< Zaburi 94 >

1 Yahwe, Ee Mungu ulipaye kisasi, Mungu ulipaye kisasi, utuangazie sisi.
Ee Bwana, ulipizaye kisasi, Ee Mungu ulipizaye kisasi, uangaze sasa.
2 Inuka, muhukumu wa nchi, uwape wenye majivuno kile wanachosahili.
Ee Mhukumu wa dunia, inuka, uwalipize wenye kiburi kama wanavyostahili.
3 Mpaka lini waovu, Yahwe, mpaka lini waovu watafurahia?
Hata lini, waovu, Ee Bwana, hata lini waovu watashangilia?
4 Wanamwaga maneno yao ya kiburi; wote watendao uovu wanajivuna.
Wanamimina maneno ya kiburi, watenda mabaya wote wamejaa majivuno.
5 Wanawaangamiza watu wako, Yahwe; wanalitesa taifa ambao ni milki yako.
Ee Bwana, wanawaponda watu wako, wanawaonea urithi wako.
6 Wanamuua mjane na mgeni aishiye nchini mwao, na wanamuua yatima.
Wanamchinja mjane na mgeni, na kuwaua yatima.
7 Nao husema, “Yahwe hawezi kuona, Mungu wa Yakobo hayagundui haya.”
Nao husema, “Bwana haoni, Mungu wa Yakobo hafahamu.”
8 Tambueni, ninyi watu wajinga! Enyi wapumbavu, mtajifunza lini?
Sikizeni, enyi wajinga miongoni mwa watu; enyi wapumbavu, lini mtakuwa na hekima?
9 Yeye aliye liumba sikio, hasikii? Yeye aliye litengeneza jicho, haoni?
Je, aliyeweka sikio asisikie? Aliyeumba jicho asione?
10 Yeye awaadhibuye mataifa, hayuko sahihi? Yeye ndiye ampaye maarifa mwanadamu.
Je, anayeadhibisha mataifa asiadhibu? Je, awafundishaye wanadamu asiwe na maarifa?
11 Yahwe anayajua mawazo ya wanadamu, kuwa ni mvuke.
Bwana anajua mawazo ya mwanadamu; anajua kwamba ni ubatili.
12 Amebarikiwa yule ambaye umuongozaye, Yahwe, yule ambaye wewe humfundisha kutoka katika sheria yako.
Ee Bwana, heri mtu anayeadhibishwa na wewe, mtu unayemfundisha kwa sheria yako,
13 Wewe humpa pumziko wakati wa shida mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa kwa ajili ya waovu.
unampa utulivu siku za shida, mpaka shimo litakapokuwa limechimbwa kwa ajili ya mwovu.
14 Maana Yahwe hatawaacha watu wake wala kutelekeza warithi wake.
Kwa kuwa Bwana hatawakataa watu wake, hatauacha urithi wake.
15 Kwa kuwa tena hukumu itakuwa ya haki; na wote walio wanyoofu wa moyo wataifuata.
Hukumu itasimamishwa tena kwenye haki, wote walio na mioyo minyofu wataifuata.
16 Ni nani atainuka kunitetea dhidi ya watendao uovu? Ni nani atasimama dhidi ya waovu kwa ajili yangu?
Ni nani atakayeinuka dhidi ya mwovu kwa ajili yangu? Ni nani atakayenikinga dhidi ya watenda maovu?
17 Kama Yahwe asingelikuwa msaada wangu, haraka ningekuwa nimelala mahali pa ukimya.
Kama Bwana asingelinisaidia upesi, ningelikuwa ninaishi katika ukimya wa kifo.
18 Niliposema, mguu wangu unateleza,” Uaminifu wa agano lako, Yahwe, uliniinua.
Niliposema, “Mguu wangu unateleza,” Ee Bwana, upendo wako ulinishikilia.
19 Wasiwasi uwapo mwingi ndani yangu, faraja yako hunifurahisha.
Wakati wasiwasi ulipokuwa mwingi ndani yangu, faraja yako ilinipa furaha nafsini mwangu.
20 Kiti cha uharibifu chaweza kushirikiana nawe, kitungacho madhara kwa njia ya sheria?
Je, kiti cha utawala wa udhalimu kitajiunga nawe, ule utawala uletao taabu kutokana na sheria zake?
21 Wao kwa pamoja hupanga njama kuwaua wenye haki na kuwahukumu adhabu ya kifo wenye haki.
Huungana kuwashambulia wenye haki, kuwahukumu kufa wasio na hatia.
22 Lakini Yahwe amekuwa mnara wangu mrefu, na Mungu wangu amekuwa mwamba wa kimbilio langu.
Lakini Bwana amekuwa ngome yangu, na Mungu wangu amekuwa mwamba ninaoukimbilia.
23 Yeye atawarudishia uovu wao wenyewe na atawaangamiza katika uovu wao wenyewe. Yahwe Mungu wetu atawaangamiza.
Yeye atawalipa kwa ajili ya dhambi zao na atawaangamiza kwa ajili ya maovu yao; Bwana Mungu wetu atawaangamiza.

< Zaburi 94 >