< Ufunuo 3 >
1 Kwa malaika wa kanisa la Sardi andika: 'Maneno ya yule anayeshikilia zile roho saba za Mungu na nyota saba. “Najua ambacho umefanya. Una sifa ya kuwa hai, lakini u-mfu.
2 Amka na kuimarisha yaliyosalia, lakini yako karibu kufa, kwa sababu sikuyaona matendo yako yamekamilika machoni pa Mungu wangu.
3 Kwa hiyo, kumbuka, yale uliyoyapokea na kusikia. Yatii na kutubu. Lakini usipoamka, nitakuja kama mwivi, na hutajua saa ipi nitakayokuja juu yako.
4 Lakini kuna majina machache ya watu katika Sardi ambao hawakuchafua nguo zao. Watatembea pamoja nami, wamevaa nguo nyeupe, kwa sababu wanastahili.
5 Yeye ashindaye atavikwa mavazi meupe, na kamwe sitalifuta jina lake kutoka katika kitabu cha uzima, na nitalitaja jina lake mbele ya Baba yangu, na mbele ya malaika.
6 Ukiwa na sikio, sikiliza Roho ayaambiavyo makanisa.”
7 “Kwa malaika wa kanisa la Philadefia andika: Maneno ya aliye mtakatifu na kweli - aliye na funguo za Daudi, hufungua na hakuna afungaye, hufunga na hakuna awezaye kufungua.
8 Najua ambacho umetenda. Tazama, nimekuwekea mbele yako mlango uliofunguliwa ambao hakuna awezaye kuufunga. Najua unazo nguvu kidogo, lakini umelitii neno langu na hujalikana jina langu.
9 Angalia! Wote walio wa sinagogi la shetani, wale wasemao wao ni Wayahudi na kumbe siyo, badala yake wanadanganya. Nitawafanya waje na kusujudu mbele ya miguu yako, na watajua ya kuwa nilikupenda.
10 Kwa kuwa umetunza amri yangu kwa uvumilivu wa uthabiti, nitakulinda pia katika saa yako ya kujaribiwa ambayo inakuja katika ulimwengu wote, kuwajaribu wale wote wanaoishi katika nchi.
11 Naja upesi. Shikilia sana kile ulichonacho ili asiwepo mtu wa kuitwaa taji yako.
12 Nitamfanya yeye ashindaye kuwa nguzo katika hekalu la Mungu wangu, na hatatoka nje kamwe. Nitaliandika kwake jina la Mungu wangu, jina la mji wa Mungu wangu (Yerusalemu mpya, ushukao chini toka mbinguni kwa Mungu wangu), na jina langu jipya.
13 Yeye aliye na sikio, na asikie ambacho Roho anasema kwa makanisa.'
14 “Kwa malaika wa kanisa la Laodikia andika: 'Maneno yake aliye Amina, wakutegemewa na shahidi mwaminifu, mtawala juu ya uumbaji wa Mungu.
15 Najua ambacho umefanya, na kwamba wewe si baridi wala moto, natamani kwamba ungekuwa wa baridi au moto!
16 Hivyo, kwa sababu wewe ni vuguvugu, si moto wala baridi, nitakutapika utoke kinywani mwangu.
17 Kwa kuwa unasema, “Mimi ni tajiri, nimekuwa na mali nyingi, na sihitaji chochote.” Lakini hujui kwamba wewe ni duni sana, wakuhuzunikiwa, maskini, kipofu na uchi.
18 Sikiliza ushauri kwangu: Nunua kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto ili upate kuwa tajiri, na nguo nyeupe za kumetameta ili ujivike mwenyewe na usioneshe aibu ya uchi wako, na mafuta ya kupaka katika macho yako upate kuona.
19 Kila nimpendaye, namwelekeza na kuwafundisha namna iwapasavyo kuishi; kwa hiyo, kuwa mkweli na kutubu.
20 Tazama nasimama katika mlango na kubisha. Yeyote asikiaye sauti yangu na kufungua mlango, nitakuja na kuingia nyumbani kwake, na kula chakula naye na yeye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa haki ya kukaa chini pamoja nami juu ya kiti changu cha enzi, kama vile mimi nilivyoshinda na kukaa chini pamoja na Baba yangu juu ya kiti chake cha enzi.
22 Yeye aliye na sikio, na asikilize ambacho Roho ayaambia makanisa.”