< Mithali 23 >

1 Unapoketi kula pamoja na mtawala, angalia kwa uangalifu kilichopo mbele yako,
Uketipo kula chakula na mtawala, angalia vyema kile kilicho mbele yako,
2 na kama ni mtu unayependa kula chakula sana weka kisu kooni.
na utie kisu kooni mwako kama ukiwa mlafi.
3 Usitamani vinono vyake maana ni chakula cha uongo.
Usitamani vyakula vyake vitamu kwa kuwa chakula hicho ni cha hila.
4 Usifanye kazi sana ili kupata mali; uwe na busara ya kutosha ili ujue wakati wa kuacha.
Usijitaabishe ili kuupata utajiri, uwe na hekima kuonyesha kujizuia.
5 Je utaruhusu macho yako yaangaze juu yake? Itaondoka, maana itawaa mabawa kama tai na kuruka angani.
Kufumba na kufumbua utajiri hutoweka, huwa kama umepata mabawa ghafula, ukaruka na kutoweka angani kama tai.
6 Usile chakula cha yule mwenye jicho baya- na usiwe na shauku ya vinono vyake,
Usile chakula cha mtu mchoyo, usitamani vyakula vyake vitamu,
7 maana ni mtu mwenye kuhesabu gharama ya chakula. “Kula na kunywa!” anakuambia, lakini moyo wake haupo pamoja nawe.
kwa maana yeye ni aina ya mtu ambaye kila mara anafikiri juu ya gharama. Anakuambia, “Kula na kunywa,” lakini moyo wake hauko pamoja nawe.
8 Utatapika kiasi kidogo ulichokula na utakuwa umepoteza sifa zako njema.
Utatapika kile kidogo ulichokula, nawe utakuwa umepoteza bure maneno yako ya kumsifu.
9 Usiongee katika usikivu wa mpumbavu, maana atadharau hekima ya maneno yako.
Usizungumze na mpumbavu, kwa maana atadhihaki hekima ya maneno yako.
10 Usihamishe jiwe la mpaka wa kale au kunyang'anya mashamba ya yatima,
Usisogeze jiwe la mpaka wa zamani wala kunyemelea kwenye mashamba ya yatima,
11 maana Mkombozi wao ni imara na atatetea kesi yao dhidi yako.
kwa kuwa Mtetezi wao ni mwenye nguvu, atalichukua shauri lao dhidi yako.
12 Elekeza moyo wako katika mafundisho na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
Elekeza moyo wako kwenye mafundisho na masikio yako kwenye maneno ya maarifa.
13 Usizuie kuadilisha mtoto, maana ukimchapa kwa fimbo, hatakufa.
Usimnyime mtoto adhabu, ukimwadhibu kwa fimbo, hatakufa.
14 Ni wewe unayepaswa kumchapa kwa fimbo na kuikoa nafsi yake kuzimu. (Sheol h7585)
Mwadhibu kwa fimbo na kuiokoa nafsi yake kutoka mautini. (Sheol h7585)
15 Mwanangu, kama moyo wako una busara, basi moyo wangu utafurahi pia;
Mwanangu, kama moyo wako una hekima, basi moyo wangu utafurahi,
16 sehemu zangu ndani kabisa zitafurahi sana midomo yako inaponena haki.
utu wangu wa ndani utafurahi, wakati midomo yako itakapozungumza lililo sawa.
17 Usiruhusu moyo wako kuwahusudu wenye dhambi, lakini endelea kumcha Yehova siku zote.
Usiuruhusu moyo wako kuwaonea wivu wenye dhambi, bali kila mara uwe na bidii katika kumcha Bwana.
18 Hakika tumaini lako halitaondolewa na siku zako za hapo baadaye.
Hakika kuna tumaini la baadaye kwa ajili yako, nalo tarajio lako halitakatiliwa mbali.
19 Sikia- wewe! - mwanangu, na uwe mwenye busara na uelekeze moyo wako katika njia.
Sikiliza, mwanangu na uwe na hekima, weka moyo wako kwenye njia iliyo sawa.
20 Usishirikiane pamoja na walevi, au pamoja na walaji wa nyama walafi,
Usiwe miongoni mwa wanywao mvinyo, au wale walao nyama kwa pupa,
21 maana mlevi na mlafi wanakuwa masikini na usingizi utawavika kwa matambara.
kwa maana walevi na walafi huwa maskini, nako kusinzia huwavika matambara.
22 Msikilize baba yako ambaye alikuzaa na usimdharau mama yako wakati akiwa mzee.
Msikilize baba yako, aliyekuzaa, wala usimdharau mama yako atakapokuwa mzee.
23 Inunue kweli, lakini usiiuze; nunua hekima, nidhamu, na ufahamu.
Nunua kweli wala usiiuze, pata hekima, adabu na ufahamu.
24 Baba yake mwenye haki atafurahia sana, na yule amzaaye mtoto mwenye busara atamfurahia.
Baba wa mwenye haki ana furaha kubwa, naye aliye na mwana mwenye hekima humfurahia.
25 Mfurahishe baba yako na mama yako na yule aliyekuzaa afurahie.
Baba yako na mama yako na wafurahi, mama aliyekuzaa na ashangilie!
26 Mwanangu, nipe moyo wako na macho yako yachunguze njia zangu.
Mwanangu, nipe moyo wako, macho yako na yafuate njia zangu,
27 Maana malaya ni shimo refu, na mke wa mume mwingine ni kisima chembamba.
kwa maana kahaba ni shimo refu na mwanamke mpotovu ni kisima chembamba.
28 Anavizia kama mnyang'anyi na huongeza idadi ya wadanganyifu miongoni mwa wanadamu.
Kama mnyangʼanyi, hungojea akivizia, naye huzidisha wasio waaminifu miongoni mwa wanaume.
29 Nani mwenye taabu? Nani mwenye huzuni? Nani mwenye mapigano? Nani mwenye malalamiko? Nani mwenye majeraha bila sababu? Nani mwenye macho mekundu?
Ni nani mwenye ole? Ni nani mwenye huzuni? Ni nani mwenye ugomvi? Ni nani mwenye malalamiko? Ni nani aliye na majeraha yasiyo na sababu? Ni nani mwenye macho mekundu?
30 Ni wale ambao huzengea kwenye mvinyo, wale wanaojaribu kuchanganya mvinyo.
Ni hao wakaao sana kwenye mvinyo, hao waendao kuonja mabakuli ya mvinyo uliochanganywa.
31 Usiutazame mvinyo ukiwa mwekundu, wakati unametameta kwenye kikombe na kutelemka kwa uraini.
Usiukodolee macho mvinyo wakati ukiwa mwekundu, wakati unapometameta kwenye bilauri, wakati ushukapo taratibu!
32 Mwisho wake unauma kama nyoka na sumu yake kama kifutu.
Mwishowe huuma kama nyoka na kutia sumu yake kama nyoka mwenye sumu.
33 Macho yako yataona vitu vigeni na moyo wako utatamka vitu vya ukaidi.
Macho yako yataona mambo mageni na moyo wako kuwazia mambo yaliyopotoka.
34 Utakuwa kama anayelala kwenye bahari au anayelala juu ya mlingoti. “
Utakuwa kama alalaye katikati ya bahari, alalaye juu ya kamba ya merikebu.
35 Wamenipiga,” utasema, “lakini sikuumia. Wamenichapa, lakini sikuwa na hisia. Nitaamka lini? Nitatafuta kinywaji kingine.”
Utasema, “Wamenipiga lakini sikuumia! Wamenichapa, lakini sisikii! Nitaamka lini ili nikanywe tena?”

< Mithali 23 >