< Zaburi 108 >

1 Ee Mungu, moyo wangu u thabiti; nitaimba, naam, nitaimba sifa pia kwa moyo mkuu.
Wimbo. Zaburi ya Daudi. Ee Mungu, moyo wangu ni thabiti; nitaimba na kusifu kwa moyo wangu wote.
2 Amka, kinanda na kinubi; nitaamka alfajiri.
Amka, kinubi na zeze! Nitayaamsha mapambazuko.
3 Nitakushukuru wewe, Yahwe, kati ya watu; nitakuimbia sifa kati ya mataifa.
Nitakusifu wewe, Ee Bwana, katikati ya mataifa; nitaimba habari zako, katikati ya jamaa za watu.
4 Kwa maana uaminifu wa agano lako ni mkuu juu ya mbingu; na uaminifu wako wafika mawinguni.
Kwa maana upendo wako ni mkuu, ni juu kuliko mbingu; uaminifu wako unazifikia anga.
5 Ee Mungu, uinuliwe, juu ya mbingu, na utukufu wako utukuke juu ya nchi.
Ee Mungu, utukuzwe juu ya mbingu, utukufu wako na uenee duniani kote.
6 Ili kwamba wale uwapendao waokolewe, utuokoe sisi kwa mkono wako wa kuume na unijibu.
Tuokoe na utusaidie kwa mkono wako wa kuume, ili wale uwapendao wapate kuokolewa.
7 Mungu ameongea katika utakatifu wake; “Nitashangilia; nitaigawanya Shekemu na nitalipima bonde la Sukothi.
Mungu amenena kutoka patakatifu pake: “Nitaigawa Shekemu kwa ushindi na kulipima Bonde la Sukothi.
8 Gileadi ni yangu, na manase ni yangu; Ephraimu ni nguvu ya kichwa changu; Yuda ni fimbo yangu ya kifalme.
Gileadi ni yangu, Manase ni yangu, Efraimu ni kofia yangu ya chuma, nayo Yuda ni fimbo yangu ya utawala.
9 Moabu ni bakuli langu la kunawia; nitatupa kiatu changu juu ya Edomu; nitapaza sauti katika ushindi kwa ajili ya Filisti.
Moabu ni sinia langu la kunawia, juu ya Edomu natupa kiatu changu; nashangilia kwa kushindwa kwa Ufilisti.”
10 Ni nani atakaye nipeleka kwenye mji imara? Ni nani atakayeniongoza mpaka Edomu?”
Ni nani atakayenipeleka hadi mji wenye ngome? Ni nani atakayeniongoza hadi nifike Edomu?
11 Ee Mungu, sio wewe uliyetukataa? Hauendi vitani na jeshi letu.
Ee Mungu, si ni wewe uliyetukataa sisi, na hutoki tena na majeshi yetu?
12 Utupe msaada dhidi ya adui yetu, maana msaada wa wanadamu ni bure.
Tuletee msaada dhidi ya adui, kwa maana msaada wa mwanadamu haufai kitu.
13 Tutashinda kwa msaada wa Mungu; atawakanyaga kwa adui zetu.
Kwa msaada wa Mungu tutapata ushindi, naye atawaponda adui zetu.

< Zaburi 108 >