< Mithali 8 >

1 Je hekima haiti? Je ufahamu hapazi sauti yake?
Je, hekima haitani? Je, ufahamu hapazi sauti?
2 Juu ya kilima kando ya barabara, kwenye njia panda, hekima anasimama.
Juu ya miinuko karibu na njia, penye njia panda, ndipo asimamapo;
3 Kando ya njia ya kuingilia mjini, karibu na milango ya mji, anaita kwa sauti.
kando ya malango yaelekeayo mjini, kwenye maingilio, hulia kwa sauti kubwa, akisema:
4 Watu, ninawaita ninyi na ninapaza sauti yangu kwa wana wa wanadamu.
“Ni ninyi wanaume, ninaowaita; ninapaza sauti yangu kwa wanadamu wote.
5 Ninyi wajinga, jifunzeni hekima, na ninyi mnaochukia maarifa, lazima mjipatieni moyo wa ufahamu.
Ninyi ambao ni wajinga, pateni akili; ninyi mlio wapumbavu, pateni ufahamu.
6 Sikiliza na mimi nitasema mambo mazuri na nifumbuapo midomo yangu nitaongea haki.
Sikilizeni, kwa maana nina mambo muhimu ya kusema; ninafungua midomo yangu kusema lililo sawa.
7 Maana kinywa changu hunena uaminifu na midomo yangu huchukia uovu.
Kinywa changu husema lililo kweli, kwa maana midomo yangu huchukia uovu.
8 Maneno ya kinywa changu yote ni haki; hakuna kilichogeuzwa wala kupotoshwa.
Maneno yote ya kinywa changu ni haki; hakuna mojawapo lililopotoka wala ukaidi.
9 Maneno yangu yote yamenyooka kwa yule mwenye kuelewa; maneno yangu ni haki kwa wale wanaotafuta maarifa.
Kwa wenye kupambanua yote ni sahihi; hayana kasoro kwa wale wenye maarifa.
10 Chagua fundisho langu badala ya fedha na maarifa kuliko dhahabu safi.
Chagua mafundisho yangu badala ya fedha, maarifa badala ya dhahabu safi,
11 Maana mimi, hekima ni bora kuliko vito; hakuna unachokitamani kinaweza kulinganishwa na mimi.
kwa maana hekima ina thamani kuliko marijani na hakuna chochote unachohitaji kinacholingana naye.
12 Mimi, hekima, naishi kwa utaratibu, na ninamiliki maarifa na busara.
“Mimi hekima, nakaa pamoja na busara; ninamiliki maarifa na busara.
13 Hofu ya Mungu ni kuchukia uovu- nachukia majivuno na kiburi, njia ya uovu, na kauli iliyopotoka- hivyo ninavichukia.
Kumcha Bwana ni kuchukia uovu; ninachukia kiburi na majivuno, tabia mbaya na mazungumzo potovu.
14 Ninaushauri mzuri na hekima sahihi; mimi ni busara; nguvu zipo kwangu.
Ushauri na hukumu sahihi ni vyangu; nina ufahamu na nina nguvu.
15 Kwa njia yangu wafalme hutawala- pia na waungwana, na wote ambao hutawala kwa haki.
Kwa msaada wangu wafalme hutawala na watawala hutunga sheria zilizo za haki,
16 Kwa njia yangu wafalme hutawala na waungwana na wote wanaotawala kwa haki.
kwa msaada wangu wakuu hutawala, na wenye vyeo wote watawalao dunia.
17 Nawapenda wale wanaonipenda, na wale wanaonitafuta kwa bidii, wataniona.
Nawapenda wale wanipendao, na wale wanitafutao kwa bidii wataniona.
18 Kwangu kunautajiri na heshima, utajiri wa kudumu na haki.
Utajiri na heshima viko kwangu, utajiri udumuo na mafanikio.
19 Tunda langu ni bora kuliko dhahabu, bora hata kuliko dhahabu safi.
Tunda langu ni bora kuliko dhahabu safi; kile nitoacho hupita fedha iliyo bora.
20 Ninazalisha kilicho bora kuliko fedha safi. Natembea katika njia ya haki,
Natembea katika njia ya unyofu katika mapito ya haki,
21 katika mapito ambayo huelekea kwenye haki, ili niwape urithi wale wanaonipenda na kuzijaza hazina zao.
nawapa utajiri wale wanipendao na kuzijaza hazina zao.
22 Yehova aliniumba tokea mwanzo- mwazoni mwa matendo yake ya nyakati za kale.
“Bwana aliniumba mwanzoni mwa kazi yake, kabla ya matendo yake ya zamani;
23 Tokea enzi za kale niliwekwa katika nafasi- tokea kwanza, tokea mwanzo wa dunia.
niliteuliwa tangu milele, tangu mwanzoni, kabla ya dunia kuumbwa.
24 Kabla ya bahari, mimi nilizaliwa- kabla ya kuwepo chemchemi zenye maji tele.
Wakati hazijakuwepo bahari, nilikwishazaliwa, wakati hazijakuwepo chemchemi zilizojaa maji;
25 Kabla ya milima na vilima kuwekwa, mimi nilizaliwa.
kabla milima haijawekwa mahali pake, kabla vilima havijakuwepo, nilikwishazaliwa,
26 Nilizaliwa kabla ya Yehova hajaiumba dunia wala makonde, hata mavumbi ya kwanza katika dunia.
kabla hajaumba dunia wala mashamba yake au vumbi lolote la dunia.
27 Nilikuwepo alipoziimarisha mbingu, wakati alipochora mstari katika sura ya kilindi.
Nilikuwepo alipoziweka mbingu mahali pake, wakati alichora mstari wa upeo wa macho juu ya uso wa kilindi,
28 Nilikuwepo alipoimarisha anga la juu na wakati wa kutengeneza kina cha chemchemi.
wakati aliweka mawingu juu na kuziweka imara chemchemi za bahari,
29 Nilikuwepo alipotengeneza mipaka ya bahari, ili maji yasisambae kuvuka pale alipoyaamuru, na wakati anaamuru misingi ya dunia sehemu ya kukaa.
wakati aliiwekea bahari mpaka wake ili maji yasivunje agizo lake, na wakati aliweka misingi ya dunia.
30 Nilikuwa kando yake, kama fundistadi mkuu, na mimi nilikuwa furaha yake siku kwa siku, nikifurahi mbele zake daima.
Wakati huo nilikuwa fundi stadi kando yake. Nilijazwa na furaha siku baada ya siku, nikifurahi daima mbele zake,
31 Nilikuwa nikifurahi katika dunia yake yote na furaha yangu ilikuwa kwa wana wa wanadamu.
nikifurahi katika dunia yake yote nami nikiwafurahia wanadamu.
32 Na sasa, wanangu, nisikilizeni, maana wale wazishikao njia zangu watakuwa na furaha.
“Basi sasa wanangu, nisikilizeni; heri wale wanaozishika njia zangu.
33 Sikilizeni fundisho langu na mpate hekima; wala msilipuuze.
Sikilizeni mafundisho yangu mwe na hekima; msiyapuuze.
34 Anisikilizaye atakuwa na furaha- kila siku akitazama katika malango yangu, akinisubiri pembeni mwa milango ya masikani yangu.
Heri mtu yule anisikilizaye mimi, akisubiri siku zote malangoni mwangu, akingoja kwenye vizingiti vya mlango wangu.
35 Maana yeyote anionaye mimi, anapata uzima, naye atapata kibali kwa Yehova.
Kwa maana yeyote anipataye mimi amepata uzima na kujipatia kibali kutoka kwa Bwana.
36 Na yeyote asiyeniona mimi, hujiumiza mwenyewe, wote wanaonichukia hupenda mauti.
Lakini yeyote ashindwaye kunipata hujiumiza mwenyewe; na wote wanichukiao mimi hupenda mauti.”

< Mithali 8 >