< Ufunuo 18 >
1 Baada ya vitu hivi nilimwona malaika mwingine akishuka chini kutoka mbinguni. Yeye alikuwa na mamlaka kuu, na nchi iliangazwa kwa utukufu wake.
2 Alilia kwa sauti kuu, akisema, “Umeanguka, umeanguka, ule mji mkuu Babeli! Umekuwa sehemu yakaapo mapepo, na sehemu ikaapo kila roho chafu, na sehemu akaapo kila mchafu na ndege achukizaye.
3 Kwa kuwa mataifa yote yamekunywa mvinyo ya tamaa ya uasherati wake ambayo humletea ghadhabu. Wafalme wa nchi wamezini naye. Wafanyabiashara wa nchi wamekuwa matajiri kwa nguvu ya maisha yake ya anasa.”
4 Kisha nilisikia sauti nyingine kutoka mbinguni iikisema, “Tokeni kwake watu wangu, ili msije mkashiriki katika dhambi zake, na ili msije mkapokea mapigo yake yoyote.
5 Dhambi zake zimerundikana juu kama mbingu, na Mungu ameyakumbuka matendo yake maovu.
6 Mlipeni kama alivyowalipa wengine, na mkamlipe mara mbili kwa jinsi alivyotenda; katika kikombe alichokichanganya, mchanganyishieni mara mbili kwa ajili yake.
7 Kama alivyojitukuza yeye mwenyewe, na aliishi kwa anasa, mpeni mateso mengi na huzuni. Kwa kuwa husema moyoni mwake, 'Nimekaa kama malkia; wala siyo mjane, na wala sitaona maombolezo.'
8 Kwa hiyo ndani ya siku moja mapigo yake yatamlemea: kifo, maombolezo, na njaa. Atateketezwa kwa moto, kwa kuwa Bwana Mungu ni mwenye nguvu, na ni mhukumu wake.”
9 Wafalme wa nchi waliozini na kuchanganyikiwa pamoja naye watalia na kumwombolezea watakapouona moshi wa kuungua kwake.
10 Watasimama mbali naye, kwa hofu ya maumivu yake wakisema, “Ole, ole kwa mji mkuu, Babeli, mji wenye nguvu! Kwa saa moja hukumu yako imekuja.”
11 Wafanyabiashara wa nchi lieni na kuomboleza kwa ajili yake, kwa kuwa hakuna hata mmoja anunuaye bidhaa zake tena -
12 bidhaa za dhahabu, fedha, mawe ya thamani, lulu, kitani nzuri, zambarau, hariri, nyekundu, aina zote za miti ya harufu nzuri, kila chombo cha pembe za ndovu, kila chombo kilichotengenezwa kwa miti ya thamani, shaba, chuma, jiwe,
13 mdalasini, viungo, uvumba, manemane, ubani, mvinyo, mafuta, unga mzuri, ngano, ng'ombe na kondoo, farasi na magari, na watumwa, na roho za watu.
14 Matunda uliyoyatamani kwa nguvu zako yameondoka kutoka kwako. Anasa zako zote na mapambo yametoweka, hayatapatikana tena.
15 Wafanyabiashara wa vitu hivi waliopata utajiri kwa mapenzi yake watasimama mbali kutoka kwake kwa sababu ya hofu ya maumivu yake, wakilia na sauti ya maombolezo.
16 Wakisema, “Ole, ole mji ule mkuu uliovikwa kitani nzuri, zambarau, na nyekundu, na kupambwa kwa dhahabu, na vito vya thamani na lulu!”
17 Ndani ya saa moja utajiri wote huo ulitoweka. Kila nahodha wa meli, kila baharia, na wote wanamaji, na wote wafanyao kazi baharini, walisimama mbali.
18 Walilia walipouona moshi wa kuungua kwake. Walisema, “Ni mji gani unafanana na mji huu mkubwa?”
19 Walitupa mavumbi juu ya vichwa vyao, na walilia, wakitokwa machozi na kuomboleza, “Ole, ole mji mkubwa mahali wote waliokuwa na meli zao baharini walikuwa matajiri kutokana na mali zake. Ndani ya saa moja umeangamizwa.”
20 “Furahini juu yake, mbingu, ninyi waumini, mitume, na manabii, kwa maana Mungu ameleta hukumu yenu juu yake!”
21 Malaika mwenye nguvu aliinua jiwe kama jiwe kuu la kusagia na alilitupa baharini, akisema, “Kwa njia hii, Babeli, ule mji mkuu, utatupwa chini kwa ukatili na hautaonekana tena.
22 Sauti ya vinanda, wanamuziki, wacheza filimbi, na tarumbeta hawatasikika tena kwenu. Wala fundi wa aina yoyote hataonekana kwenu. Wala sauti ya kinu haitasikika tena kwenu.
23 Mwanga wa taa hautaangaza ndani yako. Sauti ya bwana harusi na bibi harusi hazitasikiwa tena ndani yako, maana wafanyabiashara wako walikuwa wakuu wa nchi, na wa mataifa, wamedanganywa kwa uchawi wako.
24 Ndani yake damu ya manabii na waamini ilionekana, na damu ya wote waliouawa juu ya nchi.”