< Mithali 3 >
1 Mwanangu, usizisahau amri zangu na uyatunze mafundisho yangu katika moyo wako,
Mwanangu, usisahau mafundisho yangu, bali zitunze amri zangu moyoni mwako,
2 maana ziatakuongezea siku zako na miaka ya maisha yako na amani.
kwa kuwa zitakuongezea miaka mingi ya maisha yako na kukuletea mafanikio.
3 Usiache utiifu wa agano na uaminifu viondoke kwako, vifunge katika shingo yako, viandike katika vibao vya moyo wako.
Usiache kamwe upendo na uaminifu vitengane nawe; vifunge shingoni mwako, viandike katika ubao wa moyo wako.
4 Ndipo utapata kibali na heshima mbele Mungu na wanadamu.
Ndipo utapata kibali na jina zuri mbele za Mungu na mwanadamu.
5 Mtegemee Yehova kwa moyo wako wote na wala usitegemee ufahamu wako mwenyewe,
Mtumaini Bwana kwa moyo wako wote wala usizitegemee akili zako mwenyewe;
6 katika njia zako zote mkiri Yeye na yeye atayanyosha mapito yako.
katika njia zako zote mkiri yeye, naye atayanyoosha mapito yako.
7 Usiwe mwenye busara machoni pako mwenyewe; mche Yehova na jiepushe na uovu.
Usiwe mwenye hekima machoni pako mwenyewe; mche Bwana ukajiepushe na uovu.
8 Itakuponya mwili wako na kukuburudisha mwili wako.
Hii itakuletea afya mwilini mwako, na mafuta kwenye mifupa yako.
9 Mheshimu Yehova kwa utajiri wako na kwa malimbuko ya mazao kwa kila unachozalisha,
Mheshimu Bwana kwa mali zako na kwa malimbuko ya mazao yako yote;
10 na ndipo ghala zako zitajaa na mapipa makubwa yatafurika kwa divai mpya.
ndipo ghala zako zitakapojaa hadi kufurika, viriba vyako vitafurika kwa mvinyo mpya.
11 Mwanangu, usidharau kuadibishwa na Yohova na wala usichukie karipio lake,
Mwanangu, usiidharau adhabu ya Bwana na usichukie kukaripiwa naye,
12 maana Yehova huwaadibisha wale wapendao, kama baba anavyoshughulika kwa mtoto wake ampendezaye.
kwa sababu Bwana huwaadibisha wale awapendao, kama vile baba afanyavyo kwa mwana apendezwaye naye.
13 Yeye apataye hekima anafuraha, naye hupata ufahamu.
Heri mtu yule aonaye hekima, mtu yule apataye ufahamu,
14 Kwani katika hekima unapata manufaa kuliko ukibadilisha kwa fedha na faida yake inafaa zaidi kuliko dhahabu.
kwa maana hekima ana faida kuliko fedha na mapato yake ni bora kuliko ya dhahabu safi.
15 Hekima inathamani zaidi kuliko kito, na hakuna unachokitamani kinaweza kulinganishwa na hekima.
Hekima ana thamani kuliko marijani; hakuna chochote unachokitamani kinachoweza kulinganishwa naye.
16 Yeye anasiku nyingi katika mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto ni utajiri na heshima.
Maisha marefu yako katika mkono wake wa kuume; katika mkono wake wa kushoto kuna utajiri na heshima.
17 Njia zake ni njia za ukarimu na mapito yake ni amani.
Njia zake zinapendeza, mapito yake yote ni amani.
18 Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomshikilia, wale wanaomshikilia wanafuraha.
Yeye ni mti wa uzima kwa wale wanaomkumbatia; wale wamshikao watabarikiwa.
19 Kwa hekima Yehova aliweka msingi wa dunia, kwa ufahamu aliziimarisha mbingu.
Kwa hekima Bwana aliiweka misingi ya dunia, kwa ufahamu aliziweka mbingu mahali pake;
20 Kwa maarifa yake vina vilipasuka na mawingu kudondosha umande wake.
kwa maarifa yake vilindi viligawanywa, nayo mawingu yanadondosha umande.
21 Mwanangu, zingatia hukumu ya kweli na ufahamu, na wala usiache kuvitazama.
Mwanangu, hifadhi maamuzi mema na busara, usiache vitoke machoni pako;
22 Vitakuwa uzima wa nafsi yako na urembo wa hisani wa kuvaa shingoni mwako.
ndipo vitakapokuwa uzima nafsini mwako na pambo la neema shingoni mwako.
23 Ndipo utatembea katika njia yako kwa usalama na mguu wako hautajikwaa;
Kisha utaenda katika njia yako salama, wala mguu wako hautajikwaa;
24 ulalapo hutaogopa; utakapolala, usingizi wako utakuwa mtamu.
ulalapo, hautaogopa; ulalapo usingizi wako utakuwa mtamu.
25 Usitishwe na hofu ya ghafula au uharibifu uliosababishwa na waovu unapotokea,
Usiogope maafa ya ghafula au maangamizi yanayowapata waovu,
26 kwa maana Yehova utakuwa upande wako na ataulinda mguu wako usinaswe kwenye mtego.
kwa kuwa Bwana atakuwa tumaini lako na kuepusha mguu wako kunaswa katika mtego.
27 Usizuie mema kwa wale wanaoyastahili, wakati utendaji upo ndani ya mamlaka yako.
Usizuie wema kwa wale wanaostahili ikiwa katika uwezo wako kutenda.
28 Jirani yako usimwambie, “Nenda, na uje tena, na kesho nitakupa,” wakati pesa unazo.
Usimwambie jirani yako, “Njoo baadaye, nitakupa kesho”: wakati wewe unacho kitu kile karibu nawe.
29 Usiweke mpango wa kumdhuru jirani yako- anayeishi jirani nawe na yeye anakuamini.
Usifanye hila ya kumdhuru jirani yako, ambaye anaishi karibu na wewe akikuamini.
30 Usishindane na mtu pasipo sababu, ikiwa hajafanya chochote kukudhuru.
Usimshtaki mtu bila sababu, wakati hajakutenda dhara lolote.
31 Usimhusudu mtu jeuri au kuchagua njia zake zozote.
Usimwonee wivu mtu mwenye jeuri wala kuchagua njia yake iwayo yote,
32 Maana mtu mjanja ni chukizo kwa Yehova, bali humleta mtu mwaminifu kwenye tumaini lake.
kwa kuwa Bwana humchukia mtu mpotovu, lakini siri yake iko kwa mwenye haki.
33 Laana ya Yehova ipo katika nyumba ya watu waovu, bali huibariki maskani ya watu wenye haki.
Laana ya Bwana i juu ya nyumba ya mwovu, lakini yeye huibariki nyumba ya mwenye haki.
34 Yeye huwadhihaki wenye dhihaka, bali huwapa hisani watu wanyenyekevu.
Huwadhihaki wale wanaodhihaki, lakini huwapa neema wale wanyenyekevu.
35 Watu wenye busara huirithi heshima, bali wapumbavu huinuliwa kwa fedheha yao wenyewe.
Wenye hekima hurithi heshima, bali huwaaibisha wapumbavu.