< Ufunuo 10 >
1 Kisha nikaona malaika mwingine mkuu akishuka chini kutoka mbinguni. Alikuwa amefungwa katika wingu, na kulikuwa na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake ulikuwa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.
Kisha nikamwona malaika mwingine mwenye nguvu akishuka kutoka mbinguni. Alikuwa amevikwa wingu na upinde wa mvua juu ya kichwa chake. Uso wake ulingʼaa kama jua na miguu yake ilikuwa kama nguzo za moto.
2 Alishikilia gombo dogo katika mkono wake lililokuwa limefunuliwa, naye aliweka mguu wake wa kulia juu ya bahari na mguu wake wa kushoto juu ya nchi kavu.
Mkononi mwake alikuwa ameshika kijitabu kilichokuwa kimefunguliwa. Akauweka mguu wake wa kuume juu ya bahari na mguu wake wa kushoto akauweka juu ya nchi kavu.
3 Kisha alipaza sauti ya juu kama simba aungurumapo, na wakati alipopaza sauti radi saba ziliunguruma.
Naye akapiga kelele kwa sauti kuu kama simba anayenguruma. Alipopiga kelele, zile radi saba zikatoa ngurumo zake.
4 Wakati radi saba zilipounguruma, nilikuwa nakaribia kuandika, lakini nilisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Tunza iwe siri kile ambacho radi saba zimesema. Usiiandike.”
Nazo zile radi saba zilipotoa ngurumo, nilitaka kuanza kuandika, lakini nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, “Yatie muhuri hayo yaliyosemwa na hizo radi saba na usiyaandike.”
5 Kisha malaika niliyemwona amesimama juu ya bahari na nchi kavu, aliinua mkono wake juu mbinguni
Kisha yule malaika niliyekuwa nimemwona akiwa amesimama juu ya bahari na juu ya nchi akainua mkono wake wa kuume kuelekea mbinguni.
6 na kuapa kwa yule aishiye milele na milele —aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote vilivyomo, na bahari na vyote vilivyomo: “Hakutakuwepo kuchelewa tena. (aiōn )
Naye akaapa kwa Yule aishiye milele na milele, aliyeumba mbingu na vyote vilivyomo, dunia na vyote viijazavyo, pamoja na bahari na vyote vilivyomo ndani yake, akasema, “Hakuna kungoja tena! (aiōn )
7 Lakini katika siku ile, wakati malaika wa saba atakapokaribia kupiga tarumbeta yake, ndipo siri ya Mungu itakuwa imetimizwa, kama alivyotangaza kwa watumishi wake manabii.”
Lakini katika siku zile ambazo huyo malaika wa saba atakapokaribia kuipiga hiyo tarumbeta yake, siri ya Mungu itatimizwa, kama vile alivyowatangazia watumishi wake manabii.”
8 Sauti niliyosikia kutoka mbinguni iliniambia tena: “Nenda, chukua gombo dogo lililofunuliwa ambalo kiko katika mkono wa malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu.”
Ndipo ile sauti niliyokuwa nimeisikia kutoka mbinguni ikasema nami tena ikaniambia, “Nenda, chukua kile kitabu kilichofunguliwa kilichoko mkononi mwa yule malaika aliyesimama juu ya bahari na juu ya nchi kavu.”
9 Kisha nilikwenda kwa malaika na kumwambia anipe gombo dogo. Aliniambia, “Chukua gombo na ule. Litalifanya tumbo lako liwe na uchungu, lakini katika mdomo wako litakuwa tamu kama asali.”
Basi nikamwendea nikamwomba yule malaika anipe kile kitabu kidogo. Akaniambia, “Chukua na ukile. Kitakuwa kichungu tumboni mwako, lakini kinywani mwako kitakuwa kitamu kama asali.”
10 Nilichukua gombo dogo kutoka mkononi mwa malaika na kulila. Lilikuwa kitamu kama asali katika mdomo wangu, lakini baada ya kula, tumbo langu lilikuwa na uchungu.
Hivyo nikakichukua kile kitabu kidogo kutoka mkononi mwa yule malaika nikakila. Kilikuwa kitamu kama asali kinywani mwangu, lakini baada ya kukila, tumbo langu likatiwa uchungu.
11 Kisha baadhi ya sauti ziliniambia, “Unapaswa kutabiri tena kuhusu watu wengi, mataifa, lugha, na wafalme.”
Kisha nikaambiwa, “Imekupasa kutoa unabii tena kuhusu makabila mengi, mataifa, lugha na wafalme.”