< Ufunuo 1 >
1 Huu ni ufunuo wa Yesu Kristo ambao Mungu alimpa ili kuwaonesha watumishi wake mambo ambayo lazima yatokee karibuni. Aliyafanya yajulikane kwa kumtuma malaika wake kwa mtumishi wake Yohana.
2 Yohana alitoa ushuhuda wa kila kitu alichoona kuhusiana na neno la Mungu na kwa ushuhuda uliotolewa kuhusu Yesu Kristo.
3 Amebarikiwa yeye asomaye kwa sauti na wale wote wanaoyasikia maneno ya unabii huu na kutii kilichoandikwa humo, kwa sababu muda umekaribia.
4 Yohana, kwa makanisa saba yaliyoko Asia: neema iwe kwenu na amani kutoka kwake aliyepo, aliyekuwepo, na atakayekuja, na kutoka kwa roho saba walio mbele ya kiti chake cha enzi,
5 na kutoka kwa Yesu Kristo ambaye ni shahidi mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mtawala wa wafalme wa dunia hii. Kwake yeye atupendaye na ametuweka huru kutoka katika dhambi zetu kwa damu yake,
6 ametufanya kuwa ufalme, makuhani wa Mungu na Baba yake - kwake kuwa utukufu na nguvu milele daima. Amina. (aiōn )
7 Tazama, anakuja na mawingu; kila jicho litamwona, pamoja na wote waliomchoma. Na kabila zote za dunia wataomboleza kwake. Ndiyo, Amina.
8 “Mimi ni Alfa na Omega,” asema Bwana Mungu, “Yeye aliyepo, na aliyekuwepo, na ambaye anakuja, Mwenye nguvu.”
9 Mimi, Yohana - ndugu yenu na mmoja anayeshiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na uvumilivu thabiti ulio katika Yesu; nilikuwa katika kisiwa kiitwacho Patimo kwa sababu ya neno la Mungu na ushuhuda kuhusu Yesu.
10 Nilikuwa katika Roho siku ya Bwana. Nilisikia nyuma yangu sauti ya juu kama ya tarumbeta,
11 ikisema, “andika katika kitabu unayo yaona, na uyatume kwa makanisa saba, kwenda Efeso, kwenda Smirna, kwenda Pergamo, kwenda Thiatira, kwenda Sardi, kwenda Philadelphia, na kwenda Laodikia.”
12 Nikageuka kuona ni sauti ya nani aliyekuwa akiongea nami, na nilipogeuka niliona kinara cha dhahabu cha taa saba.
13 Katikati ya kinara cha taa alikuwemo mmoja kama Mwana wa Adamu, amevaa kanzu ndefu iliyofika chini ya miguu yake, na mkanda wa dhababu kuzunguka kifua chake.
14 Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe kama theluji, na macho yake yalikuwa kama mwali wa moto.
15 Nyayo zake zilikuwa kama shaba iliyosuguliwa sana, kama shaba ambayo imekwisha pitishwa katika moto, na sauti yake ilikuwa kama sauti ya maji mengi yanayotiririka kwa kasi.
16 Alikuwa ameshikilia nyota saba katika mkono wake wa kuume, na kutoka kinywani mwake kulikuwa na upanga mkali wenye makali kuwili. Uso wake ulikuwa uking'aa kama mwanga mkali wa jua.
17 Nilipomwona, nikaanguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa kulia juu yangu na kusema, “Usiogope! Mimi ni wa kwanza na wa Mwisho,
18 na ambaye ninaishi. Nalikuwa nimekufa, lakini tazama, ninaishi milele! Na ninazo funguo za mauti na kuzimu. (aiōn , Hadēs )
19 Kwa hiyo, yaandike uliyoyaona, yaliyopo sasa, na yale yatakayotokea baada ya haya.
20 Kwa maana iliyojificha kuhusu nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na kile kinara cha dhahabu cha taa saba: nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba, na kinara cha taa saba ni yale makanisa saba.”