< Zaburi 35 >
1 Yahwe, uwashughulikie wale wanao nishughulikia mimi; upigane nao wanao pigana nami.
Zaburi ya Daudi. Ee Bwana, pingana na wale wanaopingana nami, upigane na hao wanaopigana nami.
2 Uikamate ngao yako ndogo na ngao kubwa; inuka unisaidie.
Chukua ngao na kigao. Inuka unisaidie.
3 Uutumie mkuki wako na shoka lako la vita kwa wale wanao nifukuzia; uuambie moyo wangu, “Mimi ni wokovu wako.”
Inua mkuki wako na fumo lako dhidi ya hao wanaonifuatia. Iambie nafsi yangu, “Mimi ni wokovu wako.”
4 Waaibishwe na kudharauliwa wale wanaoutafuta uhai wangu. Warudishwe nyuma na wafedheheshwe wanao panga kunidhuru.
Wafedheheshwe na waaibishwe wale wanaotafuta uhai wangu. Wanaofanya shauri kuniangamiza warudishwe nyuma kwa hofu.
5 Wao wawe makapi mbele ya upepo, malaika wakiwafutilia mbali.
Wawe kama makapi yapeperushwayo na upepo, malaika wa Bwana akiwafukuza.
6 Njia yao na iwe giza na utelezi, malaika wa Yahwe wakiwafukuzia.
Njia yao na iwe giza na ya utelezi, malaika wa Bwana akiwafuatilia.
7 Wamenitegea mtego bila sababu; bila sababu wamechimba shimo kwa ajili ya uhai wangu.
Kwa vile walinifichia wavu wao bila sababu, na bila sababu wamenichimbia shimo,
8 Uharibifu na uwapate wao kwa kushitukiza. Mtego ambao wameutega na uwanase wao. Na wadumbukie humo, ili kwamba waangamizwe.
maafa na yawapate ghafula: wavu walionifichia na uwatege wenyewe, na waanguke katika shimo hilo, kwa maangamizo yao.
9 Bali mimi nitakuwa nafuraha ndani ya Yahwe na ndani ya wokovu wake.
Ndipo nafsi yangu itashangilia katika Bwana na kuufurahia wokovu wake.
10 Mifupa yangu yote itasema, “Yahwe, ni nani kama wewe, uokoaye walio onewa mkononi mwa walio na nguvu kuwazidi wao na masikini na wahitaji mkononi mwa wale wanaojaribu kuwaibia?”
Nitapaza sauti yangu nikisema, “Ni nani aliye kama wewe, Ee Bwana? Wewe huwaokoa maskini kutokana na wale walio na nguvu kuliko wao, maskini na mhitaji kutokana na wanaowanyangʼanya!”
11 Mashahidi wa uongo wamesimama; wananishitakia uongo.
Mashahidi wakatili wanainuka, wananiuliza mambo nisiyoyajua.
12 Kwa ajili ya wema wananilipa mabaya. Nina huzuni nyingi.
Wananilipa baya kwa jema na kuiacha nafsi yangu ukiwa.
13 Lakini, walipokuwa akiugua, nilivaa magunia; nilifunga kwa ajili yao huku kichwa changu kikiinamia kifuani kwangu.
Lakini walipokuwa wagonjwa, nilivaa nguo ya gunia na nikajinyenyekesha kwa kufunga. Maombi yangu yaliponirudia bila kujibiwa,
14 Nilienenda katika huzuni kana kwamba walikuwa ni ndugu zangu; niliinama chini nikiomboleza kana kwamba ni kwa ajili ya mama yangu.
niliendelea kuomboleza kama vile wao ni rafiki au ndugu. Niliinamisha kichwa chini kwa huzuni kama ninayemwombolezea mama yangu.
15 Bali mimi nilipokuwa mashakani, walifurahi sana na kukutanika pamoja; walikutanika pamoja kinyume na mimi, nami nilishangazwa nao. Walinirarua bila kuacha.
Lakini nilipojikwaa, walikusanyika kwa shangwe; washambuliaji walijikusanya dhidi yangu bila mimi kujua. Walinisingizia pasipo kukoma.
16 Kwa dharau kabisa walinidhihaki; walinisagia meno yao.
Kama watu wasiomcha Mungu, wamenidhihaki, wamenisagia meno.
17 Bwana, mpaka lini utaendelea kutazama? uiokoe roho yangu na mashambulizi yao ya maagamizi uyaokoe maisha yangu na simba.
Ee Bwana, utatazama mpaka lini? Niokoe maisha yangu na maangamizi yao, uhai wangu wa thamani kutokana na simba hawa.
18 Nami nitakushukuru wewe katika kusanyiko kubwa; nitakusifu kati ya watu wengi.
Nami nitakushukuru mbele ya kusanyiko kubwa, nitakusifu katikati ya watu wengi.
19 Usiwaache maadui zangu wadanganyifu kufurahi juu yangu; usiwaache waendelee na mipango yao ya uovu.
Usiwaache wale wanaonisimanga, wale ambao ni adui zangu bila sababu; usiwaache wale ambao ni adui zangu bila sababu wakonyeze jicho kwa hila.
20 Kwa maana hawaongei amani, bali wanabuni maneno ya uongo kwa wale wanaoishi kwa amani katika ardhi yetu.
Hawazungumzi kwa amani, bali wanatunga mashtaka ya uongo dhidi ya wale wanaoishi kwa utulivu katika nchi.
21 Midomo yao inapaza sauti ikinishtaki; wakisema, Aha, Aha, macho yetu yameona.”
Hunifumbulia vinywa vyao wakisema, “Aha! Aha! Kwa macho yetu wenyewe tumeliona.”
22 Yahwe wewe umeona, usikae kimya; Bwana, usiwe mbali nami.
Ee Bwana, umeona hili, usiwe kimya. Usiwe mbali nami, Ee Bwana.
23 Inuka mwenyewe na usimame kunitetea; Mungu wangu na Bwana wangu, unitetee.
Amka, inuka unitetee! Unipiganie Mungu wangu na Bwana wangu.
24 Kwa sabababu ya haki yako, Yahwe Mungu wangu, unitetee; usiwaache wafurahi kwa ajili yangu.
Nihukumu kwa haki yako, Ee Bwana Mungu wangu, sawasawa na haki yako; usiwaache wakusimange.
25 Usiwaache waseme mioyoni mwao, “Aha, tumepata tulicho kihitaji.” Usiwaache waseme, tumemmeza.”
Usiwaache wafikiri, “Aha, hili ndilo tulilotaka!” Au waseme, “Tumemmeza.”
26 Uwaaibishe na kuwa fendhehesha wale wanaotaka kunidhuru. Wale wote wanao ni dhihaki wafunikwe kwa aibu na kudharauliwa.
Wote wanaofurahia dhiki yangu waaibishwe na wachanganyikiwe; hao wanaojiinua dhidi yangu wavikwe aibu na dharau.
27 Nao wote wanao tamani kudhihirishwa kwangu washangilie na wafurahi; siku zote waseme, “Usifiwe Yahwe, yeye ajifurahishaye katika mafanikio ya mtumishi wake.
Wale wanaofurahia hukumu yangu ya haki wapige kelele za shangwe na furaha; hebu waseme siku zote, “Bwana atukuzwe, ambaye amefurahia mafanikio ya mtumishi wake.”
28 Kisha nitatangaza matendo yako ya haki na kukusifu wewe wakati wote.
Ulimi wangu utanena haki yako na sifa zako mchana kutwa.