< Warumi 10 >
1 Ndugu, nia ya moyo wangu na ombi langu kwa Mungu ni kwa ajili yao, kwa ajili ya wokovu wao.
2 Kwa kuwa nawashuhudia kwamba wanajuhudi kwa ajili ya Mungu, lakini si kwa ajili ya ufahamu.
3 Kwa kuwa hawajui haki ya Mungu, na wanatafuta kujenga haki yao wenyewe. Hawakuwa watiifu kwa haki ya Mungu.
4 Kwa kuwa Kristo ndiye utimilifu wa sheria kwa ajili ya haki ya kila mtu aaminiye.
5 Kwa kuwa Musa anaandika kuhusu haki ambayo huja kutokana na sheria: “Mtu ambaye hutenda haki ya sheria ataishi kwa haki hii.”
6 Lakini haki ambayo inatokana na imani husema hivi, “Usiseme moyoni mwako, 'Nani atapaa kwenda mbinguni?' (Hii ni kumleta Kristo chini).
7 Na usiseme, 'Nani atashuka katika shimo?”' (Hii ni, kumleta Kristo juu kutoka kwa wafu). (Abyssos )
8 Lakini inasema nini? “Neno liko karibu na wewe, katika kinywa chako na katika moyo wako.” Hilo ni neno la imani, ambalo tunatangaza.
9 Kwa kuwa kama kwa kinywa chako unamkiri Yesu ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako kwamba Mungu alimfufua kutoka kwa wafu, utaokoka.
10 Kwa kuwa kwa moyo mtu huamini na kupata haki, na kwa kinywa hukiri na kupata wokovu.
11 Kwa kuwa andiko lasema, “Kila amwaminiye hata aibika.”
12 kwa kuwa hakuna tofauti kati ya Myahudi na Myunani. Kwa kuwa Bwana yule yule ni Bwana wa wote, na ni tajiri kwa wote wamwitao.
13 Kwa kuwa kila mtu ambaye huliitia jina la Bwana ataokoka.
14 Kwa jinsi gani wanaweza kumwita yeye ambaye hawajamwamini? Na jinsi gani wanaweza kuamini katika yeye ambaye hawajamsikia? Na watasikiaje pasipo muhubiri?
15 Na jinsi gani wanaweza kuhubiri, isipokuwa wametumwa? - Kama ilivyoandikwa, “Jinsi gani ni mizuri miguu ya wale ambao wanatangaza habari za furaha za mambo mema!”
16 Lakini wote hawakusikiliza injili. Kwa kuwa Isaya hunena, “Bwana, ni nani aliyesikia ujumbe wetu?”
17 Hivyo imani huja kutokana na kusikia, na kusikia kwa neno la Kristo.
18 Lakini nasema, “Je hawakusikia?” Ndiyo, kwa hakika sana. “Sauti yao imekwisha toka nje katika nchi yote, na maneno yao kwenda miisho ya dunia.”
19 Zaidi ya yote, Ninasema, “Je Israel hakujua?” Kwanza Musa hunena, “Nitawachokoza kuwatia wivu kwa watu ambao si taifa. Kwa njia ya taifa lisilo na uelewa, nitawachochea hadi mkasirike.”
20 Na Isaya ni jasiri sana na husema, “Nilipatikana na wale ambao hawakunitafuta. Nilionekana kwa wale ambao hawakunihitaji.”
21 Lakini kwa Israel husema, “Siku zote nilinyoosha mikono yangu kwa wasiotii na kwa watu wagumu.”