< Warumi 1 >

1 Paulo, mtumishi wa Yesu Kristo, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu.
Kutoka kwangu mimi Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, na mtume niliyeteuliwa na kuitwa kwa ajili ya kuhubiri Habari Njema ya Mungu.
2 Hii ndio ile Injili aliyoiahidi zamani kupitia manabii wake katika maandiko matakatifu.
Hapo kale, Mungu aliwaahidia watu hii Habari Njema kwa njia ya manabii wake katika Maandiko Matakatifu.
3 Ni kuhusu Mwana wake, aliyezaliwa kutoka ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili.
Hii Habari Njema inamhusu Mwana wa Mungu, Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye mintarafu ubinadamu wake, alikuwa mzawa wa Daudi;
4 Yeye alitangazwa kwa Mwana wa Mungu kwa nguvu ya Roho ya utakatifu kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu.
mintarafu utakatifu wake wa kimungu, alithibitishwa kwa uwezo mkuu kwamba ni Mwana wa Mungu kwa kufufuliwa kutoka wafu.
5 Kupitia yeye tumepokea neema na utume kwa utii wa imani kati ya mataifa yote, kwa ajili ya jina lake.
Kwa njia yake, mimi nimepewa neema ya kuwa mtume, ili kwa ajili yake niwaongoze watu wa mataifa yote wapate kuamini na kutii.
6 Kati ya mataifa haya, ninyi pia mmeitwa kuwa wa Yesu Kristo.
Ninyi ni miongoni mwa watu hao; mmeitwa muwe watu wake Yesu Kristo.
7 Barua hii ni kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watu watakatifu. Neema na iwe kwenu, na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Basi, ninawaandikia ninyi nyote mlioko Roma ambao Mungu anawapenda, akawateua muwe watu wake. Nawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
8 Kwanza, namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inahubiriwa katika dunia nzima.
Awali ya yote, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inasikika duniani kote.
9 Kwa maana Mungu ni shahidi wangu, ambaye ninamtumikia kwa roho yangu katika injili ya Mwana wake, jinsi ninavyodumu katika kuwataja.
Mungu, ambaye ninamtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Habari Njema ya Mwanae, ni shahidi wangu kwamba ninawakumbukeni
10 Daima naomba katika sala zangu kwamba kwa njia yoyote nipate mwishowe kuwa na mafanikio sasa kwa mapenzi ya Mungu katika kuja kwenu.
daima katika sala zangu. Namwomba Mungu akipenda, anipatie nafasi nzuri ya kuja kwenu sasa.
11 Maana natamani kuwaona, ili nipate kuwapa ninyi baadhi ya karama za rohoni, nipate kuwaimarisha.
Kwa maana ninatamani sana kuwaoneni ili nipate kuwagawieni zawadi ya kiroho na kuwaimarisha.
12 Yaani, natazamia kutiwa moyo pamoja nanyi, kwa njia ya imani ya kila mmoja wetu, yenu na yangu.
Ndiyo kusema, tutaimarishana: imani yenu itaniimarisha mimi, na yangu itawaimarisha ninyi.
13 Sasa ndugu, sitaki mkose kufahamu kwamba, mara nyingi nimekusudia kuja kwenu, lakini nimezuiliwa mpaka sasa. Nilitaka hivi ili kuwa na matunda kwenu kama ilivyo pia miongoni mwa watu wa mataifa.
Ndugu zangu, nataka mjue kwamba mara nyingi nilikusudia kuwatembeleeni, lakini mpaka sasa nimezuiwa. Ningependa kupata mafanikio mema kati yenu kama nilivyopata kati ya watu wa mataifa mengine.
14 Nadaiwa na Wayunani na wageni pia, werevu na wajinga.
Ninalo jukumu kwa watu wote, waliostaarabika na wasiostaarabika, wenye elimu na wasio na elimu.
15 Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi niko tayari kutangaza injili kwenu pia ninyi mlio huko Roma.
Ndiyo maana ninatamani pia kuihubiri Habari Njema kwenu ninyi mlioko huko Roma.
16 Kwa maana siionei haya injili, kwa kuwa ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza na kwa Myunani pia.
Sioni aibu kutangaza Habari Njema; yenyewe ni nguvu ya Mungu inayowaokoa wote wanaoamini: Wayahudi kwanza, na wasio Wayahudi pia.
17 Kwa maana haki ya Mungu imedhihirishwa kutoka imani hata imani, kama ilivyo andikwa, “Mwenye haki ataishi kwa imani.”
Kwa maana Habari Njema inaonyesha wazi jinsi Mungu anavyowakubali watu kuwa waadilifu; jambo hili hufanyika kwa imani, tangu mwanzo mpaka mwisho. Kama ilivyoandikwa: “Mwadilifu kwa imani ataishi.”
18 Maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa watu, ambao kwa njia ya udhalimu huificha kweli.
Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa binadamu ambao kwa njia zao mbaya wanaupinga ukweli usijulikane.
19 Hii ni kwa sababu, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao. Maana Mungu amewafahamisha.
Kwa maana, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao; maana Mungu mwenyewe ameyadhirisha.
20 Maana mambo yake yasioonekana vizuri yamekuwa wazi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Yanaeleweka kupitia vitu vilivyoumbwa. Mambo haya ni uwezo wake wa milele na asili ya uungu. Matokeo yake, watu hawa hawana udhuru. (aïdios g126)
Tangu Mungu alipoumba ulimwengu, uwezo wake wa milele na uungu wake, ingawa havionekani kwa macho, vinafahamika wazi. Watu wanaweza kuyajua mambo hayo kutokana na vitu hivyo alivyoumba Mungu. Kwa hiyo hawana njia yoyote ya kujitetea! (aïdios g126)
21 Hii ni kwa sababu, ingawa walijua kuhusu Mungu, hawakumtukuza yeye kama Mungu, wala hawakumpa shukrani. Badala yake, wamekuwa wapumbavu katika mawazo yao, na mioyo yao yenye ujinga ilitiwa giza.
Ingawa wanajua kuna Mungu, lakini hawampi heshima anayostahili, wala hawamshukuru. Badala yake, fikira zao zimekuwa batili na akili zao tupu zimejaa giza.
22 Walijiita kuwa ni werevu, lakini wakawa wajinga.
Wanajidai kuwa wenye hekima, kumbe ni wapumbavu.
23 Waliubadili utukufu wa Mungu asie na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, ya wanyama wenye miguu minne, na ya viumbe vitambaavyo.
Wanaacha kumwabudu Mungu aishiye milele, na badala yake, wanaabudu sanamu zilizo mfano wa binadamu ambaye hufa, mfano wa wanyama, ndege, au wanyama watambaao.
24 Kwa hiyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa za mioyo yao kwa uchafu, kwa miili yao kufedheheshwa baina yao.
Kwa sababu hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya za mioyo yao na kufanyiana mambo ya aibu kwa miili yao.
25 Ni wao walioibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, na ambao waliabudu na kutumikia viumbe badala ya Muumbaji, ambaye anasifiwa milele. Amina. (aiōn g165)
Wanaubadili ukweli juu ya Mungu kwa uongo; wanaheshimu na kuabudu kiumbe badala ya Muumba mwenyewe, ambaye ndiye astahiliye sifa milele! Amina. (aiōn g165)
26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, kwa kuwa wanawake wao walibadilisha matumizi yao ya asili kwa kile kilicho kinyume na asili.
Kwa hiyo, Mungu amewaacha wafuate tamaa mbaya. Hata wanawake wanabadili matumizi yanayopatana na maumbile.
27 Hali kadhalika, wanaume pia wakaacha matumizi yao ya asili kwa wanawake na kuwakwa na tamaa dhidi yao wenyewe. Hawa walikuwa wanaume ambao walifanya na wanaume wenzao yasiyo wapasa, na ambao walipokea adhabu iliyostahili upotovu wao.
Nao wanaume hali kadhalika, wanaacha kufuata matumizi ya maumbile ya mume na mke wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wanafanyiana mambo ya aibu, na hivyo wanajiletea wenyewe adhabu wanayostahili kwa vitendo vyao viovu.
28 Kwa sababu walikataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye mambo yale yasiyofaa.
Kwa vile watu walikataa kumtambua Mungu, Mungu amewaacha katika fikira zao potovu, wakafanya yale ambayo hawangestahili kufanya.
29 Wamejawa na udhalimu wote, uovu, tamaa na ubaya. Wamejawa na wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu, na nia mbaya.
Wamejaa kila aina ya uovu, dhuluma, ulafi na ufisadi. Wamejaa wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu na nia mbaya; husengenya,
30 Wao pia ni wasengenyaji, wasingiziaji, na wenye kumchukia Mungu. Wenye vurugu, kiburi, na majivuno. Wao ni watunga mabaya, na wasiotii wazazi wao.
na kusingiziana; ni watu wa kuchukiza kwa Mungu, wafidhuli, wenye kiburi na majivuno; hodari sana katika kutenda mabaya, na hawawatii wazazi wao;
31 Wao hawana ufahamu; wasioaminika, hawana mapenzi ya asili, na wasio na huruma.
hawana dhamiri, hawatimizi ahadi zao, hawana wema wala huruma kwa wengine.
32 Wanaelewa kanuni za Mungu, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo wanastahili kifo. Lakini si tu wanafanya mambo hayo, wao pia wanakubaliana na wale wanaofanya mambo hayo.
Wanajua kwamba Sheria ya Mungu yasema kwamba watu wanaoishi mithili hiyo, wanastahili kifo. Zaidi ya hayo, siyo tu kwamba wanafanya mambo hayo wao wenyewe, bali hata huwapongeza wale wanaofanya mambo hayohayo.

< Warumi 1 >