< Zaburi 48 >
1 Yahwe ndiye aliye mkuu na mwenyekusifiwa sana, katika mji wa Mungu wetu kwenye mlima wake mtakatifu.
Wimbo. Zaburi ya wana wa Kora. Bwana ni mkuu, anayestahili kusifiwa sana, katika mji wa Mungu wetu, mlima wake mtakatifu.
2 Ni mzuri katika mwinuko wake, furaha ya nchi yote, ni mlima Sayuni, kwenye upande wa kaskazini, mji wa Mfalme mkuu.
Ni mzuri katika kuinuka kwake juu sana, furaha ya dunia yote. Kama vilele vya juu sana vya Safoni ni Mlima Sayuni, mji wa Mfalme Mkuu.
3 Mungu amejifunua mwenyewe katika jumba lake la kifahari kama kimbilio la usalama.
Mungu yuko katika ngome zake; amejionyesha mwenyewe kuwa ngome yake.
4 Maana, tazama, wafalme walikusanyika wenyewe; wote pamoja walipita.
Wakati wafalme walipounganisha nguvu, waliposonga mbele pamoja,
5 Nao waliuona, wakashangaa; walifadhaika, na wakaharakisha kuondoka.
walimwona nao wakashangaa, wakakimbia kwa hofu.
6 Pale pale tetemeko liliwashikilia, maumivu makali kama mwanamke anaye zaa.
Kutetemeka kuliwashika huko, maumivu kama ya mwanamke mwenye utungu wa kuzaa.
7 Kwa upepo wa mashariki wewe huivunja meli ya Tarshishi.
Uliwaangamiza kama meli za Tarshishi zilizovunjwa na upepo wa mashariki.
8 Kama tulivyo sikia, vivyo hivyo tumeona katika mji wa Yahwe wa majeshi, katika mji wa Mungu wetu; Mungu atautunza milele. (Selah)
Kama tulivyokuwa tumesikia, ndivyo tulivyoona katika mji wa Bwana Mwenye Nguvu Zote, katika mji wa Mungu wetu: Mungu ataufanya uwe salama milele.
9 Tumeutafakari uaminifu wa agano lako, Mungu, katikati ya hekalu lako.
Ee Mungu, hekaluni mwako tunatafakari upendo wako usiokoma.
10 Kama lilivyo jina lako, Mungu, hivyo ndivyo zilivyo sifa zako mpaka miisho ya dunia; mkono wako wa kuume umejaa haki.
Ee Mungu, kama jina lako lilivyo, sifa zako zinafika hadi miisho ya dunia, mkono wako wa kuume umejazwa na haki.
11 Milma Sayuni na ufurahi, nao wana wa Yuda washangilie kwa sababu ya amri ya haki yako.
Mlima Sayuni unashangilia, vijiji vya Yuda vinafurahi kwa sababu ya hukumu zako.
12 Tembeeni katika Mlima Sayuni, muuzungukie mji,
Tembeeni katika Sayuni, uzungukeni mji, hesabuni minara yake;
13 mzitazame kwa makini nguzo zake, na mtazame majumba yake ya kifahari ili kwamba muweze kuwasimulia kizazi kijacho.
yatafakarini vyema maboma yake, angalieni ngome zake, ili mpate kusimulia habari zake kwa kizazi kijacho.
14 Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele; naye atakuwa kiongozi wetu mpaka kufa.
Kwa kuwa huyu Mungu ni Mungu wetu milele na milele; atakuwa kiongozi wetu hata mwisho.