< Warumi 1 >
1 Paulo, mtumishi wa Yesu Kristo, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu.
Paulo, mtumishi wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume na kutengwa kwa ajili ya Injili ya Mungu,
2 Hii ndio ile Injili aliyoiahidi zamani kupitia manabii wake katika maandiko matakatifu.
Injili ambayo Mungu alitangulia kuiahidi kwa vinywa vya manabii wake katika Maandiko Matakatifu,
3 Ni kuhusu Mwana wake, aliyezaliwa kutoka ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili.
yaani, Injili inayomhusu Mwanawe, yeye ambaye kwa uzao wa mwili alikuwa mzao wa Daudi,
4 Yeye alitangazwa kwa Mwana wa Mungu kwa nguvu ya Roho ya utakatifu kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu.
na ambaye kwa uwezo wa Roho wa utakatifu alidhihirishwa kuwa Mwana wa Mungu kwa ufufuo wake kutoka kwa wafu, yaani, Yesu Kristo, Bwana wetu.
5 Kupitia yeye tumepokea neema na utume kwa utii wa imani kati ya mataifa yote, kwa ajili ya jina lake.
Kwa kupitia kwake na kwa ajili ya Jina lake, tumepokea neema na utume ili kuwaita watu miongoni mwa watu wa mataifa yote, waje kwenye utii utokanao na imani.
6 Kati ya mataifa haya, ninyi pia mmeitwa kuwa wa Yesu Kristo.
Ninyi nyote pia mko miongoni mwa watu walioitwa ili mpate kuwa mali ya Yesu Kristo.
7 Barua hii ni kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watu watakatifu. Neema na iwe kwenu, na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.
Kwa wote walioko Rumi wapendwao na Mungu na kuitwa kuwa watakatifu: Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.
8 Kwanza, namshukuru Mungu wangu katika Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inahubiriwa katika dunia nzima.
Kwanza kabisa, namshukuru Mungu wangu kwa njia ya Yesu Kristo kwa ajili yenu nyote, kwa sababu imani yenu inatangazwa duniani kote.
9 Kwa maana Mungu ni shahidi wangu, ambaye ninamtumikia kwa roho yangu katika injili ya Mwana wake, jinsi ninavyodumu katika kuwataja.
Kwa maana Mungu ninayemtumikia kwa moyo wangu wote katika kuhubiri Injili ya Mwanawe, ni shahidi wangu jinsi ninavyowakumbuka
10 Daima naomba katika sala zangu kwamba kwa njia yoyote nipate mwishowe kuwa na mafanikio sasa kwa mapenzi ya Mungu katika kuja kwenu.
katika maombi yangu siku zote, nami ninaomba kwamba hatimaye sasa kwa mapenzi ya Mungu, njia ipate kufunguliwa kwa ajili yangu ili nije kwenu.
11 Maana natamani kuwaona, ili nipate kuwapa ninyi baadhi ya karama za rohoni, nipate kuwaimarisha.
Ninatamani sana kuwaona ili nipate kuweka juu yenu karama za rohoni ili mwe imara,
12 Yaani, natazamia kutiwa moyo pamoja nanyi, kwa njia ya imani ya kila mmoja wetu, yenu na yangu.
au zaidi, ninyi pamoja nami tuweze kutiana moyo katika imani sisi kwa sisi.
13 Sasa ndugu, sitaki mkose kufahamu kwamba, mara nyingi nimekusudia kuja kwenu, lakini nimezuiliwa mpaka sasa. Nilitaka hivi ili kuwa na matunda kwenu kama ilivyo pia miongoni mwa watu wa mataifa.
Ndugu zangu, napenda mfahamu kwamba mara nyingi nimekusudia kuja kwenu (ingawa mpaka sasa nimezuiliwa), ili nipate kuvuna mavuno miongoni mwenu kama nilivyovuna miongoni mwa wengine ambao ni watu wa Mataifa wasiomjua Mungu.
14 Nadaiwa na Wayunani na wageni pia, werevu na wajinga.
Mimi ni mdeni kwa Wayunani na kwa wasio Wayunani, kwa wenye hekima na kwa wasio na hekima.
15 Kwa hiyo, kwa upande wangu, mimi niko tayari kutangaza injili kwenu pia ninyi mlio huko Roma.
Ndiyo sababu ninatamani sana kuihubiri Injili kwenu pia ninyi mlioko Rumi.
16 Kwa maana siionei haya injili, kwa kuwa ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwa Myahudi kwanza na kwa Myunani pia.
Mimi siionei haya Injili ya Kristo kwa maana ni uweza wa Mungu uletao wokovu kwa kila aaminiye, kwanza kwa Myahudi na kwa Myunani pia.
17 Kwa maana haki ya Mungu imedhihirishwa kutoka imani hata imani, kama ilivyo andikwa, “Mwenye haki ataishi kwa imani.”
Kwa maana katika Injili haki itokayo kwa Mungu imedhihirishwa, haki ile iliyo kwa njia ya imani hadi imani. Kama ilivyoandikwa: “Mwenye haki ataishi kwa imani.”
18 Maana ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi na uovu wote wa watu, ambao kwa njia ya udhalimu huificha kweli.
Ghadhabu ya Mungu imedhihirishwa kutoka mbinguni dhidi ya uasi wote na uovu wa wanadamu ambao huipinga kweli kwa uovu wao,
19 Hii ni kwa sababu, yote yanayoweza kujulikana juu ya Mungu ni wazi kwao. Maana Mungu amewafahamisha.
kwa maana yote yanayoweza kujulikana kumhusu Mungu ni dhahiri kwao, kwa sababu Mungu mwenyewe ameyadhihirisha kwao.
20 Maana mambo yake yasioonekana vizuri yamekuwa wazi tangu kuumbwa kwa ulimwengu. Yanaeleweka kupitia vitu vilivyoumbwa. Mambo haya ni uwezo wake wa milele na asili ya uungu. Matokeo yake, watu hawa hawana udhuru. (aïdios )
Kwa maana tangu kuumbwa kwa ulimwengu, asili ya Mungu asiyeonekana kwa macho, yaani, uweza wake wa milele na asili yake ya Uungu, imeonekana waziwazi, ikitambuliwa kutokana na yale aliyoyafanya ili wanadamu wasiwe na udhuru. (aïdios )
21 Hii ni kwa sababu, ingawa walijua kuhusu Mungu, hawakumtukuza yeye kama Mungu, wala hawakumpa shukrani. Badala yake, wamekuwa wapumbavu katika mawazo yao, na mioyo yao yenye ujinga ilitiwa giza.
Kwa maana ingawa walimjua Mungu, hawakumtukuza yeye kama ndiye Mungu wala hawakumshukuru, bali fikira zao zimekuwa batili na mioyo yao ya ujinga ikatiwa giza.
22 Walijiita kuwa ni werevu, lakini wakawa wajinga.
Ingawa walijidai kuwa wenye hekima, wakawa wajinga
23 Waliubadili utukufu wa Mungu asie na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege, ya wanyama wenye miguu minne, na ya viumbe vitambaavyo.
na kubadili utukufu wa Mungu aishiye milele kwa sanamu zilizofanywa zifanane na mwanadamu ambaye hufa, na mfano wa ndege, wanyama na viumbe vitambaavyo.
24 Kwa hiyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa za mioyo yao kwa uchafu, kwa miili yao kufedheheshwa baina yao.
Kwa hiyo, Mungu akawaacha wazifuate tamaa mbaya za mioyo yao katika uasherati, hata wakavunjiana heshima miili yao wao kwa wao.
25 Ni wao walioibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, na ambao waliabudu na kutumikia viumbe badala ya Muumbaji, ambaye anasifiwa milele. Amina. (aiōn )
Kwa sababu waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakaabudu na kutumikia kiumbe badala ya Muumba, ahimidiwaye milele! Amen. (aiōn )
26 Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, kwa kuwa wanawake wao walibadilisha matumizi yao ya asili kwa kile kilicho kinyume na asili.
Kwa sababu hii, Mungu aliwaacha wavunjiane heshima kwa kufuata tamaa zao za aibu. Hata wanawake wao wakabadili matumizi ya asili ya miili yao wakaitumia isivyokusudiwa.
27 Hali kadhalika, wanaume pia wakaacha matumizi yao ya asili kwa wanawake na kuwakwa na tamaa dhidi yao wenyewe. Hawa walikuwa wanaume ambao walifanya na wanaume wenzao yasiyo wapasa, na ambao walipokea adhabu iliyostahili upotovu wao.
Vivyo hivyo wanaume pia wakiacha matumizi ya asili ya wanawake wakawakiana tamaa wao kwa wao. Wanaume wakafanyiana matendo ya aibu na wanaume wengine nao wakapata katika maisha yao adhabu iliyowastahili kwa ajili ya upotovu wao.
28 Kwa sababu walikataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wafanye mambo yale yasiyofaa.
Nao kwa kuwa hawakuona umuhimu wa kudumisha ufahamu wa Mungu, yeye akawaachilia wafuate akili za upotovu, watende mambo yale yasiyostahili kutendwa.
29 Wamejawa na udhalimu wote, uovu, tamaa na ubaya. Wamejawa na wivu, uuaji, ugomvi, udanganyifu, na nia mbaya.
Wakiwa wamejawa na udhalimu wa kila namna, uasherati, uovu, tamaa mbaya na hila. Wamejawa na husuda, uuaji, ugomvi, udanganyifu, hadaa na nia mbaya. Wao pia ni wasengenyaji,
30 Wao pia ni wasengenyaji, wasingiziaji, na wenye kumchukia Mungu. Wenye vurugu, kiburi, na majivuno. Wao ni watunga mabaya, na wasiotii wazazi wao.
wasingiziaji, wanaomchukia Mungu, wajeuri, wenye kiburi na majivuno, wenye hila, wasiotii wazazi wao,
31 Wao hawana ufahamu; wasioaminika, hawana mapenzi ya asili, na wasio na huruma.
wajinga, wasioamini, wasio na huruma na wakatili.
32 Wanaelewa kanuni za Mungu, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo wanastahili kifo. Lakini si tu wanafanya mambo hayo, wao pia wanakubaliana na wale wanaofanya mambo hayo.
Ingawa wanafahamu sheria ya haki ya Mungu kwamba watu wanaofanya mambo kama hayo wanastahili mauti, si kwamba wanaendelea kutenda hayo tu, bali pia wanakubaliana na wale wanaoyatenda.