< Zaburi 69 >

1 Uniokoe, Mungu; maana maji yameweka uhai wangu hatarini.
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Yungiyungi.” Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, niokoe, kwa maana maji yamenifika shingoni.
2 Ninazama kwenye kina cha matope, pasipo na hahari pa kusimama; nimekuja kwenye kina kirefu cha maji, ambako mafuriko yananifunika.
Ninazama kwenye vilindi vya matope, pasipo mahali pa kukanyaga, Nimefika kwenye maji makuu, mafuriko yamenigharikisha.
3 Nimechoka sana kwa kulia kwangu; koo langu ni kavu; macho yangu yanafifia wakati namngoja Mungu wangu.
Nimechoka kwa kuomba msaada, koo langu limekauka. Macho yangu yanafifia, nikimtafuta Mungu wangu.
4 Wale wanichukiao bila sababu wako zaidi ya nywele za kichwa changu; wale ambao wangeweza kuniua, wakiwa adui zangu kwa sababu zisizo sahihi, ni wengi mno; wanalazimisha nirudishe kile ambacho sijaiba.
Wale wanaonichukia bila sababu ni wengi kuliko nywele za kichwa changu; wengi ni adui kwangu bila sababu, wale wanaotafuta kuniangamiza. Ninalazimishwa kurudisha kitu ambacho sikuiba.
5 Mungu, wewe unaujua ujinga wangu, na dhambi zangu hazifichiki kwako.
Ee Mungu, wewe unajua upumbavu wangu, wala hatia yangu haikufichika kwako.
6 Usiwaache wale wanao kungoja wewe waaibishwe kwa sababu yangu, Bwana Yahwe wa majeshi; usiwaache wale wanaokutafuta wewe wadharauliwe kwa sababu yangu, Mungu wa Israeli.
Ee Bwana, ewe Bwana Mwenye Nguvu Zote, wakutumainio wasiaibishwe kwa ajili yangu; wakutafutao wasifedheheshwe kwa ajili yangu, Ee Mungu wa Israeli.
7 Kwa ajili yako nimestahimili lawama; aibu imeufunika uso wangu.
Kwa maana nimestahimili dharau kwa ajili yako, aibu imefunika uso wangu.
8 Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, nisiye fahamika wala kuaminika kwa watoto wa mama yangu.
Nimekuwa mgeni kwa ndugu zangu, mgeni kwa wana wa mama yangu mwenyewe.
9 Kwa maana bidii ya nyumba yako imenila, na laumu zao wanao kulaumu wewe zimeniangukia mimi.
Kwa kuwa wivu wa nyumba yako unanila, matukano ya wale wanaokutukana yameniangukia.
10 Wakati nilipolia na kutokula chakula, walinitukana.
Ninapolia na kufunga, lazima nivumilie matusi.
11 Nilipoteneneza mavazi ya gunia, nikawa kituko kwao.
Ninapovaa nguo ya gunia, watu hunidharau.
12 Wale wakaao katika lango la mji huniseng'enya; mimi ni wimbo wa walevi.
Wale wanaoketi mlangoni wananisimanga, nimekuwa wimbo wa walevi.
13 Lakini kwangu mimi, maombi yangu ni kwako, Yahwe, wakati ambao wewe utayapokea; unijibu katika uaminifu wa wokovu wako.
Lakini Ee Bwana, ninakuomba, kwa wakati ukupendezao; katika upendo wako mkuu, Ee Mungu, unijibu kwa wokovu wako wa hakika.
14 Unitoe matopeni, na usiniache nizame; uniondoe mbali na wale wanaonichukia na uniokoe katika kina cha maji.
Uniokoe katika matope, usiniache nizame; niokoe na hao wanichukiao, kutoka kwenye vilindi vya maji.
15 Usiache mafuliko ya maji yanielemee, wala kina kisinimeze. Usiache mdomo wa shimo unimeze.
Usiache mafuriko yanigharikishe au vilindi vinimeze, au shimo lifumbe kinywa chake juu yangu.
16 Unijibu, Yahwe, maana uaminifu wa agano lako ni mwema; kwa maana rehema zako kwangu ni nyingi, unigeukie.
Ee Bwana, unijibu, kwa wema wa upendo wako; kwa huruma zako nyingi unigeukie.
17 Usiufiche uso wako mbali na mtumishi wako, maana niko katika dhiki; unijibu haraka.
Usimfiche mtumishi wako uso wako, uharakishe kunijibu, kwa sababu niko katika shida.
18 Uje kwangu na unikomboe. Kwa sababu ya adui zangu, uwe fidia yangu.
Njoo karibu uniokoe, nikomboe kwa sababu ya adui zangu.
19 Wewe wajua kulaumiwa kwangu, kuaibishwa kwangu, na kudharauliwa kwangu; wapinzani wangu wote wako mbele yako.
Unajua jinsi ninavyodharauliwa, kufedheheshwa na kuaibishwa, adui zangu wote unawajua.
20 Lawama imevunja moyo wangu; nimejawa na huzuni kubwa; nilitafuta mtu wa kunihurumia, lakini hakuwepo; nilitafuta wafariji, lakini sikupata.
Dharau zimenivunja moyo na nimekata tamaa, nimetafuta wa kunihurumia, lakini sikumpata, wa kunituliza, lakini sikumpata.
21 Walinipa sumu kwa ajili ya chakula changu; katika kiu yangu walinipa siki ninywe.
Waliweka nyongo katika chakula changu na walinipa siki nilipokuwa na kiu.
22 Meza yao mbele yao na iwe mtego; wafikiripo wako kwenye usalama, iwe kitanzi.
Meza iliyoandaliwa mbele yao na iwe mtego, nayo iwe upatilizo na tanzi.
23 Macho yao na yatiwe giza ili kwamba wasiweze kuona; uvifanye viuno vyao kutetemeka daima.
Macho yao yatiwe giza ili wasiweze kuona, nayo migongo yao iinamishwe daima.
24 Wamwagie gadhabu yako, ukali wa hasira yako uwafikie wao.
Uwamwagie ghadhabu yako, hasira yako kali na iwapate.
25 Sehemu yao na iwe ukiwa; mtu yeyote asiishi katika hema yao.
Mahali pao na pawe ukiwa, wala asiwepo yeyote atakayeishi katika mahema yao.
26 Kwa kuwa walimtesa yule uliyempa adhabu. Mara kwa mara walihesabu maumivu ya wale walioumizwa.
Kwa kuwa wanawatesa wale uliowajeruhi, na kuzungumza juu ya maumivu ya wale uliowaumiza.
27 Wakiwashtaki kuwa wamefanya uovu juu ya uovu; usiwaache waje kwenye ushindi wa haki yako.
Walipize uovu juu ya uovu, usiwaache washiriki katika wokovu wako.
28 Uwafute kwenye Kitabu cha Uzima na wasiandikwe pamoja na wenyehaki.
Wafutwe kutoka kitabu cha uzima na wasiorodheshwe pamoja na wenye haki.
29 Lakini mimi ni maskini na mwenye huzuni; uruhusu wokovu wako, Mungu, uniweke juu sana.
Mimi niko katika maumivu na dhiki; Ee Mungu, wokovu wako na unihifadhi.
30 Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo na nitamtukuza yeye kwa shukrani.
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo, nami nitamtukuza kwa kumtolea shukrani.
31 Nitamsifu Yahwe zaidi kuliko ng'ombe au ndama aliye na mapembe na kwato.
Hili litampendeza Bwana kuliko ngʼombe dume, zaidi ya fahali akiwa na pembe na kwato zake.
32 Wanyenyekevu wameona na kufurahi; ninyi mnao matafuta Mungu, mioyo yenu itiwe nguvu.
Maskini wataona na kufurahi: ninyi mnaomtafuta Mungu, mioyo yenu na iishi!
33 Maana Yahwe husikia wenye uhitaji naye hawadharau wafungwa wake.
Bwana huwasikia wahitaji wala hadharau watu wake waliotekwa.
34 Mbingu na nchi zimsifu yeye, bahari na vyote vitembeavyo majini.
Mbingu na dunia zimsifu, bahari na vyote viendavyo ndani yake,
35 Kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni na ataujenga tena mji wa Yuda; watu wataishi huko na kupata umiliki wao.
kwa maana Mungu ataiokoa Sayuni na kuijenga tena miji ya Yuda. Kisha watu watafanya makao yao humo na kuimiliki,
36 Ukoo wa watumishi wake watairithi; nao walipendao jina lake wataishi humo.
watoto wa watumishi wake watairithi na wale wote walipendao jina lake wataishi humo.

< Zaburi 69 >