< Mithali 14 >
1 Mwanamke mwenye busara huijenga nyumba yake, bali mwanamke mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.
Mwanamke mwenye hekima huijenga nyumba yake, bali mpumbavu huibomoa nyumba yake kwa mikono yake mwenyewe.
2 Yeye aendaye kwa uaminifu humcha Yehova, bali mkaidi humdharau katika njia zake.
Yeye ambaye njia zake ni nyofu humcha Bwana, bali yeye ambaye njia zake zimepotoka humdharau Mungu.
3 Katika kinywa cha mpumbavu hutoka chipukizi la kiburi chake, bali midomo ya wenye busara itawalinda.
Mazungumzo ya mpumbavu huleta fimbo mgongoni mwake, bali mwenye hekima hulindwa na maneno ya midomo yake.
4 Pale pasipo na mifugo hori la kulishia ni safi, bali mazao mengi huweza kupatikana kwa nguvu za maksai.
Pale ambapo hakuna mafahali, hori ni tupu, bali kutokana na nguvu za fahali huja mavuno mengi.
5 Shahidi mwaminifu hasemi uongo, bali shahidi wa uongo hupumua uongo.
Shahidi mwaminifu hadanganyi, bali shahidi wa uongo humimina uongo.
6 Mwenye dharau hutafuta hekima na hakuna hata, bali maarifa huja kwa urahisi kwa mwenye ufahamu.
Mwenye mzaha huitafuta hekima na haipati, bali maarifa huja kwa urahisi kwa anayepambanua.
7 Nenda mbali kutoka kwa mtu mpumbavu, maana hutapata maarifa kwenye midomo yake.
Kaa mbali na mtu mpumbavu, kwa maana hutapata maarifa katika midomo yake.
8 Hekima ya mtu mwenye busara ni kuifahamu njia yake mwenyewe, bali upuuzi wa wapumbavu ni udanganyifu.
Hekima ya mwenye busara ni kufikiria njia zake, bali upumbavu wa wapumbavu ni udanganyifu.
9 Wapumbavu hudharau wakati sadaka ya hatia inapotolewa, bali miongoni mwao waaminifu hushiriki fadhila.
Wapumbavu hudhihaki kujirekebisha kutoka dhambi, bali wema hupatikana miongoni mwa wanyofu.
10 Moyo unayajua machungu yake mwenyewe na hakuna mgeni anayeshiriki furaha yake.
Kila moyo hujua uchungu wake wenyewe, wala hakuna yeyote awezaye kushiriki furaha yake.
11 Nyumba ya waovu itaangamizwa, bali hema ya watu waaminifu itasitawi.
Nyumba ya mwovu itaangamizwa, bali hema la mnyofu litastawi.
12 Kuna njia ambayo huonekana sawa kwa mtu, lakini mwisho wake huelekea mauti tu.
Iko njia ionekanayo kuwa sawa kwa mtu, bali mwisho wake huelekeza mautini.
13 Moyo unaweza kucheka lakini bado ukawa katika maumivu na furaha inaweza kukoma ikawa huzuni.
Hata katika kicheko moyo waweza kuuma, nayo furaha yaweza kuishia katika majonzi.
14 Yule asiyemwaminifu atapata anachostahili kwa njia zake, bali mtu mwema atapata kilicho chake.
Wasio na imani watapatilizwa kikamilifu kwa ajili ya njia zao, naye mtu mwema atapewa thawabu kwa ajili ya njia yake.
15 Yeye ambaye hakufundishwa huamini kila kitu, bali mtu mwenye hekima huzifikiria hatua zake.
Mtu mjinga huamini kila kitu, bali mwenye busara hufikiria hatua zake.
16 Mtu mwenye hekima huogopa na kutoka kwenye ubaya, bali mpumbavu huliacha onyo kwa ujasiri.
Mtu mwenye hekima humcha Bwana na kuepuka mabaya, bali mpumbavu hukasirika kwa hamaki na uzembe.
17 Yeye ambaye anakuwa na hasira kwa haraka hufanya mambo ya kipumbavu, na mtu anayefanya hila mbaya huchukiwa.
Mtu anayekasirika kwa haraka hufanya mambo ya upumbavu, naye mtu wa hila huchukiwa.
18 Wajinga hurithi upumbavu, lakini watu wenye hekima wamezingirwa kwa maarifa.
Mjinga hurithi upumbavu, bali wenye busara huvikwa maarifa kichwani kama taji.
19 Hao ambao ni waovu watainama mbele yao walio wema na wale wenye uovu watasujudu kwenye malango ya wenye haki.
Watu wabaya watasujudu mbele ya watu wema, nao waovu kwenye malango ya wenye haki.
20 Mtu masikini huchukiwa hata na marafiki zake, bali watu matajiri wanamarafiki wengi.
Maskini huepukwa hata na majirani zao, bali matajiri wana marafiki wengi.
21 Yeye ambaye huonyesha dharau kwa jirani yake anafanya dhambi, bali yule ambaye huonyesha fadhila kwa masikini anafuraha.
Yeye anayemdharau jirani yake hutenda dhambi, bali amebarikiwa yeye aliye na huruma kwa mhitaji.
22 Je wale wanaofanya njama mbaya hawapotei? Bali wale wenye mpango wa kutenda mema watapokea agano la uaminifu na udhamini
Je, wale wanaopanga ubaya hawapotoki? Bali wale wanaopanga kilicho chema hupata upendo na uaminifu.
23 Katika kazi zote ngumu huja faida, bali palipo na maongezi tu, huelekea kwenye umasikini.
Kazi zote zinazofanywa kwa bidii huleta faida, bali mazungumzo matupu huelekea umaskini tu.
24 Taji ya watu wenye busara ni utajiri wao, bali upuuzi wa wapumbavu huwaletea upuu zaidi.
Utajiri wa wenye hekima ni taji yao, bali upumbavu wa wapumbavu huzaa upumbavu.
25 Shahidi mkweli huokoa maisha, bali shahidi wa uongo hupumua uongo.
Shahidi wa kweli huokoa maisha, bali shahidi wa uongo ni mdanganyifu.
26 Mtu anapokuwa na hofu ya Yehova, pia anakuwa na matumaini zaidi ndani yake; vitu hivi vitakuwa kama sehemu imara ya ulinzi kwa watoto wa mtu huyu.
Yeye amchaye Bwana ana ngome salama, na kwa watoto wake itakuwa kimbilio.
27 Kumcha Yehova ni chemchemi ya uzima, ili kwamba mtu aweze kujiepusha kutoka katika mitego ya mauti.
Kumcha Bwana ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.
28 Utukufu wa mfalme upo katika idadi kubwa ya watu wake, bali pasipo watu mfalme huangamia.
Wingi wa watu ni utukufu wa mfalme, bali pasipo watu mkuu huangamia.
29 Mtu mvumilivu anaufahamu mkubwa, bali mtu mwepesi wa kuhamaki hukuza upuuzi.
Mtu mwenye subira ana ufahamu mwingi, bali anayekasirika haraka huonyesha upumbavu.
30 Moyo wenye raha ni uzima wa mwili, bali husuda huozesha mifupa.
Moyo wenye amani huupa mwili uzima, bali wivu huozesha mifupa.
31 Anayemkandamiza masikini humlaani Muumba wake, bali anayeonyesha fadhila kwa wahitaji humtukuza yeye.
Yeye amwoneaye maskini huonyesha dharau kwa Muumba wao, bali yeyote anayemhurumia mhitaji humheshimu Mungu.
32 Mtu mwovu huangushwa chini kwa matendo yake mabaya, bali mtu mwenye haki anakimbilio hata katika kifo.
Waovu huangamizwa kwa matendo yao maovu, bali hata katika kifo wenye haki hupata kimbilio.
33 Hekima hukaa katika moyo wa ufahamu, bali hata miongoni mwa wapumbavu hujiachilia mwenyewe kwa kujulikana
Hekima hukaa katika moyo wa mwenye ufahamu bali haijulikani miongoni mwa wapumbavu.
34 Kutenda haki huliinua taifa, bali dhambi ni chukizo kwa watu wowote.
Haki huinua taifa, bali dhambi ni aibu kwa watu wote.
35 Fadhila ya mfalme ni kwa mtumishi mwenye kutenda kwa hekima, bali hasira yake ni kwa yule atendaye kwa kuaibisha.
Mfalme hupendezwa na mtumishi mwenye hekima, bali ghadhabu yake humwangukia mtumishi mwenye kuaibisha.