< Zaburi 58 >

1 Je, ninyi watawala mnaongea haki? Mnahukumu kwa haki, ninyi watu?
Kwa mwimbishaji. Mtindo wa “Usiharibu!” Utenzi wa Daudi. Enyi watawala, je, kweli mwanena kwa haki? Je, mnahukumu kwa unyofu miongoni mwa watu?
2 Hapana, mnafanya uovu mioyoni mwenu; munaeneza vurugu nchi yote kwa mikono yenu.
La, mioyoni mwenu mnatunga udhalimu, na mikono yenu hupima jeuri duniani.
3 Waovu huenenda katika upotovu hata walipokuwa tumboni; wao wanaenenda katika upotovu tangu kuzaliwa, wakiongea uongo.
Waovu ni wapotovu tangu kuzaliwa kwao, toka tumboni mwa mama zao ni wakaidi na husema uongo.
4 Sumu yao ni kama sumu ya nyoka; wako kama fira kiziwi azibaye masikio yake,
Sumu yao ni kama sumu ya nyoka, kama ile ya fira ambaye ameziba masikio yake,
5 ambaye hasikilizi sauti ya waganga, haijalishi ustadi walio nao.
ambaye hatasikia sauti ya kutumbuiza ya mwaguzi, hata kama mganga angecheza kwa ustadi kiasi gani.
6 Vunja meno yao midomoni mwao, Mungu; uyatoe meno ya mwana simba, Yahwe.
Ee Mungu, yavunje meno katika vinywa vyao; Ee Bwana, vunja meno makali ya hao simba!
7 Wayeyuke kama maporomoko ya maji; wafyatuapo mishale yao, iwe kama haina ncha.
Na watoweke kama maji yapitayo kwa kasi, wavutapo pinde zao, mishale yao na iwe butu.
8 Wawe kama konokono ambaye huyeyuka na kutoweka, kama mtoto aliye zaliwa kabla ya wakati ambaye hakuona jua.
Kama konokono ayeyukavyo akitembea, kama mtoto aliyezaliwa akiwa mfu, wasilione jua.
9 Kabla ya vyungu vyenu kupata joto la kuungua kwa miiba, yeye ataviondosha kwa upepo mkali, miiba ya kijani yote na ile inayoungua.
Kabla vyungu vyenu havijapata moto wa kuni za miiba, zikiwa mbichi au kavu, waovu watakuwa wamefagiliwa mbali.
10 Mwenye haki atafurahia atakapoona kisasi cha Mungu; ataiosha miguu yake kwenye damu ya waovu,
Wenye haki watafurahi waonapo wakilipizwa kisasi, watakapochovya nyayo zao katika damu ya waovu.
11 hivyo watu watasema, “Hakika kuna tuzo kwa ajili ya mtu wenye haki; hakika kuna Mungu ahukumuye ulimwengu.”
Ndipo wanadamu watasema, “Hakika utulivu wa wenye haki bado una thawabu, hakika kuna Mungu ahukumuye dunia.”

< Zaburi 58 >