< Zaburi 66 >

1 Mpigieni Mungu kelele za shangwe, nchi yote;
Kwa mwimbishaji. Wimbo. Zaburi. Mpigieni Mungu kelele za shangwe, dunia yote!
2 Imbeni utukufu wa jina lake; mzitukuze sifa zake.
Imbeni utukufu wa jina lake; mpeni sifa zake kwa utukufu!
3 Mwambieni Mugu, “Matendo yako yanatisha kama nini! Kwa ukuu wa nguvu zako maadui zako watajisalimisha kwako.
Mwambieni Mungu, “Jinsi gani yalivyo ya kutisha matendo yako! Uwezo wako ni mkuu mno kiasi kwamba adui wananyenyekea mbele zako.
4 Nchi yote watakuabudu wewe na watakuimbia wewe; wataliimbia jina lako.” (Selah)
Dunia yote yakusujudia, wanakuimbia wewe sifa, wanaliimbia sifa jina lako.”
5 Njoni na mtazame kazi za Mungu; yeye anatisha katika matendo yake awatendeayo wanadamu.
Njooni mwone yale Mungu aliyoyatenda, mambo ya kutisha aliyoyatenda miongoni mwa wanadamu!
6 Aligeuza bahari kuwa nchi kavu; wao walitembea kwa mguu juu ya mto; huko tulishangilia katika yeye.
Alifanya bahari kuwa nchi kavu, wakapita kati ya maji kwa miguu, njooni, tumshangilie.
7 Yeye anatawala milele kwa nguvu zake; macho yake yanachunguza mataifa; waasi wasijivune. (Selah)
Yeye hutawala kwa uwezo wake milele, macho yake huangalia mataifa yote: waasi wasithubutu kujiinua dhidi yake.
8 Mtukuzeni Mungu, enyi watu wa mataifa yote, sauti ya sifa zake isikike.
Enyi mataifa, msifuni Mungu wetu, sauti ya sifa yake isikike,
9 Yeye atuwekaye hai, naye hairuhusu miguu yetu iteleze.
ameyahifadhi maisha yetu na kuizuia miguu yetu kuteleza.
10 Kwa maana wewe, Mungu, umetupima sisi, wewe umetupima kama inavyopimwa fedha.
Ee Mungu, wewe ulitujaribu, ukatusafisha kama fedha.
11 Wewe ulituingiza sisi kwenye wavu; uliweka mzigo mzito viunoni mwetu.
Umetuingiza kwenye nyavu na umetubebesha mizigo mizito migongoni mwetu.
12 Wewe uliwafanya watu wasafiri juu ya vichwa vyetu; tulipita motoni na majini, lakini ukatuleta mahali pa wazi palipo salama.
Uliwaruhusu watu watukalie vichwani, tulipita kwenye moto na kwenye maji, lakini ulituleta kwenye nchi iliyojaa utajiri tele.
13 Nitaingia nyumbani mwako nikiwa na sadaka ya kuteketezwa; nitakulipa viapo vyangu
Nitakuja hekaluni mwako na sadaka za kuteketezwa na kukutimizia nadhiri zangu:
14 ambavyo midomo yangu iliahidi na kinywa changu kiliongea nilipokuwa katika dhiki.
nadhiri ambazo midomo yangu iliahidi na nilizotamka kwa kinywa changu nilipokuwa katika shida.
15 Nitakutolea sadaka ya kuteketezwa ya wanyama wanene pamoja na harufu nzuri ya kondoo waume; Nitatoa ng'ombe na mbuzi. (Selah)
Nitakutolea dhabihu za wanyama wanono na sadaka za kondoo dume, nitakutolea mafahali na mbuzi.
16 Njoni, msikie, ninyi nyote mnao mwabudu Mungu, nami nitatangaza yale yeye aliyoitendea roho yangu.
Njooni msikilize ninyi nyote mnaomcha Mungu, nami niwaambie aliyonitendea.
17 Nilimlilia kwa kinywa changu, naye alipendezwa na ulimi wangu.
Nilimlilia kwa kinywa changu, sifa zake zilikuwa katika ulimi wangu.
18 Kama ningelikuwa na dhambi ndani ya moyo wangu, Bwana asingenisikiliza.
Kama ningekuwa nimeyaficha maovu moyoni mwangu, Bwana asingekuwa amenisikiliza;
19 Lakini Mungu hakika amesikia; amesikia sautiya kuomba kwangu.
lakini hakika Mungu amenisikiliza na amesikia sauti yangu katika maombi.
20 Atukuzwe Mungu, ambaye hakuyakataa maombi yangu wala kuweka uaminifu wa agano lake mbali nami.
Sifa apewe Mungu, ambaye hakulikataa ombi langu wala kunizuilia upendo wake!

< Zaburi 66 >