< Zaburi 111 >

1 Msifuni Yahwe. Nitamshukuru Yahwe kwa moyo wangu wote katikati ya kusanyiko la wanye haki, na katika mkutano.
Msifuni Bwana. Nitamtukuza Bwana kwa moyo wangu wote, katika baraza la wanyofu na katika kusanyiko.
2 Kazi za Yahwe ni kuu, zikisubiriwa na wale wazitamanio.
Kazi za Bwana ni kuu, wote wanaopendezwa nazo huzitafakari.
3 Kazi yake ni adhama na utukufu, na haki yake yadumu milele.
Kazi zake zimejaa fahari na utukufu, haki yake hudumu daima.
4 Hufanya mambo makuu ambayo yatakumbukwa; Yahwe ni mwenye huruma na neema.
Amefanya maajabu yake yakumbukwe, Bwana ni mwenye neema na huruma.
5 Huwapa chakula wafuasi wake waaminifu. Siku zote atalikumbuka agano lake.
Huwapa chakula wale wanaomcha, hulikumbuka agano lake milele.
6 Alionesha uweza wa kazi zake kwa watu wake kwa kuwapa urithi wa mataifa.
Amewaonyesha watu wake uwezo wa kazi zake, akiwapa nchi za mataifa mengine.
7 Kazi za mikono yake ni za kuaminika na haki; maagizo yake yote ni ya kuaminika.
Kazi za mikono yake ni za uaminifu na haki, mausia yake yote ni ya kuaminika.
8 Yamethibitika milele, yamefanywa katika uaminifu na vizuri.
Zinadumu milele na milele, zikifanyika kwa uaminifu na unyofu.
9 Aliwapa ushindi watu wake; aliliteuwa agano lake milele; jina lake ni takatifu na lakutisha.
Aliwapa watu wake ukombozi, aliamuru agano lake milele: jina lake ni takatifu na la kuogopwa.
10 Kumcha Yahwe ni mwanzo wa hekima; wale washikao maagizo yake wana uelewa mzuri. Sifa yake yadumu milele.
Kumcha Bwana ndicho chanzo cha hekima, wote wanaozifuata amri zake wana busara. Sifa zake zadumu milele.

< Zaburi 111 >