< Zaburi 104 >

1 Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote, Ewe Yahwe Mungu wangu, wewe ni mkubwa sana; umevikwa kwa utukufu na enzi.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Ee Bwana Mungu wangu, wewe ni mkuu sana, umejivika utukufu na enzi.
2 Unajifunika mwenyewe kwa nuru kama kwa mavazi; umetandaza mbingu kama pazia za hema.
Amejifunika katika nuru kama vile kwa vazi, amezitandaza mbingu kama hema
3 Umeweka mawinguni mihimili ya vyumba vyako; huyafanya mawingu gari lako; hutembea juu ya mbawa za upepo.
na kuziweka nguzo za orofa yake juu ya maji. Huyafanya mawingu kuwa gari lake, na hupanda kwenye mbawa za upepo.
4 Yeye huufanya upepo kuwa wajumbe wake, miale ya moto kuwa watumishi wake.
Huzifanya pepo kuwa wajumbe wake, miali ya moto watumishi wake.
5 Aliiweka misingi ya nchi, nayo haitahamishwa kamwe.
Ameiweka dunia kwenye misingi yake, haiwezi kamwe kuondoshwa.
6 Wewe uliifunika nchi kwa maji kama kwa mavazi; maji yalifunika milima.
Uliifunika kwa kilindi kama kwa vazi, maji yalisimama juu ya milima.
7 Kukemea kwako kulifanya maji kupungua; kwa sauti ya radi yako yakaondoka kasi.
Lakini kwa kukemea kwako maji yalikimbia, kwa sauti ya radi yako yakatoroka,
8 Milima iliinuka, na mabonde yakaenea mahali ambapo wewe ulikwisha pachagua kwa ajili yao.
yakapanda milima, yakateremka mabondeni, hadi mahali pale ulipoyakusudia.
9 Umeweka mipaka kwa ajili yao ambao hayawezi kuupita; hayawezi kuifunika nchi tena.
Uliyawekea mpaka ambao hayawezi kuuvuka, kamwe hayataifunika dunia tena.
10 Yeye alifanya chemchemi kutiririsha maji mabondeni; mito kutiririka katikati ya milima.
Huzifanya chemchemi zimwage maji mabondeni, hutiririka kati ya milima.
11 Inasambaza maji kwa ajili ya wanyama wote wa shambani; punda wa porini hukata kiu yao.
Huwapa maji wanyama wote wa kondeni, punda-mwitu huzima kiu yao.
12 Kandokando ya mito ndege hujenga viota vyao; huimba kati ya matawi.
Ndege wa angani hufanya viota kando ya maji, huimba katikati ya matawi.
13 Humwagilia milima kutoka katika chumba chake cha maji mawinguni. Nchi imejazwa kwa matunda ya kazi yake.
Huinyeshea milima kutoka orofa zake, dunia inatoshelezwa kwa matunda ya kazi yake.
14 Huzifanya nyasi kukua kwa ajili ya mifugo na mimea kwa ajili ya binadamu kulima ili kwamba mwanadamu aweze kuzalisha chakula toka nchini.
Huyafanya majani ya mifugo yaote, na mimea kwa watu kulima, wajipatie chakula kutoka ardhini:
15 Hutengeneza mvinyo kumfurahisha mwanadamu, mafuta yakumfanya uso wake ung'ae, na chakula kwa ajili ya kuimarisha uhai wake.
divai ya kuufurahisha moyo wa mwanadamu, mafuta kwa ajili ya kungʼarisha uso wake, na mkate wa kutia mwili nguvu.
16 Miti ya Yahwe hupata mvua nyingi; Mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
Miti ya Bwana inanyeshewa vizuri, mierezi ya Lebanoni aliyoipanda.
17 Hapo ndege hutengeneza viota vyao. Na korongo, misunobari ni nyuma yake.
Humo ndege hufanya viota vyao, korongo ana nyumba yake kwenye msunobari.
18 Mbuzi mwitu huishi kwenye milima mrefu; na urefu wa milima ni kimilio la wibari.
Milima mirefu ni makao ya mbuzi-mwitu, majabali ni kimbilio la pelele.
19 Aliuchagua mwezi kuweka alama ya majira; jua latambua kuchwa kwake.
Mwezi hugawanya majira, na jua hutambua wakati wake wa kutua.
20 Wewe hufanya giza la usiku ambapo wanyama wote wa msituni hutoka nje.
Unaleta giza, kunakuwa usiku, wanyama wote wa mwituni huzurura.
21 Wana simba huunguruma kwa ajili ya mawindo na hutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
Simba hunguruma kwa mawindo yao, na kutafuta chakula chao kutoka kwa Mungu.
22 Jua linapochomoza, huenda zao na kujilaza mapangoni mwao.
Jua huchomoza, nao huondoka, hurudi na kulala katika mapango yao.
23 Wakati huo huo, watu hutoka nje kuelekea kazi zao na utumishi wake mpaka jioni.
Kisha mwanadamu huenda kazini mwake, katika kazi yake mpaka jioni.
24 Yahwe, ni jinsi gani kazi zako zilivyo nyingi na za aina mbalimbali! Kwa hekima ulizifanya zote; nchi inafurika kwa kazi zako.
Ee Bwana, jinsi matendo yako yalivyo mengi! Kwa hekima ulizifanya zote, dunia imejaa viumbe vyako.
25 Kule kuna bahari, yenye kina kirefu na pana, ikiwa na viume vingi visivyo hesabika, vyote vidogo na vikubwa.
Pale kuna bahari, kubwa na yenye nafasi tele, imejaa viumbe visivyo na idadi, vitu vyenye uhai vikubwa na vidogo.
26 Meli husafili humo, na ndimo alimo Lewiathani uliye muumba acheze baharini.
Huko meli huenda na kurudi, pia Lewiathani, uliyemuumba acheze ndani yake.
27 Hawa wote hukutazama wewe uwape chakula kwa wakati.
Hawa wote wanakutazamia wewe, uwape chakula chao kwa wakati wake.
28 Unapowapa chakula, hukusanyika; ufunguapo mkono wako, wanatosheka.
Wakati unapowapa, wanakikusanya, unapofumbua mkono wako, wao wanashibishwa mema.
29 Unapouficha uso wako, wanateseka; ukiiondoa pumzi yao, wanakufa na kurudi mavumbini.
Unapoficha uso wako, wanapata hofu, unapoondoa pumzi yao, wanakufa na kurudi mavumbini.
30 Unapotuma Roho yako, wanaumbwa, nawe unaifanya upya nchi.
Unapopeleka Roho wako, wanaumbwa, nawe huufanya upya uso wa dunia.
31 Utukufu wa Yahwe na udumu milele; Yahwe na aufurahie uumbaji wake.
Utukufu wa Bwana na udumu milele, Bwana na azifurahie kazi zake:
32 Yeye hutazama nchi, nayo hutikisika; huigusa milima, nayo hutoa moshi.
yeye aitazamaye dunia, nayo ikatetemeka, aigusaye milima, nayo ikatoa moshi.
33 Nitamwimbia Yahwe maisha yangu yote; nitamwimbia sifa Mungu wangu nigali ninaishi.
Nitamwimbia Bwana maisha yangu yote; nitaimba sifa kwa Mungu wangu muda wote ninaoishi.
34 Mawazo yangu na yawe matamu kwake; nitafurahia katika Yahwe.
Kutafakari kwangu na kumpendeze yeye, ninapofurahi katika Bwana.
35 Wenye dhambi na waondoshwe katika nchi, na waovu wasiwepo tena. Ninamsifu Yahwe maisha yangu yote. Msifuni Yahwe.
Lakini wenye dhambi na watoweke katika dunia na waovu wasiwepo tena. Ee nafsi yangu, msifu Bwana. Msifuni Bwana.

< Zaburi 104 >