< Mithali 25 >
1 Hizi tena ni mithali za Sulemani, zilinakiliwa na watu wa Hezekia, mfalme wa Yuda.
2 Ni utukufu wa Mungu kuficha jambo, bali utukufu wa wafalme kutafiti juu ya jambo.
3 Kama mbingu ni kwa kimo na dunia ni kwa kina, ndivyo hivyo moyo wa wafalme hauchunguziki.
4 Ondoa takataka kutoka kwenye fedha na mfua vyuma anaweza kutumia fedha katika ufundi wake.
5 Pamoja na hayo, waondoe watu waovu mbele ya mfalme na kiti chake cha enzi kitaimarishwa kwa kutenda haki.
6 Usijitukuze mwenyewe mbele ya mfalme na usisimame katika sehemu iliyoteuliwa kwa watu wakuu.
7 Ni bora yeye akuambie, “Njoo hapa” kuliko wewe kujiaibisha mbele ya mkuu.
8 Usiharakishe kufanya kuhukumu, kwa kile ulichokishuhudia. Maana utafanya nini mwishoni, wakati jirani yako atakapokuaibisha?
9 Jitetee kesi yako kati ya jirani yako na wewe na usifunue siri ya mtu mwingine,
10 au vinginevyo anayekusikia ataleta aibu juu yako na taarifa mbaya juu yako haiwezi kunyamazishwa.
11 Kunena maneno yenye kuchaguliwa vizuri, ni kama nakshi za dhahabu iliyoungwa kwenye fedha.
12 Kama pete ya dhahabu au kito kilichotengenezwa kwa dhahabu safi ndivyo lilivyo karipio la busara kwenye sikio linalosikia.
13 Kama baridi ya theluji wakati wa mavuno ndivyo alivyo mjumbe mwaminifu kwa wenye kumtuma; huyahifadhi maisha ya mabwana wake.
14 Kama mawingu na upepo bila mvua ndivyo alivyo mwenye kujisifu kuhusu zawadi asiyoitoa.
15 Kwa uvumilivu mtawala anaweza kushawishiwa na ulimi raini unaweza kuvunja mfupa.
16 Kama utapata asali, kula ya kutosha- vingenevyo, ukila nyingi sana, utaitapika.
17 Usiweke mguu wako kwenye nyumba ya jirani yako mara nyingi, anaweza kuchoshwa nawe na kukuchukia.
18 Mtu anayetoa ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake ni kama rungu lililotumiwa katika vita, au upanga, au mshale mkali.
19 Kumtumaini mtu asiye mwaminifu wakati wa taabu ni kama jino bovu au mguu unaoteleza.
20 Kama mtu anayevua nguo katika hali ya baridi, au kama siki iliyotiwa kwenye magadi, ndivyo alivyo anayeimba wimbo kwa mwenye moyo mzito.
21 Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale na kama ana kiu, mpe maji ya kunywa,
22 maana utamwekea mkaa juu ya kichwa chake na Yehova atakupa thawabu.
23 Ni hakika upepo wa kaskazini huleta mvua, ndivyo mtu anayesema siri hufanya sura zikasirike.
24 Ni bora kuishi kwenye pembe ya darini kuliko kuchangia nyumba pamoja na mwanamke mgomvi.
25 Kama maji ya baridi kwa mwenye kiu, ndivyo ilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali.
26 Kama chemchemi iliyochafuliwa au kisima kilichoharibiwa ndivyo alivyo mtu mwema ambaye huyumbayumba mbele ya watu waovu.
27 Si vema kula asali nyingi mno; hivyo ni kama kutafuta heshima baada heshima.
28 Mtu bila kujitawala ni kama mji ulibomolewa na usiokuwa na kuta.