< Mithali 13 >

1 Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya baba yake, bali mwenye dhihaka hatasikiliza karipio.
Mwana mwenye hekima husikia mafundisho ya babaye, bali mwenye dharau hasikilizi maonyo.
2 Mtu hufurahia vitu vizuri kutokana na matunda ya kinywa chake, bali hamu ya wadanganyifu ni jeuri.
Kutoka tunda la midomo yake mtu hufurahia mambo mema, bali wasio waaminifu wanatamani sana jeuri.
3 Yeye anayelinda kinywa chake huyalinda maisha, bali anayefumbua sana midomo yake atajiangamiza mwenyewe.
Yeye alindaye midomo yake hulinda nafsi yake, bali yeye asemaye kwa haraka ataangamia.
4 Hamu ya watu wavivu ni uchu lakini hawapati kitu, bali hamu ya watu wenye bidii hutoshelezwa sana.
Mvivu hutamani sana na hapati kitu, bali nafsi ya mwenye bidii hutoshelezwa kikamilifu.
5 Atendaye haki huchukia uongo, bali mtu mwovu hukinzana mwenyewe, na kufanya ya kuaibisha.
Mwenye haki huchukia uongo, bali waovu huleta aibu na fedheha.
6 Wenye haki huwalinda wale ambao ni wakamilifu katika mapito yao, bali uovu huwaangusha wale watendao dhambi.
Haki humlinda mtu mwadilifu, bali uovu humwangusha mwenye dhambi.
7 Kuna mtu ambaye hujitajirisha mwenyewe, lakini hana chochote na kuna mtu ambaye hutoa kila kitu, bado ni tajiri kweli.
Mtu mmoja hujifanya tajiri, kumbe hana chochote; mwingine hujifanya maskini, kumbe ana utajiri mwingi.
8 Mtu tajiri anaweza kufidia maisha yake kwa mali zake, bali mtu masikini hatapokea kitisho cha aina hiyo.
Utajiri wa mtu waweza kukomboa maisha yake, bali mtu maskini hasikii kitisho.
9 Mwanga wa mtu atendaye haki hufurahia, bali taa ya waovu itazimika.
Nuru ya mwenye haki hungʼaa sana, bali taa ya mwovu itazimwa.
10 Kiburi huzaa mafarakano, bali kwa wale wasikiao shauri jema kuna hekima.
Kiburi huzalisha magomvi tu, bali hekima hupatikana kwa wale wanaozingatia ushauri.
11 Penye majivuno mengi utajiri hufifia, bali yeye apataye pesa kwa kufanya kazi kwa mkono wake pesa zake zitaongezeka.
Fedha isiyo ya halali hupungua, bali yeye akusanyaye fedha kidogo kidogo huongezeka.
12 Tumaini linapoachwa, huvunja moyo, bali kukamilishwa kwa shauku ni mti wa uzima.
Kilichotarajiwa kikikawia kuja moyo huugua, bali tumaini lililotimizwa ni mti wa uzima.
13 Yule ambaye anadharau fundisho bado atakuwa chini ya utawala wake, bali yeye ambaye anaheshimu amri atapewa thawabu.
Yeye anayedharau mafundisho anajiletea maangamizi, bali yeye anayeheshimu agizo hupewa tuzo.
14 Mafundisho ya mtu mwenye hekima ni chemchemi ya uzima, yanakuondoa kutoka kwenye mitego ya mauti.
Mafundisho ya mwenye busara ni chemchemi ya uzima, ili kumwepusha mtu na mitego ya mauti.
15 Busara njema huleta fadhila, bali njia ya wadanganyifu haina mwisho.
Ufahamu mzuri hupata upendeleo, bali njia ya asiye mwaminifu ni ngumu.
16 Watu wenye busara hutenda kwa maarifa kwa kila uamuzi, bali mpumbavu huonyesha upuuzi wake.
Kila mwenye busara hutenda kwa maarifa, bali mpumbavu hudhihirisha upumbavu wake.
17 Mjumbe mbaya huangukia kwenye shida, bali balozi mwaminifu huleta upatanisho.
Mjumbe mwovu huanguka kwenye taabu, bali mjumbe mwaminifu huleta uponyaji.
18 Yeye ambaye hupuuza kurudiwa atapata umasikini na aibu, bali heshima itamjia yeye ambaye hujifunza kutokana na masahihisho.
Yeye anayedharau maonyo hupata umaskini na aibu, bali yeye anayekubali maonyo huheshimiwa.
19 Shauku iliyotambuliwa ni tamu kwa hamu, bali wapumbavu huchukia kuacha uovu.
Tarajio lililotimizwa ni tamu kwa nafsi, bali wapumbavu huchukia sana kuacha ubaya.
20 Tembea pamoja na watu wenye hekima nawe utakuwa na hekima, bali rafiki wa wapumbavu atateseka.
Yeye atembeaye na mwenye hekima atapata hekima, bali rafiki wa mpumbavu hupata madhara.
21 Maafa huwakimbilia wenye dhambi, bali wale watendao haki hupewa thawabu kwa mema.
Balaa humwandama mtenda dhambi, bali mafanikio ni thawabu kwa mwenye haki.
22 Mtu mwema huacha urithi kwa wajukuu wake, bali mali ya mwenye dhambi huwekwa akiba kwa yule atendaye haki.
Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi, bali mali ya wenye dhambi imehifadhiwa kwa ajili ya wenye haki.
23 Shamba la masikini lisilolimwa linaweza huzalisha chakula kingi, bali huchukuliwa kwa udhalimu.
Shamba la mtu maskini laweza kuzalisha chakula kingi, bali dhuluma hukifutilia mbali.
24 Yeye ambaye hamrudi mwanawe humchukia, bali yule anayempenda mwanawe humjali kwa kumwadibisha.
Yeye aizuiaye fimbo yake hampendi mwanawe, bali yeye ampendaye huwa mwangalifu kumwadibisha.
25 Yeye atendaye haki hula hadi kutosheleza hamu yake bali tumbo la mwovu linanjaa daima.
Mwenye haki hula mpaka akaridhisha moyo wake, bali tumbo la mwovu hutaabika kwa njaa.

< Mithali 13 >