< Zaburi 103 >
1 Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote, na vyote vilivyomo ndani yangu, nitalisifu jina lake takatifu.
Zaburi ya Daudi. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Vyote vilivyomo ndani yangu vilihimidi jina lake takatifu.
2 Maishani mwangu mwote nitamsifu Yahwe, na kukumbuka matendo yake yote mazuri.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, wala usisahau wema wake wote,
3 Yeye husamehe dhambi zako zote; huponya magonjwa yako yote.
akusamehe dhambi zako zote, akuponya magonjwa yako yote,
4 Huukomboa uhai wako dhidi ya uharubifu; hukuvika taji kwa uaminifu wa agano lake na hutenda kwa rehema.
aukomboa uhai wako na kaburi, akuvika taji ya upendo na huruma,
5 Huyatosheleza maisha yako kwa mambo mema ili kwamba ujana wako ufanywe upya kama tai.
atosheleza mahitaji yako kwa vitu vyema, ili ujana wako uhuishwe kama wa tai.
6 Yahwe hutenda yaliyo haki naye hutenda hukumu ya haki kwa ajili ya wote walio onewa.
Bwana hutenda haki, naye huwapa hukumu ya haki wote wanaoonewa.
7 Alimjulisha Musa njia zake, matendo yake kwa uzao wa Israeli.
Alijulisha Mose njia zake, na wana wa Israeli matendo yake.
8 Yahwe ni wa huruma na neema; ni mvumilivu; ana agano kuu la uaminifu.
Bwana ni mwingi wa huruma na mwenye neema; si mwepesi wa hasira, bali amejaa upendo.
9 Hataadhibu siku zote; hakasiriki siku zote.
Yeye hatalaumu siku zote, wala haweki hasira yake milele,
10 Hatushughulikii sisi kama dhambi zetu zinavyostahili au kutulipa kulingana na uhitaji wa dhambi zetu.
yeye hatutendei kulingana na dhambi zetu wala hatupatilizi kwa kadiri ya maovu yetu.
11 Kama mbingu zilivyo juu zaidi ya nchi, ndivyo ulivyo ukuu wa uaminifu wa agano lake kwao wale wanaomcha yeye.
Kama vile mbingu zilivyo juu ya dunia sana, ndivyo wema wake ulivyo mwingi kwa wanaomcha;
12 Kama vile mashariki ilivyo mbali na magharibi, hivi ndivyo ameondoa hatia zetu za dhambi zetu mbali nasi.
kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, ndivyo Mungu alivyoziweka dhambi zetu mbali nasi.
13 Kama vile baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo Yahwe alivyo na huruma kwao wamchao.
Kama baba alivyo na huruma kwa watoto wake, ndivyo Bwana anavyowahurumia wale wanaomcha;
14 Maana anajua tulivyo umbwa; anajua kuwa tu mavumbi.
kwa kuwa anajua tulivyoumbwa, anakumbuka kwamba sisi tu mavumbi.
15 Kama ilivyo kwa mwanadamu, siku zake ni kama majani; hustawi kama ua katika shamba.
Kuhusu mwanadamu, siku zake ni kama majani, anachanua kama ua la shambani;
16 Upepo hulipiga, nalo hutoweka, na hakuna hata mmoja awezaye kuelezea mahali lilipokua.
upepo huvuma juu yake nalo hutoweka, mahali pake hapalikumbuki tena.
17 Lakini agano la uaminifu wa Yahwe uko kwa wale wamchao yeye milele hata milele. Haki yake ni endelevu kwa uzao wao.
Lakini kutoka milele hata milele upendo wa Bwana uko kwa wale wamchao, nayo haki yake kwa watoto wa watoto wao:
18 Wanashika agano lake na kukumbuka kutii maagizo yake.
kwa wale walishikao agano lake na kukumbuka kuyatii mausia yake.
19 Yahwe ameweka kiti chake cha enzi mbinguni, na ufalme wake watawala juu ya kila mtu.
Bwana ameweka imara kiti chake cha enzi mbinguni, ufalme wake unatawala juu ya vyote.
20 Msifuni Yahwe, enyi malaika zake, ninyi hodari wenye nguvu na mtendao neno lake, na kutii sauti ya neno lake.
Mhimidini Bwana, enyi malaika zake, ninyi mlio mashujaa mnaozitii amri zake, ninyi mnaotii neno lake.
21 Msifuni Yahwe, enyi jeshi la malaika wote, ninyi ni watumishi mfanyao mapenzi yake.
Mhimidini Bwana, ninyi jeshi lake lote la mbinguni, ninyi watumishi wake mnaofanya mapenzi yake.
22 Msifuni Yahwe, viumbe wake wote, mahali popote atawalapo. Nitamsifu Yahwe maisha yangu yote.
Mhimidini Bwana, kazi zake zote kila mahali katika milki yake. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.