< Warumi 11 >
1 Basi nasema, je, Mungu aliwakataa watu wake? Hata kidogo. Kwa kuwa mimi pia ni Mwiisraeli, wa ukoo wa Abrahamu, wa kabila la Benyamini.
2 Mungu hakuwakataa watu wake, aliowajua tangu mwanzo. Je hamjui andiko linasema nini kuhusu Eliya, jinsi alivyomsihi Mungu juu ya Israeli?
3 “Bwana, wamewaua manabii wako, nao wamebomoa madhabahu zako. Mimi peke yangu nimesalia, nao wanatafuta uhai wangu.”
4 Lakini jibu la Mungu lasema nini kwako? “Nimetunza kwa ajili yangu watu elfu saba ambao hawampigii magoti Baali.”
5 Hata hivyo, wakati huu wa sasa pia kuna walio salia kwa sababu ya uchaguzi wa neema.
6 Lakini ikiwa ni kwa neema, si tena kwa matendo. Vinginevyo neema haitakuwa tena neema.
7 Ni nini basi? Jambo ambalo Israeli alikuwa akitafuta, hakukipata, bali wateule walikipata, na wengine walitiwa uzito.
8 Ni kama ilivyoandikwa: “Mungu amewapa roho ya ubutu, macho ili wasione, na masikio ili wasisikie, mpaka leo hii.”
9 Naye Daudi anasema, “Acha meza zao na ziwe wavu, mtego, sehemu ya kujikwaa, na kulipiza kisasi dhidi yao.
10 Acha macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona. Ukawainamishe migongo yao daima.”
11 Basi nasema, “Je, wamejikwaa hata kuanguka?” Isiwe hivyo kamwe. Badala yake, kwa kushindwa kwao, wokovu umefika kwa Mataifa, ili wao wenyewe watiwe wivu.
12 Sasa ikiwa kushindwa kwao ni utajiri wa ulimwengu, na kama hasara yao ni utajiri wa mataifa, ni kiasi gani zaidi itakuwa kukamilika kwao?
13 Na sasa naongea nanyi watu wa Mataifa. Kwa kuwa nimekuwa mtume kwa watu wa Mataifa mengine, najivunia huduma yangu.
14 Labda nitawatia wivu walio mwili mmoja na mimi. Labda tutawaokoa baadhi yao.
15 Maana ikiwa kukataliwa kwao ni maridhiano ya dunia, kupokelewa kwao kutakuwaje ila uhai toka kwa wafu?
16 Kama matunda ya kwanza ni akiba, ndivyo ilivyo kwa donge la unga. Kama mzizi ni akiba, matawi nayo kadhalika.
17 Lakini kama baadhi ya matawi yamekatwa, kama wewe, tawi pori la mzeituni, ulipandikizwa kati yao, na kama ulishiriki pamoja nao katika mizizi ya utajiri wa mzeituni,
18 usijisifu juu ya matawi. Lakini kama unajisifu, si wewe ambaye unaisaidia mizizi, bali mizizi inakusaidia wewe.
19 Basi utasema, “Matawi yalikatwa ili nipate kupandikizwa katika shina.”
20 Hiyo ni kweli. Kwa sababu ya kutoamini kwao walikatwa, lakini wewe ulisimama imara kwa sababu ya imani yako. Usijifikirie mwenyewe kwa hali ya juu sana, bali ogopa.
21 Kwa maana ikiwa Mungu hakuyaachia matawi ya asili, hatakuhurumia wewe pia.
22 Angalia, basi, matendo mema na ukali wa Mungu. Kwa upande mmoja, ukali ulikuja juu ya Wayahudi ambao walianguka. Lakini kwa upande mwingine, wema wa Mungu huja juu yako, kama utadumu katika wema wake. Vinginevyo wewe pia utakatiliwa mbali.
23 Na pia, kama hawataendelea katika kutoamini kwao, watapandikizwa tena. Maana Mungu anao uwezo wa kuwapandikiza tena.
24 Kwa maana ikiwa ninyi mlikatwa nje kwa ulio kwa asili mzeituni mwitu, na kinyume cha asili mlipandikizwa katika mzeituni ulio mwema, si zaidi sana hawa Wayahudi, ambao ni kama matawi ya asili kuweza kupandikizwa tena ndani ya mzeituni wao wenyewe?
25 Kwa maana ndugu sitaki msijue, kuhusiana na siri hii, ili kwamba msiwe na hekima katika kufikiri kwenu wenyewe. Siri hii ni kwamba ugumu umetokea katika Israeli, hadi kukamilika kwa mataifa kutakapokuja.
26 Hivyo Israeli wote wataokoka, kama ilivyoandikwa: “Kutoka Sayuni atakuja Mkombozi. Atauondoa uovu kutoka kwa Yakobo.
27 Na hili litakuwa agano langu pamoja nao, wakati nitakapoziondoa dhambi zao.”
28 Kwa upande mmoja kuhusu injili, wanachukiwa kwa sababu yenu. Kwa upande mwingine kutokana na uchaguzi wa Mungu, wamependwa kwa sababu ya mababu.
29 Kwa kuwa zawadi na wito wa Mungu haubadiliki.
30 Kwa kuwa awali ninyi mlikuwa mmemwasi Mungu, lakini sasa mmeipokea rehema kwa sababu ya kuasi kwao.
31 Kwa njia iyo hiyo, sasa hawa Wayahudi wameasi. Matokeo yake ni kwamba kutokana na huruma mliyojaliwa ninyi wanaweza pia kupokea rehema.
32 Maana Mungu amewafunga watu wote katika uasi, ili aweze kuwahurumia wote. (eleēsē )
33 Jinsi zilivyo kuu utajiri na hekima na maarifa ya Mungu! Hazichunguziki hukumu zake, na njia zake hazigunduliki!
34 “Maana ni nani aliyeijua nia ya Bwana? Au ni nani amekuwa mshauri wake?
35 Au ni nani kwanza aliyempa kitu Mungu, ili alipwe tena?”
36 Kwa maana kutoka kwake, na kwa njia yake na kwake, vitu vyote vipo. Kwake uwe utukufu milele. Amina. (aiōn )