< Zaburi 97 >

1 Yahwe anatawala; nchi ishangilie; visiwa vingi na vifurahi.
Bwana anatawala, nchi na ifurahi, visiwa vyote vishangilie.
2 Mawingu na giza vyamzunguka. Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake.
Mawingu na giza nene vinamzunguka, haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake cha enzi.
3 Moto huenda mbele zake nao huwateketeza adui zake pande zote.
Moto hutangulia mbele zake na huteketeza adui zake pande zote.
4 Taa yake huangaza ulimwengu; nchi huona na kutetemeka.
Umeme wake wa radi humulika dunia, nchi huona na kutetemeka.
5 Milima huyeyuka kama nta mbele za Yahwe, Bwana wa dunia yote.
Milima huyeyuka kama nta mbele za Bwana, mbele za Bwana wa dunia yote.
6 Mbingu hutangaza haki yake, na mataifa yote huuona utukufu wake.
Mbingu zinatangaza haki yake, na mataifa yote huona utukufu wake.
7 Wale wote waabuduo sanamu za kuchonga wataaibishwa, wale wanao jivuna katika sanamu zisizo na maana mpigieni yeye magoti, enyi miungu wote!
Wote waabuduo sanamu waaibishwa, wale wajisifiao sanamu: mwabuduni yeye, enyi miungu yote!
8 Sayuni ilisikia na kufurahi, na miji ya Yuda ilishangilia kwa sababu ya amri zako za haki, Yahwe.
Sayuni husikia na kushangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako, Ee Bwana.
9 Kwa kuwa wewe, Yahwe, ndiye uliye juu sana, juu ya nchi yote. Umetukuka sana juu ya miungu yote.
Kwa kuwa wewe, Ee Bwana, ndiwe Uliye Juu Sana kuliko dunia yote; umetukuka sana juu ya miungu yote.
10 Ninyi ambao mnampenda Yahwe, chukieni uovu! Yeye hulinda uhai wa watakatifu wake, naye huwatoa mikononi mwa waovu.
Wale wanaompenda Bwana na wauchukie uovu, kwa maana yeye hulinda maisha ya waaminifu wake na kuwaokoa kutoka mkononi mwa mwovu.
11 Nuru imepandwa kwa ajili ya wenye haki na furaha kwa ajili ya wanyoofu wa moyo.
Nuru huangaza wenye haki na furaha kwa watu wanyofu wa moyo.
12 Furahini katika Yahwe, enyi wenye haki; na mpeni shukurani mkumbukapo utakatifu wake.
Furahini katika Bwana, ninyi mlio wenye haki, lisifuni jina lake takatifu.

< Zaburi 97 >