< Wafilipi 1 >
1 Paulo na Timotheo, watumishi wa Kristo Yesu, Kwa wale walitengwa katika Kristo wanaoishi Filipi, pamoja na waangalizi na mashemasi.
Waraka wa Paulo na Timotheo, watumishi wa Kristo Yesu: Kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu walioko Filipi, pamoja na waangalizi na mashemasi:
2 Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na Bwana wetu Yesu Kristo.
Neema na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana wetu Yesu Kristo iwe nanyi.
3 Namshukuru Mungu wangu kila ninapowakumbuka ninyi nyote.
Ninamshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo ninyi.
4 Mara zote katika kila ombi langu kwa ajili yenu ninyi nyote, huwa na furahi ninapowaombea.
Katika maombi yangu yote daima nimekuwa nikiwaombea ninyi nyote kwa furaha,
5 Nina shukrani nyingi kwa sababu ya ushirika wenu katika injili tangu siku ya kwanza mpaka leo.
kwa sababu ya kushiriki kwenu katika kueneza Injili, tangu siku ya kwanza hadi leo.
6 Nina hakika kuwa yeye aliyeanzisha kazi njema ndani yenu ataendelea kuikamilisha mpaka siku ya Bwana Yesu Kristo.
Nina hakika kwamba yeye aliyeianza kazi njema mioyoni mwenu, ataiendeleza na kuikamilisha hata siku ya Kristo Yesu.
7 Ni sawa kwangu kujisikia hivi juu yenu ninyi nyote kwa sababu nimewaweka moyoni wangu. Maana ninyi mmekuwa washirika wenza katika neema katika kifungo changu na katika utetezi na uthibitishaji wangu wa injili.
Ni haki na ni wajibu wangu kufikiri hivi juu yenu nyote, kwa sababu ninyi mko moyoni mwangu. Ikiwa nimefungwa au nikiwa ninaitetea na kuithibitisha Injili, ninyi nyote mnashiriki neema ya Mungu pamoja nami.
8 Mungu ni shahidi wangu, jinsi nilivyo na shauku juu ya yenu nyote katika undani wa pendo la Kristo Yesu.
Mungu ni shahidi wangu jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote kwa huruma ya Kristo Yesu.
9 Na ninaomba kwamba: upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote.
Haya ndiyo maombi yangu: kwamba upendo wenu uongezeke zaidi na zaidi katika maarifa na ufahamu wote,
10 Ninaomba kwa ajili ya hili ili muwe na uwezo wa kupima na kuchagua mambo yaliyo bora sana. Pia ninawaombea ili muwe safi pasipokuwa na hatia yoyote katika siku ya Kristo.
ili mpate kutambua yale yaliyo mema, mkawe safi, wasio na hatia hadi siku ya Kristo,
11 Na pia ili mjazwe na tunda la haki lipatikanalo katika Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.
mkiwa mmejawa na matunda ya haki yapatikanayo kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa za Mungu.
12 Sasa ndugu zangu, nataka mjue kuwa, mambo yaliyotokea kwangu yameifanya injili iendelee sana.
Basi, ndugu zangu, nataka mjue kwamba mambo yale yaliyonipata kwa kweli yamesaidia sana kueneza Injili.
13 Ndiyo maana vifungo vyangu katika Kristo, vimejulikana kwa walinzi wa ikulu yote na kwa kila mtu pia.
Matokeo yake ni kwamba imejulikana wazi kwa walinzi wote wa jumba la kifalme na kwa wengine wote kuwa nimefungwa kwa ajili ya Kristo.
14 Na ndugu wengi katika Bwana, kwa sababu ya vifungo vyangu, wameshawishika na kuthubutu kulihubiri Neno pasipo hofu.
Kwa sababu ya vifungo vyangu, ndugu wengi katika Bwana wametiwa moyo kuhubiri neno la Mungu kwa ujasiri zaidi na bila woga.
15 Baadhi kweli hata humtangaza Kristo kwa fitina na ugomvi, na pia wengine kwa nia njema.
Ni kweli kwamba wengine wanamhubiri Kristo kutokana na wivu na kwa kutaka kushindana, lakini wengine wanamhubiri Kristo kwa nia njema.
16 Wale wanaomtangaza Kristo kwa upendo wanajua kuwa nimewekwa hapa kwa ajili ya utetezi wa injili.
Hawa wa mwisho wanamhubiri Kristo kwa moyo wa upendo, wakifahamu kwamba nimo humu gerezani kwa ajili ya kuitetea Injili.
17 Bali wengine wanamtangaza Kristo kwa ubinafsi na nia mbaya. Hudhani kuwa wanasababisha matatizo kwangu katika minyororo yangu.
Hao wa kwanza wanamtangaza Kristo kutokana na tamaa zao wenyewe wala si kwa moyo mweupe, bali wanakusudia kuongeza mateso yangu katika huku kufungwa kwangu.
18 Kwa hiyo? Sijali, aidha njia ikiwa ni kwa hila au kwa kweli, Kristo anatangazwa, na katika hili ninafurahia! Ndiyo, nitafurahia.
Lakini inadhuru nini? Jambo la muhimu ni kwamba kwa kila njia, ikiwa ni kwa nia mbaya au njema, Kristo anahubiriwa. Nami kwa ajili ya jambo hilo ninafurahi. Naam, nami nitaendelea kufurahi,
19 kwa kuwa ninajua ya kuwa hili litaleta kufunguliwa kwangu. Jambo hili litatokea kwa sababu ya maombi yenu na kwa msaada wa Roho wa Yesu Kristo.
kwa maana ninajua kwamba kwa maombi yenu na kwa msaada unaotolewa na Roho wa Yesu Kristo, yale yaliyonipata mimi yatageuka kuwa wokovu wangu.
20 Kulingana na matarajio yangu ya uhakika na kweli ni kwamba, sitaona aibu. Badala yake, kwa ujasiri wote, kama ambavyo siku zote na sasa, natarajia kuwa Kristo atainuliwa katika mwili wangu, ikiwa katika uzima au katika kifo.
Ninatarajia kwa shauku kubwa na kutumaini kwamba sitaaibika kwa njia yoyote, bali nitakuwa na ujasiri wa kutosha ili sasa kama wakati mwingine wowote, Kristo atukuzwe katika mwili wangu, ikiwa ni kwa kuishi au kwa kufa.
21 Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo na kufa ni faida.
Kwa maana kwangu mimi, kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.
22 Lakini, kama kuishi katika mwili huzaa tunda katika kazi yangu, kwa hiyo sijui ni lipi la kuchagua.
Kama nitaendelea kuishi katika mwili, kwangu hili ni kwa ajili ya matunda ya kazi. Lakini sijui nichague lipi? Mimi sijui!
23 Maana ninasukumwa sana na mawazo haya mawili. Nina hamu ya kuuacha mwili na kuwa pamoja na Kristo, kitu ambacho ni cha thamani sana sana.
Ninavutwa kati ya mambo mawili: Ninatamani kuondoka nikakae pamoja na Kristo, jambo hilo ni bora zaidi.
24 Ingawa, kubaki katika mwili huu ni jambo la muhimu sana kwa ajili yenu.
Lakini kwa sababu yenu ni muhimu zaidi mimi nikiendelea kuishi katika mwili.
25 Kwa kuwa nina uhakika juu ya hili, ninajua nitabaki na kuendelea kuwa pamoja nanyi nyote, kwa ajili ya maendeleo na furaha ya imani yenu.
Kwa kuwa nina matumaini haya, ninajua kwamba nitaendelea kuwepo na kuwa pamoja nanyi nyote, ili mpate kukua na kuwa na furaha katika imani.
26 Na hii italeta furaha yenu kubwa katika Kristo Yesu, kwasababu yangu itaongezeka, kwa sababu ya uwepo wangu tena pamoja nanyi.
Ili kwamba furaha yenu iwe nyingi katika Kristo Yesu kwa ajili yangu kwa kule kuja kwangu kwenu tena.
27 Mnatakiwa kuishi maisha yenu katika mwenendo mzuri uipasayo injili ya Kristo. fanyeni hivyo ili nikija kuwaona au nisipokuja, nisikie kuwa mmesimama imara katika roho moja. natamani kusikia kuwa mna roho moja, mkiishindania imani ya injili kwa pamoja.
Lakini lolote litakalotukia, mwenende kama ipasavyo Injili ya Kristo, ili kwamba nikija na kuwaona au ikiwa sipo, nipate kusikia haya juu yenu: Kuwa mnasimama imara katika roho moja, mkiishindania imani ya Injili kwa umoja,
28 na msitishwe na kitu chochote kinachofanywa na maadui zenu. Hii kwao ni ishara ya uharibifu. Bali kwenu ni ishara ya wokovu kutoka kwa Mungu.
wala msitishwe na wale wanaowapinga. Hii ni ishara kwao kuwa wataangamia, lakini ninyi mtaokolewa, na hii ni kazi ya Mungu.
29 kwa maana ninyi mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, bali na kuteswa pia katika Yeye.
Kwa maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, bali pia kuteswa kwa ajili yake,
30 kwa maana mna mgogoro uleule kama mliouona kwangu na mnasikia kwamba ninao hata sasa.
kwa kuwa mnashiriki mashindano yale yale mliyoyaona nikiwa nayo na ambayo hata sasa mnasikia kuwa bado ninayo.