< Mithali 4 >

1 Wanangu, sikilizeni, fundisho la baba, na zingatieni ili mjue maana ya ufahamu.
Sikilizeni wanangu, mafundisho ya baba yenu; sikilizeni kwa makini na mpate ufahamu.
2 Mimi ninawapa mafundisho mazuri; msiyaache mafundisho yangu.
Ninawapa mafundisho ya maana, kwa hiyo msiyaache mafundisho yangu.
3 Mimi nilikuwa mwana kwa baba yangu, mpole na mtoto pekee kwa mama yangu,
Nilipokuwa mvulana mdogo katika nyumba ya baba yangu, ningali mchanga na mtoto pekee kwa mama yangu,
4 baba alinifundisha akiniambia, “Moyo wako uzingatie sana maneno yangu; shika amri zangu nawe uishi.
baba alinifundisha akisema, “Yashike maneno yangu yote kwa moyo wako wote; yashike maagizo yangu na wewe utaishi.
5 Jipatie hekima na ufahamu; usisahau na kuyakataa maneno ya kinywa changu;
Pata hekima, pata ufahamu; usiyasahau maneno yangu wala usiyaache.
6 usiiache hekima nayo itakulinda; ipenda nayo itakuhifadhi salama.
Usimwache hekima naye atakuweka salama; mpende, naye atakulinda.
7 Hekima ni kitu cha muhimu sana, hivyo jipatie hekima na tumia namna zote kuweza kupata ufahamu.
Hekima ni bora kuliko vitu vyote; kwa hiyo jipe hekima. Hata ikikugharimu vyote ulivyo navyo, pata ufahamu.
8 Tunza hekima nayo itakutukuza; ikumbatie nayo itakuheshimu.
Mstahi, naye atakukweza; mkumbatie, naye atakuheshimu.
9 Hekima itaweka kilemba cha heshima juu ya kichwa chako; itakupa taji zuri.
Atakuvika shada la neema kichwani mwako na kukupa taji ya utukufu.”
10 Mwanangu, sikiliza, na kuzingatia maneno yangu, nawe utapata miaka mingi ya maisha yako.
Sikiliza mwanangu, kubali ninachokuambia, nayo miaka ya maisha yako itakuwa mingi.
11 Ninakuelekeza katika njia ya hekima, nimekuongoza katika mapito yaliyonyooka.
Ninakuongoza katika njia ya hekima na kukuongoza katika mapito yaliyonyooka.
12 Unapotembea, hakuna atakayesimama katika njia yako na kama ukikimbia hutajikwaa.
Utembeapo, hatua zako hazitazuiliwa; ukimbiapo, hutajikwaa.
13 Shika mwongozo wala usiuache, utakuongoza, maana ni uzima wako.
Mkamate sana elimu, usimwache aende zake; mshike, maana yeye ni uzima wako.
14 Usifuate njia ya waovu wala usiende katika njia ya watendao uovu.
Usiuweke mguu wako katika njia ya waovu wala usitembee katika njia ya watu wabaya.
15 Jiepushe nayo, usipite katika njia hiyo; geuka na upite njia nyingine.
Epukana nayo, usisafiri katika njia hiyo; achana nayo, na uelekee njia yako.
16 Maana hawawezi kulala mpaka wafanye ubaya na hupotewa na usingizi hadi wasababishe mtu kujikwaa.
Kwa kuwa hawawezi kulala mpaka watende uovu; wanashindwa hata kusinzia mpaka wamwangushe mtu.
17 Maana wao hula mkate wa uovu na hunywa divai ya vurugu.
Wanakula mkate wa uovu, na kunywa mvinyo wa jeuri.
18 Bali njia ya mwenye kutenda haki ni kama mwanga ung'aao, huangaza zaidi na zaidi hadi mchana inapowasili kwa ukamilifu.
Njia ya wenye haki ni kama nuru ya kwanza ya mapambazuko, ambayo hungʼaa zaidi na zaidi mpaka mchana mkamilifu.
19 Njia ya waovu ni kama giza - hawajui ni kitu gani huwa wanajikwaa juu yake.
Lakini njia ya waovu ni kama giza nene; hawajui kinachowafanya wajikwae.
20 Mwanangu, zingatia maneno yangu; sikiliza kauli zangu.
Mwanangu, yasikilize kwa makini yale ninayokuambia; sikiliza kwa makini maneno yangu.
21 Usiziache zikaondoka machoni pako; uzitunze katika moyo wako.
Usiruhusu yaondoke machoni pako, yahifadhi ndani ya moyo wako;
22 Maana maneno yangu ni uzima kwa wenye kuyapata na afya katika mwili wao.
kwa sababu ni uzima kwa wale wanaoyapata na afya kwa mwili wote wa mwanadamu.
23 Ulinde salama moyo wako na uukinge kwa bidii zote; kwa kuwa katika moyo hububujika chemichemi za uzima.
Zaidi ya yote, linda moyo wako, kuliko yote uyalindayo, maana ndiko zitokako chemchemi za uzima.
24 Jiepushe na kauli za udanganyifu na ujiepushe na mazungumzo ya ufisadi.
Epusha kinywa chako na ukaidi; weka mazungumzo machafu mbali na midomo yako.
25 Macho yako yatazame mbele kwa unyoofu na kwa uthabiti tazama mbele sawasawa.
Macho yako na yatazame mbele, kaza macho yako moja kwa moja mbele yako.
26 Usawazishe pito la mguu wako; na njia zako zote zitakuwa salama.
Sawazisha mapito ya miguu yako na njia zako zote ziwe zimethibitika.
27 Usigeuke upande wa kulia au kushoto; ondoa mguu wako mbali na uovu.
Usigeuke kulia wala kushoto; epusha mguu wako na ubaya.

< Mithali 4 >