< Zaburi 5 >

1 Sikiliza nikuitapo, Yahweh; tazama kuugua kwangu.
Kwa mwimbishaji. Kwa filimbi. Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, tegea sikio maneno yangu, uangalie kupiga kite kwangu.
2 Sikiliza sauti yangu nikuitapo, Ee Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa kuwa ni kwako Bwana naomba.
Sikiliza kilio changu ili unisaidie, Mfalme wangu na Mungu wangu, kwa maana kwako ninaomba.
3 Yahweh; sikia kilio changu asubuhi; na asubuhi nitaleta dua yangu kwako na kungoja kwa matarajio.
Asubuhi, unasikia sauti yangu, Ee Bwana; asubuhi naleta haja zangu mbele zako, na kusubiri kwa matumaini.
4 Hakika wewe ni Mungu usiye kubaliana na uovu; watu waovu hawawezi kuwa wageni wako.
Wewe si Mungu unayefurahia uovu, kwako mtu mwovu hataishi.
5 Wenye kiburi hawata simama katika uwepo wako; wewe unawachukia wote wanaofanya maovu.
Wenye kiburi hawawezi kusimama mbele yako, unawachukia wote watendao mabaya.
6 Nawe utawaharibu waongo; Yahweh huwadharau vurugu na watu wadanganyifu.
Unawaangamiza wasemao uongo. Bwana huwachukia wamwagao damu na wadanganyifu.
7 Lakini kwangu mimi, kwa sababu ya ukuu na uaminifu wa agano lako, nitakuja nyumbani mwako; na kwa heshima nitakuinamia mbele ya hekalu lako takatifu.
Lakini mimi, kwa rehema zako kuu, nitakuja katika nyumba yako, kwa unyenyekevu, nitasujudu kuelekea Hekalu lako takatifu.
8 Oh Bwana, uniongoze katika haki yako kwa sababu ya adui zangu; usawazishe njia yako mbele yangu.
Niongoze katika haki yako, Ee Bwana, kwa sababu ya adui zangu, nyoosha njia yako mbele yangu.
9 Kwa kuwa midomoni mwao hamna ukweli; utu wao wa ndani ni mwovu; makoo yao ni kaburi lililo wazi; husifu kinafiki kwa ulimi wao.
Hakuna neno kinywani mwao linaloweza kuaminika, mioyo yao imejaa maangamizi. Koo lao ni kaburi lililo wazi, kwa ndimi zao, wao hunena udanganyifu.
10 Mungu, wafanye kuwa na hatia; mipango yao iwe kuanguka kwao! Kwa ajili ya makosa yao mengi uwatoe nje, kwa kuwa wamekuasi wewe.
Uwatangaze kuwa wenye hatia, Ee Mungu! Hila zao ziwe anguko lao wenyewe. Wafukuzie mbali kwa sababu ya dhambi zao nyingi, kwa kuwa wamekuasi wewe.
11 Bali wale wanao kukimbilia wafurahi; uwafanye wapige kelele kwa shangwe siku zote kwa sababu unawapigania; uwafanye wenye furaha ndani yako, wale walipendao jina lako.
Lakini wote wakimbiliao kwako na wafurahi, waimbe kwa shangwe daima. Ueneze ulinzi wako juu yao, ili wale wapendao jina lako wapate kukushangilia.
12 Kwa maana utawabariki wenye haki, Yahweh; utawazunguka kwa neema kama ngao.
Kwa hakika, Ee Bwana, unawabariki wenye haki, unawazunguka kwa wema wako kama ngao.

< Zaburi 5 >