< Ufunuo 16 >
1 Nikasikia sauti kubwa ikiita kutoka kwenye sehemu ya patakatifu na ikasema kwa wale malaika saba, “Nenda na ukamwage juu ya dunia mabakuli saba ya ghadhabu ya Mungu.”
2 Malaika wa kwanza alienda na kumwaga bakuli lake katika dunia; majeraha mabaya na yenye maumivu makali yalikuja kwa watu wenye alama ya mnyama, kwa wale ambao waliabudu sanamu yake.
3 Malaika wa pili alimwaga bakuli lake katika bahari; ikawa kama damu ya mtu aliyekufa, na kila kiumbe hai katika bahari kilikufa.
4 Malaika wa tatu akamwaga bakuli lake katika mito na katika chemichemi za maji; zikawa damu.
5 Nikasikia malaika wa maji akisema, “Wewe ni mwaminifu - mmoja uliyepo na uliyekuwako, Mtakatifu - kwa sababu umezileta hukumu hizi.
6 Kwa sababu walimwaga damu za waamini na manabii, umewapa wao kunywa damu; ndicho wanachostahili.”
7 Nikasikia madhabahu ikijibu, “Ndiyo! Bwana Mungu mwenye kutawala juu ya vyote, hukumu zako ni kweli na za haki.”
8 Malaika wa nne akamwaga kutoka kwenye bakuli lake juu ya jua, na likapewa ruhusa kuunguza watu kwa moto.
9 Waliunguzwa kwa joto lenye kutisha, na wakalikufuru neno la Mungu, mwenye nguvu juu ya mapigo yote. Hawakutubu wala kumpa yeye utukufu.
10 Malaika wa tano akamwaga kutoka kwenye bakuli lake katika kiti cha enzi cha mnyama, na giza likaufunika ufalme wake. Walisaga meno katika maumivu makali.
11 Wakamtukana Mungu wa mbinguni kwa sababu ya maumivu yao na majeraha yao, na bado waliendelea kutokutubu kwa kile walichotenda.
12 Malaika wa sita alimwaga kutoka kwenye bakuli lake katika mto mkubwa, Frati, na maji yake yakakauka ili kuweza kuandaa njia kwa wafalme watakaokuja kutoka mashariki.
13 Nikaona roho tatu chafu zilizoonekana kama chura watokao nje ya mdomo wa yule joka, yule mnyama, na yule nabii wa uongo.
14 Ni roho za pepo zitendazo ishara na miujiza. Walikuwa wakienda kwa wafalme wa dunia yote ili kuweza kuwakusanya pamoja kwa vita katika siku kuu ya Mungu, mwenye kutawala juu ya vyote.
15 (“Tazama! Ninakuja kama mwizi! Heri yule adumuye katika kukesha, atunzaye mavazi yake ili asiweze kwenda nje uchi na kuiona aibu yake.”)
16 Waliwaleta pamoja katika sehemu iliyoitwa katika kiebrania Amagedoni.
17 Malaika wa saba alimwaga kutoka kwenye bakuli lake katika anga. Kisha sauti kuu ikasikika kutoka pakatifu na kutoka kwenye kiti cha enzi, ikisema, “Imekwisha!”
18 Kulikuwa na miale ya mwanga wa radi, ngurumo, vishindo vya radi, na tetemeko la kutisha - tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijawahi kutokea duniani tangu wanadamu wamekuwepo duniani, hivyo ni tetemeko kubwa zaidi.
19 Mji mkuu uligawanyika katika sehemu tatu, na miji ya mataifa ikaanguka. Kisha Mungu akamkumbusha Babeli mkuu, na akaupa mji huo kikombe kilichokuwa kimejaa divai kutoka kwenye ghadhabu yake iliyo kali.
20 Kila kisiwa kikapotea na milima haikuonekana tena.
21 Mvua kubwa ya mawe, ikiwa na uzito wa talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya watu, na wakamlaani Mungu kwa mapigo ya mvua ya mawe kwa sababu lile pigo lilikuwa baya sana.