< Zaburi 19 >

1 Kwa kiongozi wa muziki. Zaburi ya Daudi. Mbingu za tangaza utukufu wa Mungu, na mawingu hufanya kazi ya mikono yake ijulikane!
Kwa mwimbishaji. Zaburi ya Daudi. Mbingu zinatangaza utukufu wa Mungu, anga zahubiri kazi ya mikono yake.
2 Siku hadi siku hotuba hutokea; usiku hadi usiku hufunua maarifa.
Siku baada ya siku zinatoa habari, usiku baada ya usiku zinatangaza maarifa.
3 Hakuna hotuba wala misemo; sauti zao hazisikiki.
Hakuna msemo wala lugha, ambapo sauti zao hazisikiki.
4 Bali maneno yao husambaa nje duniani kote, na hotuba zao hata mwisho wa dunia. Yeye ametengeneza hema kwa ajili ya jua kati yao.
Sauti yao imeenea duniani pote, nayo maneno yao yameenea hadi miisho ya ulimwengu. Katika mbingu amepiga hema kwa ajili ya jua,
5 Jua liko kama mfano wa bwana harusi akitokea chumbani kwake na kama mtu shujaa ambaye hushangila pale anapokimbia mbio zake.
linafanana na bwana arusi akitoka chumbani mwake, kama shujaa afurahiavyo kukamilisha kushindana kwake.
6 Jua huchomoza kutokea upeo wa macho na likikatisha winguni kwenda jingine; hakuna chochote kinacho epuka joto lake.
Huchomoza upande mmoja wa mbingu, na kufanya mzunguko wake hadi upande mwingine. Hakuna kilichojificha joto lake.
7 Sheria ya Yahwe ni kamilifu, huokoa roho; ushuhuda wa Yahwe ni wa kuaminika, ukifanya hekima nyepesi.
Sheria ya Bwana ni kamilifu, ikihuisha nafsi. Shuhuda za Bwana ni za kuaminika, zikimpa mjinga hekima.
8 Maelekezo ya Yahwe ni ya hakika, yakiufanya moyo kuwa na furaha; amri ya Yahwe ni safi, ikileta mwanga kwenye macho yetu.
Maagizo ya Bwana ni kamili, nayo hufurahisha moyo. Amri za Bwana huangaza, zatia nuru machoni.
9 Hofu ya Yahwe ni safi, inadumu milele; amri za haki ya Yahwe ni za kweli na zote ni za hakika!
Kumcha Bwana ni utakatifu, nako kwadumu milele. Amri za Bwana ni za hakika, nazo zina haki.
10 Nazo zina thamani kuliko dhahabu, nazo ni tamu kuliko asali na matone ya asali kutoka sega la asali (sega la nyuki).
Ni za thamani kuliko dhahabu, kuliko dhahabu iliyo safi sana, ni tamu kuliko asali, kuliko asali kutoka kwenye sega.
11 Ndiyo, kupitia hizo mtumishi wako anaonywa; na katika kuziamini kuna thawabu.
Kwa hizo mtumishi wako anaonywa, katika kuzishika kuna thawabu kubwa.
12 Ni nani ambaye aweza kuyatambua makosa yake yote mwenyewe? Unitakase makosa yaliyo fichika.
Ni nani awezaye kutambua makosa yake? Nisamehe makosa yangu nisiyoyajua.
13 Pia umuepushe mtumishi wako na dhambi za majivuno; usiziruhusu kunitawala. Ndipo nitakuwa mkamilifu, na mimi sitakuwa na hatia ya makosa mengi.
Mlinde mtumishi wako na dhambi za makusudi, nazo zisinitawale. Ndipo nitakapokuwa sina lawama, wala sitakuwa na hatia ya kosa kubwa.
14 Maneno ya midomo yangu na mawazo ya moyo wangu nayakubalike machoni pako, ewe Yahwe, mwamba wangu na mkombozi wangu.
Maneno ya kinywa changu na mawazo ya moyo wangu, yapate kibali mbele zako, Ee Bwana, Mwamba wangu na Mkombozi wangu.

< Zaburi 19 >