia uvumilivu na kupitia kutiwa moyo na maandiko tungekuwa na ujasiri.
Kwa maana kila kitu kilichoandikwa zamani, kiliandikwa kutufundisha, ili kwamba kwa saburi na faraja tunayopata katika Maandiko tuwe na tumaini.
5 Sasa Mungu wa uvumilivu na wa kutia moyo awape kuwa na nia sawa kwa kila mmoja kulingana na Yesu Kristo.
Mungu atoaye saburi na faraja, awajalie ninyi roho ya umoja miongoni mwenu mnapomfuata Kristo Yesu,
6 Aweze kufanya hivi kwa nia moja muweze kumsifu kwa kinywa kimoja Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
ili kwa moyo mmoja mpate kumtukuza Mungu aliye Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo.
7 Kwa hiyo mpokeeni kila mmoja, kama vile Kristo alivyowapokea, kwa utukufu wa Mungu.
Karibishaneni ninyi kwa ninyi kama Kristo alivyowakaribisha ninyi ili kumletea Mungu utukufu.
8 Kwani nasema kwamba Kristo amefanywa mtumishi wa tohara kwa niaba ya ukweli wa Mungu. Alifanya hivi ili kwamba aweze kuthibitisha ahadi zilizotolewa kwa mababa,
Kwa maana nawaambia kwamba, Kristo amekuwa mtumishi kwa wale waliotahiriwa ili kuonyesha kweli ya Mungu na kuthibitisha zile ahadi walizopewa baba zetu wa zamani,
9 na kwa mataifa kumtukuza Mungu kwa neema yake. Kama ambavyo imeandikwa, “Kwa hiyo nitatoa sifa kwako miongoni mwa mataifa na kuimba sifa katika jina lako.”
pia ili watu wa Mataifa wamtukuze Mungu kwa rehema zake. Kama ilivyoandikwa: “Kwa hiyo nitakutukuza katikati ya watu wa Mataifa; nitaliimbia sifa jina lako.”
10 Tena inasema, “Furahini, ninyi watu wa mataifa, pamoja na watu wake.”
Tena yasema, “Enyi watu wa Mataifa, furahini pamoja na watu wa Mungu.”
11 Na tena, “Msifuni Bwana, ninyi mataifa yote; acha watu wa mataifa yote wamsifu yeye.”
Tena, “Msifuni Bwana, ninyi watu wa Mataifa wote, na kumwimbia sifa, enyi watu wote.”
12 Tena Isaya asema, “Kutakuwa na shina la Yese, na mmoja atakayeinuka kutawala juu ya mataifa. Mataifa watakuwa na tumaini katika yeye.”
Tena Isaya anasema, “Shina la Yese litachipuka, yeye atakayeinuka ili kutawala juu ya mataifa. Watu wa Mataifa watamtumaini.”
13 Sasa Mungu wa tumaini awajaze na furaha yote na amani kwa kuamini, ili kwamba muweze kuzidi katika tumaini, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
Mungu wa tumaini awajaze ninyi furaha yote na amani katika kumwamini, ili mpate kujawa na tumaini tele kwa nguvu ya Roho Mtakatifu.
14 Mimi mwenyewe pia nimeshawishiwa nanyi, ndugu zangu. Nimeshawishiwa kwamba pia ninyi wenyewe mmejazwa na wema, mmejazwa na maarifa yote. Ninashawishiwa kwamba, ninyi mwaweza pia kuhimizana kila mmoja na mwenzake.
Ndugu zangu, mimi mwenyewe ninasadiki kwamba mmejaa wema na ufahamu wote, tena mnaweza kufundishana ninyi kwa ninyi.
15 Lakini ninaandika kwa ujasiri zaidi kwenu juu ya mambo fulani ili kuwakumbusha tena, sababu ya kipawa nilichopewa na Mungu.
Nimewaandikia kwa ujasiri vipengele kadha wa kadha katika waraka huu kama kuwakumbusha tena kwa habari ya ile neema Mungu aliyonipa,
16 Kipawa hiki kilikuwa kwamba niweze kuwa mtumishi wa Yesu Kristo aliyetumwa kwa mataifa, kujitoa kama kuhani wa injili ya Mungu. Ningeweza kufanya hivi ili kujitoa kwangu kwa mataifa kuwe kumekubaliwa, kumetengwa na Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu.
ili kuwa mhudumu wa Kristo Yesu kwa watu wa Mataifa nikiwa na huduma ya kikuhani ya kutangaza Injili ya Mungu, ili watu wa Mataifa wapate kuwa dhabihu inayokubaliwa na Mungu, iliyotakaswa na Roho Mtakatifu.
17 Hivyo furaha yangu iko katika Kristo Yesu na katika mambo ya Mungu.
Kwa hiyo ninajisifu katika Kristo Yesu, kwenye utumishi wangu kwa Mungu.
18 Kwani sitaweza kuthubutu kunena lolote isipokuwa kwamba Kristo amekamilisha kupitia kwangu utii wa mataifa. Haya mambo yametimizwa kwa neno na tendo,
Kwa maana sitathubutu kusema kitu chochote zaidi ya kile ambacho Kristo amefanya kwa kunitumia mimi katika kuwaongoza watu wa Mataifa wamtii Mungu kwa yale niliyosema na kufanya,
19 kwa nguvu za ishara na maajabu, na kwa nguvu za Roho Mtakatifu. Hii ilikuwa ili kwamba kutoka Yerusalem, na kuzungukia mbali kama Iliriko, niweze kuichukua nje kwa ukamilifu injili ya Kristo.
kwa nguvu za ishara na miujiza, kwa uweza wa Roho wa Mungu, hivyo kuanzia Yerusalemu hadi maeneo yote ya kandokando yake mpaka Iliriko, nimekwisha kuihubiri Injili ya Kristo kwa ukamilifu.
20 Kwa njia hii, nia yangu imekuwa kuitangaza injili, lakini si mahali Kristo anajulikana kwa jina, ili kwamba nisiweze kujenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
Hivyo ni nia yangu kuhubiri Habari Njema, si pale ambapo Kristo amekwisha kujulikana, ili nisije nikajenga juu ya msingi wa mtu mwingine.
21 Kama ilivyoandikwa: “Ambao kwa yeye hawana habari zake alikuja watamwona, na wale ambao hawakumsikia watamfahamu.”
Lakini kama ilivyoandikwa: “Wale ambao hawajahubiriwa habari zake wataona, nao wale ambao hawajazisikia watafahamu.”
22 Kwahiyo nilikuwa pia nimezuiliwa mara nyingi kuja kwenu.
Hii ndiyo sababu nimezuiliwa mara nyingi nisiweze kuja kwenu.
23 Lakini sasa, sina tena sehemu yoyote katika mikoa hii, na nimekuwa nikitamani kwa miaka mingi kuja kwenu.
Lakini sasa kwa kuwa hakuna nafasi zaidi kwa ajili yangu katika sehemu hii, ninatamani kuja kwenu kama ambavyo nimekuwa na shauku kwa miaka mingi.
24 Hivyo mara zote nikienda Hispania, ninatumaini kuwaona nikipita, na kuweza kupelekwa njia yangu na ninyi, baada ya kuwa nimefurahia ushirika na ninyi kwa muda.
Nimekusudia kufanya hivyo nitakapokuwa njiani kwenda Hispania. Natarajia kuwaona katika safari yangu na kusafirishwa nanyi mpaka huko, baada ya kufurahia ushirika wenu kwa kitambo kidogo.
25 Lakini sasa ninakwenda Yerusalemu kuwahudumia waumini.
Sasa, niko njiani kuelekea Yerusalemu kwa ajili ya kuwahudumia watakatifu huko.
26 Maana iliwapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo maalumu kwa masikini miongoni mwa waumini huko Yerusalemu.
Kwa kuwa imewapendeza watu wa Makedonia na Akaya kufanya changizo kwa ajili ya maskini walioko miongoni mwa watakatifu huko Yerusalemu.
27 Ndiyo, ilikuwa kwa upendo wao, na hakika, wamekuwa wadeni wao. Maana ikiwa mataifa wameshiriki katika mambo yao ya kiroho, wanadaiwa na wao pia kuwahudumia katika mahitaji ya vitu.
Imewapendeza kufanya hivyo, naam, kwani ni wadeni wao. Kwa maana ikiwa watu wa Mataifa wameshiriki baraka za rohoni za Wayahudi, wao ni wadeni wa Wayahudi, ili Wayahudi nao washiriki baraka zao za mambo ya mwilini.
28 Kwahiyo, wakati nimekamilisha hivi na kuwa na utoshelevu wa tunda hili kwao, mimi nitakwenda njiani pamoja nanyi huko Hispania.
Kwa hiyo baada ya kukamilisha kazi hii na kuhakikisha kuwa wamepokea kila kitu kilichokusanywa, nitapitia kwenu nikiwa njiani kwenda Hispania.
29 Najua kwamba, wakati nikija kwenu, nitakuja katika utimilifu wa baraka za Kristo.
Ninajua kwamba nitakapokuja kwenu, nitakuja na wingi wa baraka za Kristo.
30 Sasa ninawasihi, ndugu, kwa Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa upendo wa Roho, kwamba mshiriki pamoja nami katika maombi yenu kwa Mungu kwa ajili yangu.
Basi, ndugu zangu, nawasihi kwa Jina la Bwana wetu Yesu Kristo na kwa upendo wa Roho Mtakatifu, kujiunga nami katika taabu zangu mkiniombea kwa Mungu.
31 Ombeni kwamba niweze kuokolewa kutoka kwao wasio na utii katika Yudea, na kwamba huduma yangu huko Yerusalemu iweze kupokelewa na waumini.
Ombeni ili nipate kuokolewa mikononi mwa wale wasioamini walioko Uyahudi, na kwamba utumishi wangu upate kukubaliwa na watakatifu wa huko Yerusalemu,
32 Ombeni kwamba ninaweza kuja kwenu kwa furaha kupitia mapenzi ya Mungu, na kwamba niweze kuwa pamoja nanyi, kupata kupumzika.
ili kwa mapenzi ya Mungu niweze kuja kwenu kwa furaha, nami niburudishwe pamoja nanyi.
33 Na Mungu wa amani awe pamoja nanyi nyote. Amina
Mungu wa amani na awe pamoja nanyi nyote. Amen.

< Warumi 15 >