< Ufunuo 19 >

1 Baada ya mambo haya nilisikia sauti kama ya mlio mkubwa wa kundi kubwa la watu mbinguni ikisema, “Haleluya. Wokovu, utukufu, na nguvu ni vya Mungu wetu.
Baada ya haya nikasikia sauti kama ya umati mkubwa mbinguni wakipiga kelele wakisema: “Haleluya! Wokovu na utukufu na uweza ni vya Mungu wetu,
2 Hukumu zake ni kweli na za haki, kwa kuwa amemhukumu kahaba mkuu aliyeiharibu nchi kwa uzinzi wake. Amefanya kisasi kwa damu ya watumishi wake, ambayo aliimwaga yeye mwenyewe.”
kwa maana hukumu zake ni za kweli na za haki. Amemhukumu yule kahaba mkuu aliyeuharibu ulimwengu kwa uzinzi wake. Mungu amemlipiza kisasi kwa ajili ya damu ya watumishi wake.”
3 Kwa mara ya pili walisema, “Haleluya! Moshi hutoka kwake milele na milele.” (aiōn g165)
Wakasema tena kwa nguvu: “Haleluya! Moshi wake huyo kahaba unapanda juu milele na milele.” (aiōn g165)
4 Wale wazee ishirini na wanne na viumbe hai wanne wakasujudu na kumwabudu Mungu akaaye kwenye kiti cha enzi. Walikuwa wakisema, “Amina. Haleluya!”
Wale wazee ishirini na wanne pamoja na wale viumbe wanne wenye uhai wakaanguka kifudifudi, wakamwabudu Mungu, aliyekuwa ameketi kwenye kile kiti cha enzi. Wakasema kwa sauti kuu: “Amen, Haleluya!”
5 Ndipo sauti ilitoka kwenye kiti cha enzi, ikisema, “Msifuni Mungu wetu, enyi watumishi wake wote, ninyi mnaomcha yeye, wote wasio na umuhimu na wenye nguvu.”
Kisha sauti ikatoka katika kile kiti cha enzi, ikisema: “Msifuni Mungu wetu, ninyi watumishi wake wote, ninyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa!”
6 Ndipo nilisikia sauti kama sauti ya kundi kubwa la watu, kama sauti ya ngurumo ya maji mengi, na kama ngurumo ya radi, ikisema, “Haleluya! Bwana ni Mungu wetu, mtawala juu ya wote, hutawala.
Kisha nikasikia sauti kama ya umati mkubwa, kama sauti ya maji mengi yaendayo kasi na kama ngurumo kubwa ya radi wakipiga kelele wakisema: “Haleluya! Kwa maana Bwana Mungu wetu Mwenyezi anatawala.
7 Na tushangilie na kufurahi na kumpa utukufu kwa sababu harusi na sherehe ya Mwana Kondoo imekuja, na bibi harusi yuko tayari.”
Tufurahi, tushangilie na kumpa utukufu! Kwa maana arusi ya Mwana-Kondoo imewadia na bibi arusi wake amejiweka tayari.
8 Aliruhusiwa kuvalishwa kitani safi na yenye kung'aa (kitani safi ni matendo ya haki ya waumini).
Akapewa kitani safi, nyeupe inayongʼaa, ili avae.” (Hiyo kitani safi inawakilisha matendo ya haki ya watakatifu.)
9 Malaika akasema nami, “Yaandike haya: Wamebarikiwa walioalikwa kwenye sherehe ya harusi ya Mwana kondoo.” Vilevile akaniambia, “Haya ni maneno ya kweli ya Mungu.”
Ndipo malaika akaniambia, “Andika: ‘Wamebarikiwa wale walioalikwa kwenye karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo!’” Naye akaongeza kusema, “Haya ndiyo maneno ya kweli ya Mungu.”
10 Nilisujudu mbele ya miguu yake nikamwabudu, lakini akaniambia, “Usifanye hivi! Mimi ni mtumishi mwenzako na wa ndugu zako mwenye kuushika ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu, kwa kuwa ushuhuda wa Yesu ni roho ya unabii.”
Ndipo nikaanguka kifudifudi miguuni pake ili kumwabudu, lakini yeye akaniambia, “Usifanye hivyo! Mimi pia ni mtumishi mwenzako pamoja na ndugu zako walio na ushuhuda wa Yesu. Mwabudu Mungu! Maana ushuhuda wa Yesu ndio roho ya unabii.”
11 Kisha niliona mbingu zimefunguka, na tazama kulikuwa na farasi mweupe! Na yule aliyekuwa amempanda anaitwa Mwaminifu na wa Kweli. Huhukumu kwa haki na kufanya vita.
Kisha nikaona mbingu imefunguka na hapo mbele yangu akiwepo farasi mweupe, ambaye yeye aliyempanda aliitwa Mwaminifu na Kweli. Yeye huhukumu kwa haki na kufanya vita.
12 Macho yake ni kama mwali wa moto, na juu ya kichwa chake ana taji nyingi. Ana jina lililoandikwa juu yake asilolifahamu mtu yeyote isipokuwa yeye mwenyewe.
Macho yake ni kama miali ya moto na juu ya kichwa chake kuna taji nyingi. Ana jina lililoandikwa ambalo hakuna mtu yeyote anayelijua isipokuwa yeye mwenyewe.
13 Amevaa vazi lililochovywa katika damu, na jina lake aliitwa Neno la Mungu.
Amevaa joho lililochoviwa katika damu, na Jina lake ni “Neno la Mungu.”
14 Majeshi ya mbinguni yalikuwa yakimfuata juu ya farasi weupe, walivalishwa kitani nzuri, nyeupe na safi.
Majeshi ya mbinguni walikuwa wakimfuata, wakiwa wamepanda farasi weupe, hali wamevaa mavazi ya kitani safi, nyeupe na nzuri.
15 Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao huyaangamiza mataifa, naye atawatawala kwa fimbo ya chuma. Naye hukanyaga vyombo vya mvinyo kwa hasira kali ya Mungu, hutawala juu ya wote.
Kinywani mwake hutoka upanga mkali ambao kwa huo atayaangusha mataifa. “Atayatawala kwa fimbo yake ya utawala ya chuma.” Hulikanyaga shinikizo la mvinyo wa ghadhabu ya Mungu Mwenyezi.
16 Naye ameandikwa juu ya vazi lake na katika paja lake jina, MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA.
Kwenye joho lake na paja lake pameandikwa jina hili: Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana.
17 Niliona malaika amesimama katika jua. Aliwaita kwa sauti kuu ndege wote warukao juu, “Njoni, kusanyikeni pamoja kwenye chakula kikuu cha Mungu.
Nami nikamwona malaika amesimama ndani kwenye jua, akaita ndege wote warukao angani kwa sauti kuu, “Njooni, kusanyikeni kwa ajili ya karamu kubwa ya Mungu,
18 Njoni mle nyama ya wafalme, nyama ya majemedari, nyama ya watu wakubwa, nyama ya farasi na wapanda farasi, na nyama ya watu wote, walio huru na watumwa, wasio na umuhimu na wenye nguvu.”
ili mpate kula nyama ya wafalme na ya majemadari, ya mashujaa, ya farasi na ya wapanda farasi, nyama ya wanadamu, wote walio huru na watumwa, wadogo na wakubwa.”
19 Nilimwona mnyama na wafalme wa nchi pamoja na majeshi yao. Walikuwa wamejipanga kwa ajili ya kufanya vita na mmoja aliyepanda farasi na jeshi lake.
Kisha nikamwona yule mnyama na wafalme wa dunia pamoja na majeshi yao wakiwa wamekusanyika pamoja ili kufanya vita dhidi ya yule aliyempanda farasi pamoja na jeshi lake.
20 Mnyama alikamatwa na nabii wake wa uongo aliyezifanya ishara katika uwepo wake. Kwa ishara hizi aliwadanganya wale walioipokea chapa ya mnyama na walioisujudia sanamu yake. Wote wawili walitupwa wangali hai katika ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. (Limnē Pyr g3041 g4442)
Lakini yule mnyama akakamatwa pamoja na huyo nabii wa uongo ambaye alikuwa amefanya ishara kwa niaba ya huyo mnyama, ambaye kwa ishara hizi aliwadanganya wale waliopokea chapa ya huyo mnyama na kuiabudu sanamu yake. Hawa wawili wakatupwa wakiwa hai ndani ya ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti. (Limnē Pyr g3041 g4442)
21 Wale waliobaki waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa mmoja aliyepanda juu ya farasi. Ndege wote walikula mizoga ya miili yao.
Wale waliosalia waliuawa kwa upanga uliotoka kinywani mwa yule aliyekuwa amempanda farasi nao ndege wote wakajishibisha kwa nyama yao.

< Ufunuo 19 >