< Zaburi 105 >

1 Mshukuruni Yahwe, liitieni jina lake; myafanye matendo yake yajulikane kati ya mataifa.
Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake, wajulisheni mataifa yale aliyoyatenda.
2 Mwimbieni yeye, mwimbieni sifa yeye; semeni matendo yake yote ya ajau.
Mwimbieni yeye, mwimbieni yeye sifa, waambieni matendo yake yote ya ajabu.
3 Mjivune katika utakatifu wa jina lake; moyo wao wamtafutao Yahwe ufurahi.
Lishangilieni jina lake takatifu, mioyo ya wale wamtafutao Bwana na ifurahi.
4 Mtafuteni Yahwe na nguvu zake; utafuteni uwepo wake siku zote.
Mtafuteni Bwana na nguvu zake, utafuteni uso wake siku zote.
5 Kumbukeni mambo ya ajabu aliyoyatenda,
Kumbuka matendo ya ajabu aliyoyafanya, miujiza yake na hukumu alizozitamka,
6 miujiza yake na amri zitokazo kinywani mwake, enyi kizazi cha Ibrahimu mtumishi wake, enyi watu wa Yakobo, wachaguliwa wake.
enyi wazao wa Abrahamu mtumishi wake, enyi wana wa Yakobo, wateule wake.
7 Yeye ni Yahwe, Mungu wetu. Amri zake ziko juu ya nchi yote.
Yeye ndiye Bwana Mungu wetu, hukumu zake zimo duniani pote.
8 Naye hulikumbuka agano lake milele, neno alilo amuru kwa ajili ya vizazi elfu.
Hulikumbuka agano lake milele, neno ambalo aliamuru, kwa vizazi elfu,
9 Hulikumbuka agano alilolifanya na Ibrahimu na kiapo alicho mwapia Isaka.
agano alilolifanya na Abrahamu, kiapo alichomwapia Isaki.
10 Hiki ndicho alicho mthibitishia Yakobo kama agano na kama agano la milele kwa Israeli.
Alilithibitisha kwa Yakobo kuwa amri, kwa Israeli liwe agano la milele:
11 Alisema, “Nitakupa wewe ardhi ya Kanaani kama sehemu yako ya urithi.”
“Nitakupa wewe nchi ya Kanaani kuwa sehemu utakayoirithi.”
12 Alisema hili wakati tu walipokuwa wachache katika hesabu, yaani wachahe sana, nao walikuwa wageni katika nchi.
Walipokuwa wachache kwa idadi, wachache sana na wageni ndani yake,
13 Walienda taifa hadi taifa na kutoka ufalme moja kwenda mwingine.
walitangatanga kutoka taifa moja hadi jingine, kutoka ufalme mmoja hadi mwingine.
14 Hakuruhusu yeyote kuwaonea; aliwakemea wafalme kwa ajili yao.
Hakuruhusu mtu yeyote awaonee; kwa ajili yao aliwakemea wafalme, akisema:
15 Alisema, “Msiwaguze wapakwa mafuta wangu, na msiwadhuru manabii wangu.”
“Msiwaguse niliowatia mafuta; msiwadhuru manabii wangu.”
16 Aliita njaa katika nchi; akaondoa upatikanaji wa mkate wote.
Akaiita njaa juu ya nchi na kuharibu chakula chao chote,
17 Akatuma mtu mbele yao; Yusufu aliuzwa kama mtumishi.
naye akatuma mtu mbele yao, Yosefu, aliyeuzwa kama mtumwa.
18 Miguu yake ilifungwa kwa pingu; alivishwa mnyororo wa chuma shingoni mwake,
Walichubua miguu yake kwa minyororo, shingo yake ilifungwa kwa chuma,
19 mpaka wakati wa maneno yake ulipotimia, nalo neno la Yahwe lilimjaribu.
hadi yale aliyotangulia kusema yalipotimia, hadi neno la Bwana lilipomthibitisha.
20 Mfalme alituma watumishi kumfungua; mtawala wa watu alimuweka huru.
Mfalme alituma watu wakamfungua, mtawala wa watu alimwachia huru.
21 Alimuweka kuwa msimamizi wa nyumba yake kama mtawala wa mali zake zote
Alimfanya mkuu wa nyumba yake, mtawala juu ya vyote alivyokuwa navyo,
22 kuwaelekeza wakuu kama alivyopenda na kuwafundisha viongozi wake hekima.
kuwaelekeza wakuu wa mfalme apendavyo na kuwafundisha wazee wake hekima.
23 Kisha Israeli iliingia Misri, na Yakobo aliishi kwa muda katika nchi ya Hamu.
Kisha Israeli akaingia Misri, Yakobo akaishi kama mgeni katika nchi ya Hamu.
24 Yahwe aliwajalia watu wake wazae sana, na aliwafanya wenye nguvu kuliko adui zao.
Bwana aliwafanya watu wake kuzaana sana, akawafanya kuwa wengi sana kuliko adui zao,
25 Alisababisha adui zao wawachukie watu wake, na kuwatendea visivyo watumishi wake.
ndiye aliigeuza mioyo yao iwachukie watu wake, wakatenda hila dhidi ya watumishi wake.
26 Alimtuma Musa, mtumishi wake, na Haruni, ambaye alikwisha mchagua.
Akamtuma Mose mtumishi wake, pamoja na Aroni, aliyemchagua.
27 Walifanya ishara zake kati ya Wamisri na maajabu yake katika ya nchi ya Hamu.
Walifanya ishara zake za ajabu miongoni mwao, miujiza yake katika nchi ya Hamu.
28 Alituma giza na likaifanya nchi hiyo kuwa giza, lakini watu wake hawakutii amri zake.
Alituma giza na nchi ikajaa giza, kwani si walikuwa wameyaasi maneno yake?
29 Aligeuza maji kuwa damu na aliua samaki wao.
Aligeuza maji yao kuwa damu, ikasababisha samaki wao kufa.
30 Nchi yao ilijaa vyura, hata katika vyumba vya watawala wao.
Nchi yao ilijaa vyura tele, ambao waliingia hadi kwenye vyumba vya kulala vya watawala wao.
31 Alisema, na makundi ya inzi na chawa wakaja mjini mwote.
Alisema, yakaja makundi ya mainzi, na viroboto katika nchi yao yote.
32 Aliigeuza mvua yao kuwa mvua ya mawe, pamoja na miali ya moto juu ya ardhi yao.
Alibadilisha mvua yao ikawa mvua ya mawe, yenye umeme wa radi nchini yao yote,
33 Aliiharibu mizabibu yao na mitini yao; akaivunja miti ya mji wao.
akaharibu mizabibu yao na miti ya tini, na akaangamiza miti ya nchi yao.
34 Alisema, na nzige wakaja, nzige wengi sana.
Alisema, nzige wakaja, tunutu wasio na idadi,
35 Nzige walikula mboga zao zote za majani katika nchi yao. Walikula mazao yote ardhini.
wakala kila jani katika nchi yao, wakala mazao ya ardhi yao.
36 Aliua kila mzaliwa wa kwanza katika nchi yao, malimbuko ya nguvu zao.
Kisha akawaua wazaliwa wote wa kwanza katika nchi yao, matunda ya kwanza ya ujana wao wote.
37 Aliwatoa nje Waisraeli wakiwa na fedha na dhahabu; hakuna mmoja wa kabila lake aliyejikwaa njiani.
Akawatoa Israeli katika nchi wakiwa na fedha na dhahabu nyingi, wala hakuna hata mmoja kutoka kabila zao aliyejikwaa.
38 Misri ilifurahi walipoondoka, maana Wamisri waliwaogopa.
Misri ilifurahi walipoondoka, kwa sababu hofu ya Israeli ilikuwa imewaangukia.
39 Alitandaza wingu liwafunike na alifanya moto uwaangazie wakati wa usiku.
Alitandaza wingu kama kifuniko, na moto kuwamulikia usiku.
40 Waisraeli waliomba chakula, naye aliwaletea kware na aliwatosheleza kwa mkate kutoka mbiguni.
Waliomba, naye akawaletea kware, akawashibisha kwa mkate wa mbinguni.
41 Aliugawa mwamba, maji yalimwagika kutoka humo; yalitiririka katika jangwa kama mto.
Alipasua mwamba, maji yakabubujika, yakatiririka jangwani kama mto.
42 Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu aliyoifanya kwa Ibrahimu mtumishi wake.
Kwa maana alikumbuka ahadi yake takatifu, aliyompa Abrahamu mtumishi wake.
43 Aliwaongoza watu wake kwa furaha, wateule wake kwa kelele za ushindi.
Aliwatoa watu wake kwa furaha, wateule wake kwa kelele za shangwe,
44 Aliwapa nchi za mataifa; walichukua milki ya mali za watu
akawapa nchi za mataifa, wakawa warithi wa mali wengine walikuwa wameitaabikia:
45 ili waweze kushika amri zake na kutii sheria zake. Msifuni Yahwe.
alifanya haya ili wayashike mausia yake na kuzitii sheria zake. Msifuni Bwana.

< Zaburi 105 >